google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATIMA YAKO, MAISHA YAKO

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 12.07.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: HATIMA YAKO, MAISHA YAKO.

Tunajifunza juu ya hatima kwa sababu maisha ya mtu yamefungwa katika hatima. Hatima ya mtu ilianza kabla hajazaliwa; imeandikwa katika Zaburi 139:16, “Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.” Mungu alitujua kabla hatujatungwa mimba, na kwamba siku zetu zimeandikwa katika kitabu cha Mungu. Mtu ataanzia wapi na ataishia wapi, imeshaamuriwa na Mungu mwenyewe (Yeremia 1:5). Yeremia aliwekwa kuwa nabii wa mataifa kabla hajatungwa mimba.

Mungu ndiye anaweka watu “kuwa”. Kwenye kitabu cha Mungu Yeremia anasomeka kuwa nabii wa mataifa. Kwakuwa Mungu ndiye amemuweka kuwa nabii wa mataifa, Mungu anaandaa na watu wa mataifa watakaomsikiliza Yeremia. Kabla hatujaumbwa / kuzaliwa na mama zetu, taarifa zetu zipo kwenye kitabu cha Mungu kama ambavyo imeandikwa katika Isaya 34:16. Yale yaliyoandikwa na Mungu kuhusu mtu, hayo ndiyo mafanikio ya mtu, kusudi la mtu au hatima ya mtu. Maisha ya mtu ndiyo hatima yake, na ni lazima yatimie.

Watu wote tupo kwenye kitabu cha Mungu. Tukijitafuta kwenye kitabu cha Mungu tutajipata; mkulima, mtoto, mfanyabiashara, mfanyakazi, n.k. wote wapo kwenye kitabu cha Bwana. Ndani ya kitabu cha Bwana, huduma, hatima, kazi, biashara, ndoa na vyote vinapatikana. Ukishindwa kujitafuta, siyo kosa la Bwana bali ni kosa lako mwenyewe.

Danieli alisoma kitabu cha Bwana kilichoandika hatima yao ya kurudishwa kwa watu wa Yerusalemu kutoka katika nchi ya ukiwa. Alipojitafuta na kujipata, Danieli alimgeukia Mungu kwa maombi na kufunga ili ahadi ya Mungu juu yao itimie (Danieli 9:2). Ukishaona yale mambo ya kukaa kwenye dhiki yamekoma, taka kwa Bwana kurudi kwenye nchi ya maziwa na asali; taka nguvu za Bwana, taka miujiza ya Bwana.

Mtu anaweza kuwa kwenye wakati ambao Mungu amemuandikia aende kwenye kusudi lake, lakini kwa sababu ya kutokusoma kitabu cha Bwana, mtu huyo anakuwa amefichwa jangwani. Siku zote unatakiwa kujiweka karibu na Mungu ili uweze kujua wakati ambao Mungu amekuamuria kama ulivyoandikiwa.

Shida kubwa iliyopo ni kuwa, watu wengi hawapendi kusoma. Baba yetu, ASKOFU DR. Josephat Gwajima ametuandikiwa vitabu vingi vyenye maarifa ya kila aina yanayomgusa kila mtu. Mfano, Silaha za Vita Vyetu, Maombi ya Kushindana, Jinsi ya Kufufua Wafu, Mkate wa Kila Siku, Ushindi Kwa Damu ya Yesu, Matukio Katika Damu ya Ukoo, n.k. Ukisoma vitabu hivi unapata maarifa ya kupambana na kushinda vita inayokukabili. Shida yako uliyonayo kaisome kwenye vitabu vya baba; katafute katika kitabu cha Bwana maana hakuna jambo hata moja ambalo utalikosa. Wafanyabiashara wameandikiwa, wakulima pia; kwa mfano, Yesu anasema yeye ni mzabibu wa kweli na Baba yake ni mkulima, na kwamba tawi lisilozaa huliondoa (Yohana 15:1-2).

Je, ni nini maana ya maisha? Unazaliwa, unasoma, unapata kazi, unastaafu kazi na kupewa kiinua mgongo, kiinua mgongo kinaisha, unakufa. Siyo sawa. Lipo kusudi la maisha; yampasa mtu kutafuta kwenye kitabu cha Bwana. Mafanikio ya mtu na anguko la mtu yapo ndani ya kitabu; chagua vizuri kitabu cha kusoma na kitabu cha kusomewa. Kuna kitabu ukisomewa anguko lako linaanza na maisha yako yanaharibika, kama vile, biashara inaharibika, kazi inaharibika, ndoa inaharibika, na mambo mengine yanaharibika, lakini kipo kitabu ambacho ukisomewa kila kitu kinakaa sawa. Jambo la msingi ni kujua unasomewa kitabu gani na ni cha nani. Kuna kitabu cha Mungu lakini pia vipo vitabu vya kichawi / waganga. Vitabu vya kichawi / waganga ni vitabu vya uharibifu (Matendo ya Mitume 19:19).

Mungu anakitabu kimoja tu lakini waovu / wachawi wana vitabu vingi. Siyo wingi wa vitabu unaoleta mafanikio; tafuta mafanikio katika kitabu cha Bwana. Ni mambo gani kuhusu uzao, shule, mafanikio, yaliyoandikwa kwenye vitabu vya waganga juu ya mtu? Ni kitu gani kilichoandikwa? Wapo wachawi / waganga ambao wameboresha kabisa vitabu vyao wakatengeneza kuwa vya kielekroniki ili kufanana na vya watumishi wa Mungu. Unaweza ukakuta mtu yupo ibadani anatumia kishikwambi (ipad) ukadhani anasoma kitabu cha Mungu kumbe ana kitabu cha kichawi anasoma. Imeandikwa katika 2 Wakorintho 2:11 kuwa “…” na imeandikwa katika Luka 3:4 kuwa “…”.

“Kila kitabu cha kichawi kuharibu maisha ya mtu, kuharibu taifa, kuharibu kanisa, kuharibu kazi, kuharibu ndoa tunavichoma moto, kwa jina la Yesu! Ninachoma moto kila kitabu cha wachawi kilichoandikwa kuharibu maisha yangu, kitabu chochote kilichoandikwa kuharibu masomo yangu, ninakichoma moto kwa damu ya Yesu; kitabu chochote cha kichawi kilichoandikwa kuharibu miradi yangu, kuharibu kampuni yangu, kuharibu kazi, nakichoma moto; ninachoma moto vitabu vya ukoo, ninavichoma moto vitabu vya waganga, ninavichoma moto vitabu vya magonjwa, ninavichoma moto vitabu vya vifungo, ninavichoma moto, kwa jina la Yesu!”

Kuna vitabu vya kuharibu mambo kabla hayajatokea katika ukomavu. Mtu anayekusomea vitabu humuoni ila yanaonekana matokeo tu. Mfano; unaanza biashara kwa ukamilifu wa kila kitu, unafanya matangazo kwa njia nyingi za kukuletea wateja lakini hupati wateja. Matangazo ni muhimu sana lakini hayatoshi; katafute katika kitabu cha Bwana yale uliyoandikiwa. Baba yetu alitafuta katika kitabu cha Bwana akajipata na akatangaza kuwa hakuna wa kuzuia mpaka yatimie. Ufufuo na Uzima hatuna bango lolote la kuhamasisha watu kuja kanisani, lakini watu maelfu huja kanisani; kuna kitabu kimeandika.

Katafute katika kitabu cha Mungu mambo yale yanayokuhusu wewe mwenyewe, uyaombee na uyasimamie. Usitafute mambo ya watu wengine maana hayatakusaidia. Daudi anasema katika kitabu cha Zaburi 37:25, “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.” kama Daudi asemavyo, nami katika umri huu, sijawahi kuona mtu mbea amefanikiwa kwa umbea wake, wala umbea kuleta chakula nyumbani; tafuta ya kwako uliyoandikiwa.

Wale wanaotafuta ya wengine na kuyasema, mfano, “fulani anajifanya wa kiroho sana na kujifanya ananena nena sana kwa lugha,” yakikutokea wewe ongeza bidii zaidi kwa maana imeandikwa katika Warumi 1:16, “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”

Ukiona mtu anaomba / anafunga, jua anafanya hivyo kwa ajili yake na uzao wake na kuyatafuta yale aliyoandikiwa. Binadamu hawana cha kukupa; anayewalipa watu sawa na matendo yao siyo binadamu ni Mungu (Ufunuo 20:12). Yesu mwenyewe alisemwa, alidhihakiwa na kuambiwa amepagawa wakati akifanya yale aliyoandikiwa; hata katika Sinagogi akifundisha, wazazi wake hawakutaka kumsikiliza. Hakuna makosa kwa kutendewa mambo na watu; jipime katika kitabu kilichoandika mambo yako. Watu wasikuamurie mambo yako.

Kuna watu huamuriwa na wazazi wao wabaki kwenye dini ya wazazi wao itakayowazika. Sisi ni roho, tuliotolewa na Bwana na tutarudi kwake. Miili yetu haituamurii mambo yetu; tunalifuata kusudi vilevile tulivyoandikiwa, na kama tukitoka ndani ya miili iliyotubeba, wanaobaki (hao ndugu zetu katika miili) wataamua wenyewe kuizika miili au iwanukie. Undugu siyo kwa sababu ya miili iliyotubeba, la hasha! Ndugu zetu ni wale tunaoshiriki pamoja hatima zetu.

Kuna muda upendo wa wazazi ni kikwazo kwa mtoto kuishi hatima yake hapa duniani. Ndugu wanaweza kukuzuia usiende kwenye hatima yako; huruma ya mwanadamu inaweza ikamzuia mtu asiende kwenye hatima yake. Huruma ya binadamu ni kikwazo cha huruma ya Mungu kwa mtu. Unapozuia huruma ya Mungu unazuia muujiza wa Mungu, mfano, mtu mgonjwa akihurumiwa kwa sababu ya kuumwa kwake, eti, “usiende kanisani kwa sababu unaumwa” huruma hiyo inafunga neno la uponyaji, kwa maana imeandikwa katika Mathayo 4:24 “Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.” Wakamletea ni kitendo cha imani cha kuamini Mungu yupo huko unakowapeleka wagonjwa; huko ndiko kwenye huruma ya Mungu.

Huruma ya Mungu ndiyo inasababisha miujiza ya Mungu; ruhusu huruma ya Mungu itende kazi kwako. Kuna upotoshaji umezoeleka na washirikina kuwa jisaidie kwanza na Mungu atakusaidia au jihurumie na Mungu atakuhurumia. Huruma ya Mungu inatutaka tumtumikie Mungu kwanza. Kitu chochote au hali yoyote isizuie kumtumikia Mungu kwa maana haanzi Mungu kumhurumia mtu ila tunaanza sisi kwanza kumtumikia Mungu halafu anatuhurumia. Hakuna kumtumikia Mungu, hakuna huruma ya Mungu, kwa maana imeandikwa katika Kutoka 23:25 kuwa, “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.”

Mungu ameweka kusudi ndani ya mtu; unapotembea, tembea na kusudi lake (Wafilipi 1:6). Hatutafuti cha kufanya kwa maana kilishawekwa ndani yetu (Waefeso 2:10). Imeandikwa katika Mhubiri 3:11 kuwa, “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.” Moyo unaoongelewa hapa ni kumaanisha mtu wa ndani ambaye ni roho.

Maisha ya Mtume Paulo: akiitwa Sauli, alikuwa muuaji akitekeleza maandiko ya Mafarisayo. Alisimamia zoezi la kumpiga mawe Stefano kwa maana vitabu vya Mafarisayo viliandika hayo; vitabu alivyosoma hapo awali vilimfanya awe muuaji (Matendo ya Mitume 7:58-60, Matendo ya Mitume 8:3). Akipandacho mtu ndicho atavuna, Paulo naye alipigwa mawe (Wagalatia 6:7).

Paulo alichambuka akalijua kusudi la maisha yake lile aliloandikiwa tangu tumboni mwa mama yake, ambalo ni kupeleka injili kwa mataifa kwa hali yoyote (Wagalatia 1:15). Yakupasa uchambuke na uijue neema ya Bwana juu yako. Changamoto ipo kwa watu kutojua jinsi Mungu anavyofanya kazi; wamefumbwa wasijue / wamepofushwa (2 Wakorintho 4:3-4). Madhara ya kufumbwa yanaweza kupelekea kumtenda vibaya mwenye hatima yako au kumfyeka unayemtafuta (Luka 24:13-17, Marko 16:12-13, Yohana 20:11-31).

Unachokitafuta kipo kwa watu, tatizo umefumbwa; katafute katika kitabu cha Bwana. Kuna watu wakiambiwa neno hawaliamini, mfano, wanamuacha Yesu ili wakamtafute Yesu. Mambo ya Mungu siyo ya kimantiki, ila ni ya kuamini. Hatuyafuati kwa sababu tunayaelewa; tunayafuata kwa sababu tunayaamini (Warumi 10:17, Isaya 53:1-5). Maombi yale yale, mfungo ule ule, kuna watu wanajibiwa na kupata na wengine hawapati. Tofauti siyo kuelewa ila ni kuamini; usiache kuomba.

Yesu aliyedharauliwa na kuaibika, hatima yake imeisha vizuri akipaa kwenda kwa Baba yake ambaye ni Baba yetu pia kwa utukufu sana kwenye mlima wa Mungu huku watu wengi wakimtazama; ni hivyo hata kwetu. Tuna hatima kubwa ila tumetengenezewa sababu ya kuingia kwenye matatizo. Anayetengeneza matatizo hatoki mbali, ni ama ndugu, ama mwanafamilia. Maisha yaliyopindishwa aliyonayo mtu siyo mwisho wake, yapo hivyo kwa kutojua alichoandikiwa; omba neema ya Mungu kuyaishi uliyoandikiwa, kwa jina la Yesu.

Adui anaweza akaiona hatima ya mtu bila mtu huyo kuijua, akamsomea kitabu na kumpeleka mbali na hatima yake; huko ndiko kutupwa nyuma ya jangwa. Wanachologa wachawi ni hatima ya mtu ili awe dhaifu na kukosa sifa ya kuyaishi yale aliyoandikiwa. Kwanini upo kwenye matatizo? Upo kwenye matatizo kwa sababu, hatima yako kubwa ambayo adui ameiona imepelekea utengenezewe matatizo, lakini kwenye kitabu cha Bwana hatima yako kubwa ina mwisho mwema na heshima kubwa.

Kisa cha Yeftha ni mfano mzuri wa mtu mwenye hatima kubwa aliyetengezewa zengwe na ndugu zake (Waamuzi 11:1-5). Yeftha mtoto wan je ya ndoa, aliyezaliwa kwa kahaba, akatengwa na ndugu zake. Huiondoi hatima ya Yeftha maana imeandikwa kwenye kitabu cha Bwana. Kuna watu wanatendewa mabaya na ndugu zao kwa sababu tu wamefiwa na wazazi; kufiwa hakuzuii hatima ya mtu. Usimtendee mtu mabaya kwa maana huijui hatima yake; ipo siku utamuhitaji mtu huyo. Ukipelekwa nyuma ya jangwa nenda na hatima yako, na ukitoka nyuma ya jangwa utoke na hatima yako.

Hatima pia hufungamana na watu wengine. Mungu anaweza akaweka hatima kubwa kwa mtu ili awabebe wenzake. Usimpige vita mwenye hatima hiyo kwa maana mafanikio yake yatakuja kukuinua na wewe. Yeftha baada ya kutengwa na ndugu zake, alitafutwa badae na hao hao ndugu zake kwa ajili ya kuwasaidia vitani; Yeftha akawa kichwa chao.

Hakuna jambo jepesi; hata huduma siyo nyepesi. Ukipelekwa nyuma ya jangwa usikate tamaa, pigania hatima yako. Hata Ufufuo na Uzima tulipelekwa nyuma ya jangwa kwa miezi sita, mahali petu pakakaliwa na maaskari lakini Mungu akaturudisha. Vivyo hivyo, kama ambavyo Mungu alirudisha hatima ya kanisa, atarudisha hatima ya mtu mmoja mmoja. Usikubali kukaa jangwani; itake hatima yako kwa maana iko neema ya kurejea kwenye hatima yako.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments