google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATIMA YAKO, MAISHA YAKO

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 02.08.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: HATIMA YAKO, MAISHA YAKO

“Tukikumbuka tulikotoka, kuambatana kunaongezeka!”

Kwa nini somo juu ya hatima linafundishwa sana? Sababu ni moja, kuwa hatima ya mtu na maisha ya mtu vimefungwa pamoja. Tunapambana sana kila siku ili kukidhi maisha ya kila siku. Kwenye hatima ya mtu kuna mahitaji ya mtu ya kila siku. Majibu ya mahitaji ya mtu yapo kwenye hatima ya mtu. Hatima ni kusudi la kuumbwa mtu; lilitangulia kusudi akafuata mtu. Kile unachokiita “natafuta maisha” ni unatafuta hatima. Mtu anapozaliwa anazaliwa angali hatima yake ipo. Uwezo wa mtu kuishi maisha yake, ndiyo uwezekano wa mtu kuishi hatima yake.

Vita ya hatima ni kubwa kuliko vita zote. Mitego ya adui iko ndani ya hatima ya mtu. Unaweza ukashambuliwa na adui kabla hujajua hata hatima yako. Mtu haanzi anapozaliwa; adui huiona hatima ya mtu hata kabla mimba ya mtu haijatungwa. Adui anaweza akaloga tumbo ili mtu atakayezaliwa asiishi hatima yake, yaani azaliwe na mapungufu. Mtu azaliwapo na mapungufu hayo, watu husema, “ana tatizo la kuzaliwa” lakini ni uongo, hizo ni hila za shetani (Yohana 9:1-3).

Adui anakuzuia sawasawa na hatima yako ilivyo. Hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya; ulimwengu wa roho hauna bahati mbaya. Imeandikwa katika Isaya 34:16, kuwa “Tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya.”. Kila hatima ya mtu imeandikwa kwenye kitabu cha Bwana. 

Kila mtu anapatikana kwenye kitabu cha Bwana; rafiki, ndugu, mume, mke, mfanyabiashara, mkulima, mfanyakazi, mtoto, wote wako ndani ya kitabu cha Bwana. Ukitafuta kwenye kitabu cha Bwana utajipata, na ukimtafuta yeyote utampata naye. Ongoza watu / majirani zako wajipate; huu ni ujasiri unaofanya makuhani wa Bwana wasimame madhabahuni kulisema neno la Bwana, maana walishajipata kwenye kitabu cha Bwana, nao wanawaongoza wengine ili wajipate au wawapate

Ndio maana sasa kwa kuwa wote wanapatikana hakuna hata mmoja asiyekuwa na kazi kama ilivyoandikwa katika Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”.

Kila aliyeumbwa na Mungu ameumbiwa kazi njema. Kila kusudi jema ni kazi njema ya Mungu ndani ya mtu, na Mungu ndiye aliyeiweka ndani ya mtu, naye Mungu ndiye mwenye jukumu la kuisimamia kazi hiyo na kuilinda. Kitendo cha kusikiliza neno la Mungu ni kitendo cha kuanza kazi iliyo ndani yako (Waefeso 2:10). Kazi, ambayo ni kusudi jema la Mungu, tuliumbiwa nayo, na tulizaliwa nayo; mtu anapozaliwa, yu na kusudi la Mungu.

Katika jamii zetu, kuna shughuli za kijamii ambazo tunapozaliwa, tunakuta wazazi wetu wakizifanya. Shughuli hizo ni kama, ufugaji, kilimo, biashara n.k. Wazazi wengi huwa wanapambana watoto wao wafanye kazi au shughuli ambazo wao wanafanya. Mzazi hupima utii wa mtoto kwa kuona mtoto anafanya vile ambavyo mzazi anataka; wazazi wa kimwili wanalazimisha watoto wao kuwa vile wanavyotaka wazazi. Kama baba ni mfugaji, atataka mtoto kuwa mfugaji na atapima mafanikio ya mtoto kwa uwezo na wingi wa mifugo aliyonayo. Hata kwenye taaluma, biashara, kilimo, wazazi huwapeleka watoto wao kwenye malengo hayo. Matokeo ya matakwa ya wazazi kwa watoto wao ni kuliweka kusudi la Mungu pembeni na kufanya yale wazazi wao hutaka wafanye

Kazi ya Mungu ndani ya mtu haiendani kabisa na vipaumbele vya wazazi wa kimwili. Kuna kusudi ambalo mtu analipata au kazi ambayo mtu anapata kupitia elimu yake, biashara yake, kilimo chake, shughuli zake, kwa sababu cha muhimu ni kupata mahitaji. 

Katika agano la kale (kitabu cha Isaya), Yesu alitabiriwa kuzaliwa, na mahitaji ni kuibeba dunia mabegani mwake, kuteswa, kufa na kufufuka; yote hayo ni kabla hajazaliwa. Bahati mbaya, Yesu akazaliwa kwenye familia ya seremala. Tunajiuliza, kwanini Yesu azaliwe kwenye nyumba ya seremala na siyo kwenye nyumba ya kuhani ikiwa kazi yake ni injili kama ilivyotabiriwa? Hivyo ndivyo ilivyompendeza Mungu. Sisi siyo wa kwanza kuzaliwa kwenye familia zilizo tofauti na kazi zetu ndani yetu. 

Haijalishi umezaliwa wapi au umeshushiwa wapi, ila muhimu ni lile kusudi jema ndani yako ambalo Bwana ameliweka ndani yako kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Seremala anawezakuzaa kuhani mbeba hatima ya ulimwengu mzima na mhubiri. Haijalishi mtu amezaliwa na nani katika mwili huu, hatima iko ndani ya mtu; yampasa / yatupasa kuiamsha, kwa jina la Yesu! (Luka 17:21). Aliyeianza kazi anaisimamia mwenyewe, anailea mwenyewe, anailinda mwenyewe na anaifikisha mwenyewe. Ukifanya kazi iliyo ndani yako, ni agizo la Bwana, naye anawajibika kukulinda mpaka kazi itimie “na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mathayo 28:20.

Yesu akazaliwa chini ya seremala, akawa fundi seremala, na akafahamika kwa useremala. Hata hivyo, Yesu alipoanza kufanya kazi aliyoandikiwa, aliwashangaza wengi katika jamii yake, waliojiuliza amepata wapi Hekima na miujiza aliyofanya (Mathayo 13:54-57). Wao walimjua tu kama seremala; “amepata wapi” inamaanisha kazi iliyowekwa ndani yake hawakumjua aliyemuwekea. “Amepata wapi” ni amewekewa ndani yake na Baba yake.

Mambo ya Yesu kuwashangaza watu yameongelewa pia katika kitabu cha Marko 6:1-3; hii inatufundisha kuwa kuna watu wapo wanafanya mambo mengi ambayo siyo kusudi la maisha yao na hawajui, na hawatafuti katika kitabu cha Bwana kujua.

Wale ambao hawajaandikiwa na kuwekewa hawawezi kuyafanya yale ayafanyayo yule aliyeandikiwa na kuwekewa na Bwana ndani yake. Familia haiwezi kujadili wokovu wa mwanafamilia na kazi iliyowekwa na Bwana ndani yake; ukiona wanaanza kukujadili juu ya wokovu wako, mfano, maneno kama “mbona mienendo yake siyo kama dini ya wazazi wake” jua umeanza kuwashangaza. Yesu anashangaza; ukifanya kazi isiyoshangaza, jua bado una kazi. Mtume Petro hakuwa mwenye elimu, alizaliwa kwenye jamii ya uvuvi lakini alitenda muujiza kwa jina la Yesu na watu wakashangaa sana (Matendo ya Mitume 3:6-11). Petro alishangaza kwa sababu alifanya kazi iliyoanzishwa na Yesu ndani yake, naye Yesu anailinda; elimu haishangazi.

Anza kudhihirisha ile kazi iliyo ndani yako. Wakikosa kujua umepata wapi uwezo huo, watakujia kwa sura ya kukuchukia. Adui asipojua mambo yako yamepatikana wapi, hawezi kuzuia. Angalia sana watu wanaokusifia; wanakutengeneza ili utoe siri yako / zako, wakuangamize. Mafarisayo walimtega Yesu ili wajue nguvu zake ziko wapi lakini hawakuweza (Mathayo 21:23-27).

Lazima ulinde siri. Siyo kila watu wanatakiwa kujua mambo yako. Kuna wakati mtu anashindwa kufikia hatua fulani kwa sababu ya kushindwa kuzuia taarifa muhimu za mambo yake muhimu. Samsoni ni mmoja wa anguko la kushindwa kuzuia taarifa muhimu. Wafilisti hawakujua nguvu za Samsoni zinatoka wapi, hivyo hawakuweza kumshinda Samsoni. Wafilisti wakakaa mbali na Samsoni ila wakamtuma Delila akachunguze chanzo cha nguvu za Samsoni.

Siyo kila ajaye kwenye maisha yako ana kusudi jema; wapo huja ili kukuangusha / kukuangamiza; omba neema ya Mungu kushinda, na yeyote asiye sahihi aondoke kwenye maisha yako wala asiyakaribie. Delila ni mtego wa Wafilisti kwa Samsoni. Kila nyuma ya mtego kuna jeshi kubwa lenye dhamira ya kukuangamiza.

Adui hatanii. Delila anajaribu mara kadhaa kujua chanzo cha / asili ya nguvu za Samsoni bila mafanikio, lakini hakati tamaa. Baada ya kujaribiwa sana, Samsoni anatoa siri ya asili ya nguvu zake; hilo likawa aguko lake. Kutokuwa na siri juu ya asili yako ni tatizo; adui akijua asili yako atakufunga. Linda ulichopewa na Bwana.

Ni muhimu ujijue wewe mwenyewe na ujue kujielezea. Tafuta kwenye kitabu cha Bwana yale yanayokuhusu; usitafute ya wengine. Ilikuwa ni desturi ya Yesu kwenda katika sinagogi. Siku moja alipoenda katika sinagogi alipewa kitabu kusoma, naye Yesu akatafuta mahali alipoandikiwa mambo yake tu, akasoma (Luka 4:16-22).

Yesu alijijua zaidi ya walivyomjua kuwa seremala. Aliyajua aliyoandikiwa. Hakuandikiwa kuwa seremala; yesu alichambuka akajijua. Nasi leo yatupasa tuchambuke tuache ambayo hatukuandikiwa tuyaendee tuliyoandikiwa na tuyatende. Watu wengi wamenaswa kwenye shughuli za wazazi wao bila kujua kusudi mama lililowekwa ndani yao. Kuna watu wengi wamejipa kazi ya kufanya majukumu ya kufurahisha watu wengine; mfano, kuwa kiongozi wa ukoo.

Sisi tuna wito wa kutenda kazi ya Bwana. Wito wa mtu kwa Mungu wake hauhitaji vikao vya mashauriano na watu, ndugu au wazazi, kwa maana imeandikwa katika Wagalatia 1:15 kuwa, “Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,”. Wale wanaozuia usifuate wito wako, ndiyo hao hao siku moja utakuwa msaada kwao. Acha yasiyokupasa uyaendee uliyoandikiwa; Musa alikataa kuitwa mwana wa binti Farao akaliendea kusudi lake (Waebrania 11:24-26).

Sehemu isiyo na vita ni kambi ya adui. Asiye na vita amekubali ushirika na adui; sisi tumekataa ushirika na adui. Kanisa la Bwana limejengwa juu ya mwamba; chochote kutoa kuzimu tunayo amri ya kukiambia kaa chini.

Haijalishi umezaliwa lini, nenda katafute ulipoandikiwa. Yesu aliandikiwa miaka 700 kabla hajazaliwa, lakini alipozaliwa alienda katika sinagogi akasoma yale aliyoandikiwa. Yale aliyosoma Yesu aliandikiwa katika “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;” Isaya 61:1-2.

Sauli mzaliwa wa familia ya Kishi yenye shughuli za ufugaji, kazi yake iliwekwa ndani yake na Bwana ya kuwa atakuwa mfalme wa Israeli. Ili Sauli afikie kusudi hilo, ililazimu punda wapotee na Sauli apewe jukumu la kwenda nyikani kutafuta punda waliopotea (1 Samweli 9:1, 10:1). Njia ya kufikia kusudi ilishaandikwa. Kuna muda matatizo na changamoto za mtu ni sababu tu ya kumfikisha kwenye kusudi lake. Usimdharau mtu; hujui kesho yake. Sauli akaambatana na mtumishi mmoja kwenda kuwatafuta punda waliopotea, wasiwapate hata Sauli akakata tamaa na kutaka kurudi lakini yule mtumishi akamsisitiza kumtafuta muonaji awasaidie; wakati mwingine hatima inahitaji kushurutishwa ili itimie. Walipomuona muonaji /Samweli, Sauli alipokelewa siyo kama aliyepoteza bali kwa Samweli Sauli alionekana ni mtu mkubwa aliyesubiriwa kumiminiwa mafuta awe mfalme wa Israeli. Maisha yanahitaji watu; tafuta watu wa uhakika na uwaheshimu.

Mtumishi aliyeambatana na Sauli naye anapokelewa vizuri pamoja na Sauli; ambatana na muombee mwenye hatima kwa maana kupenya kwake ni kupenya kwako. Sauli anamiminiwa mafuta kuwa mfalme, siyo kwa sababu ya elimu au uzoefu, ila ni kwa sababu ya asili aliyoiweka, na kuwapa uwezo kutumika wale aliowaita na kufanya kazi pamoja nao aliowachagua; Mungu siyo wa uzoefu.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments