google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAPELELEZI WA HATIMA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 09.08.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: WAPELELEZI WA HATIMA

Hatima ya mtu ndiyo maisha ya mtu. Wapelelezi siyo jambo geni kulisikia na ni jambo zuri; hata kwenye biblia Mungu hutambua wapelelezi. Taarifa kutoka kwa wapelelezi juu ya upelelezi waliofanya ni jambo la kuzingatia sana. Nchi zina wapelelezi, taasisi pia. Zamani za wazee wetu, mtu akitaka kuoa walitumwa wapelelezi ili kujua siri fulani muhimu za ukoo na familia husika; mfano, ikiwa ukoo una ukoma au kama ukoo ni wa hovyo. Upelelezi unatumika kwenye mambo mengi ili kufanya maamuzi sahihi.

Kimsingi kwenye taasisi kuna wapelelezi wa aina tano; -

1.   Wapelelezi wakazi wa eneo (Local spies): Hawa ni wenyeji wa eneo ambao hutoa taarifa muhimu bila kujua kama wanapelelezwa. Hutangulia kwa kusifiwa (wanajazwa) halafu wanalewa sifa na kuanza kutoa siri.

2.   Wapelelezi wa ndani (Inward spies): Hawa ni wapelelezi ndani ya taasisi husika inayopelelezwa; ni waajiriwa. Kwa kadiri wanavyofanya kazi ndiyo wanavyopeleleza. Kwa mfano, hata hapa kanisani yawezekana kabisa wapo na wamejiunga kwenye madarasa ya baba au Glory Choir, au Wana wa Asafu na wanahudumu kabisa, lakini wanapeleleza mambo ya hapa kanisani na kupeleka kwa waliowatuma.

3.   Wapelelezi Wajinga (Doomed spies): Hawa ni wapelelezi wasio na maarifa ambao mara nyingi hugundulika na kupewa taarifa za uongo.

4.   Wapelelezi walioongoka (Converted Spies): Hawa ni wapelelezi waliotumwa kupeleleza eneo Fulani lakini wenyeji wa eneo hilo ama wakawatendea wema au wakawashawishi mpaka wakaanza kutoa siri za waliowatuma.

5.   Wapelelezi waliofanikiwa / walionusurika (Surviving Spies): Hawa ni wapelelezi waliofanikiwa kupata taarifa na kuzipeleka zinakohitajika / kwa waliowatuma.

Upelelezi upo kila mahali hata kwenye biblia umeelezwa. Katika biblia, kwa mfano, Mungu anamwambia Musa apeleke watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani (Hesabu 13:1-3). Hapa tunaona kuwa upelelezi halikuwa wazo la Musa ila ni wazo la Mungu anayeijua hiyo nchi na kuwajua wenyeji wake.

Musa akakusanya vichwa kumi na mbili kutoka katika kabila kumi na mbili za wana wa Israeli, ambao walienda kuipeleleza Kanaani na kuleta taarifa kwa Musa. Kuna wakati taarifa ya upelelezi inaweza ikakukatisha tamaa; taarifa ya upelelezi wa Kanaani ilitolewa kwa jamii yote ya wana wa Israeli bila siri, na ile ya wale kumi isipokuwa Kalebu na Yoshua iliwahuzunisha sana maana iliwavunja moyo. Taarifa ya upelelezi iliyowatia moyo ni ile ya Kalebu na Yoshua ambayo iliwapa nguvu wana wa Israeli kuwa Mungu ameyeyusha mioyo ya Wakanaani na kuwa wanaweza kushinda vita; walitoa taarifa ya ushawishi wa mioyo yao, hata walipotaka kudhuriwa Bwana aliwaokoa.

Tunajifunza kuwa, Bwana haangalii wingi wa watu ili aokoe; yeye ni Mungu wa mmoja aliye kwenye njia ya kweli. Mungu hushuka na kusimama pamoja na mtu aliye kwenye njia ya kweli dhidi ya maadui zake. Hasira ya Bwana iliwaka dhidi ya taarifa ya wale wapelelezi wapotoshaji. Siku zote angalia taarifa ya Bwana; usiangalie ni hali gani utakayoambana nayo, kama ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume 27:25 kuwa, “Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”. Mungu akikwambia nenda, wewe nenda kwa maana yeye ndiye muasisi wa upelelezi. Mungu akikusemesha juu ya jambo moja, nenda kalipeleleze kwanza.

Upelelezi pia unaonekana katika kitabu cha Yoshua 2:1-3, ya kuwa, Yoshua alituma wapelelezi wawili, kwa siri, kuipeleleza Yeriko. Wenyeji wa nchi wakatoa taarifa kwa mfalme juu ya wapelelezi walioingia. Mfalme akatuma askari wake kuwakamata, lakini Rahabu aliyekuwa akawaficha wapelelezi wa Bwana wakawa salama, na yeye akawa salama. Nchi ikipelelezwa ikapelelezeka, imekwisha; mambo ya mtu yakipelelezwa yakapelelezeka, amekwisha. Adui hashambulii bila kupeleleza kwanza.

Mambo ya upelelezi hayakuanza na sisi; yapo kwenye biblia. Adui hutumia taarifa ya upelelezi kumshambulia mtu; adui haji mpaka awe na taarifa. Mfano, pale Bustani ya Edeni, nyoka alipeleleza kwanza ili kuwaangusha Adamu na Eva. Hatima ya Adamu na Eva ilikuwa ni Bustani ya Edeni. Kabla hatima ya mtu haijaharibika, ilipelelezwa kwanza. Yakupasa uanze kushughulika na mpelelezi anayepeleleza maisha yako kabla hajapata taarifa zako.

Nyoka alikuwa mwerevu kuliko Wanyama wote (Mwanzo 3:1-3). Maneno ya nyoka, “Ati!”  ni njama ya kutafuta taarifa. Mpelelezi ana akili ya upelelezi; haji akikwambia nimekuja kukupeleleza. Kuwa mwerevu; usimfafanulie jambo mpelelezi. Eva alimfafanulia nyoka nahiyo ikawa ni kosa kubwa lililomfanya nyoka ajue ulipo mtego. Mtego wa shetani ni kumtamanisha mtu kufanya alichokatazwa kukifanya. Ni rahisi sana kufanya ulichokatazwa kwa sababu utataka kujua kwanini umekatazwa. Kosa walilolifanya Adamu na Eva likawaondoa kwenye hatima yao.

Adui hutumia taarifa unazotoa kukudhuru; ukifanikiwa kuficha taarifa zako, umeshinda.mfano, ukiambiwa, “mbona siku hizi unang’aa sana”, waambie tu “damu ya mwana kondoo inatung’arisha", au ukiambiwa “mbona una furaha sana siku hizi” wewe sema tu “Furaha ya Bwana ndiyo nguvu zangu”. Yafiche mambo yako dhidi ya wapelelezi.

Baada ya mpelelezi (nyoka) kuwapeleleza nao (Adamu na Eva) wakapelelezeka, shida zikaanzia hapo; mavazi awali hayakuwa tatizo, yakawa tatizo; Wanyama hawakuwa na tatizo na wanadamu, ghafla wakawa maadui n.k.

Wapelelezi huja kwa sura ya kuvutia; Neno la Bwana litawafichua wote kwa jina la Yesu Kristo! kwa moto wa roho mtakatifu tunawapima na kuwaweka wazi wapelelezi wa mambo yetu wajulikane maana kwa neno la bwana wanachambuka na hakuna wa kutoroka. Imeandikwa katika Waebrania 4:12 kuwa, “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”

Kwa jina la Yesu, mpelelezi yeyote aliyekuja kupeleleza mambo ya miradi yangu, kwa jina la Yesu siku ya leo hautanitoroka, kwa jina la Yesu!

Wapelelezi wa nchi hupeleleza ili nchi ikae sawa. Je, anayepeleleza mambo ya mtu, imani ya mtu, ndoa, nini lengo lake?

Imeandikwa katika Wagalatia 2:4-5 kuwa, “Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani; ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.”.  Kwa neno hili, ni dhahiri ya kuwa wapelelezi wa mambo binafsi ya mtu wanalenga kumtia mtu utumwani. Utumwa ni jambo lolote baya kwenye maisha ya mtu; magonjwa, umasikini, hofu n.k.

Kila mtu ana hatima yake katika Kristo, na wote tuna furaha katika Kristo. Adui hapendi tuwe na furaha katika Kristo; anakuja ili aturudishe kwenye utumwa, kwenye vifungo, kwenye matatizo, kwenye msongo wa mawazo. Tunampinga adui kwa maana Imeandikwa katika Warumi 8:15 kuwa, “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.”.

Bwana ametuagiza tufurahi katika Bwana kama ilivyoandikwa katika Wafilipi 4:4 kuwa, “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.”.  Sisi siyo watumwa katika jina la Yesu; tunaikataa hofu.

Adui akikukosa kwenye kukupeleleza utaiona hasira yake. Kwa jina la Yesu, ninakosekana kwenye mawindo wa adui zangu!

Hatima ya Yesu Ilichorwa na kusudi lake liliandikwa kabla ya kuzaliwa kwake. Wakati wa kuzaliwa, wachawi kutoka Mashariki ya mbali walifika kwa Herode kutaka kumuona mtoto Yesu wamsujudie. Herode anafadhaika na kuwapeleleza mamajusi na kupata taarifa kuwa mtoto kazaliwa yapata miaka miwili. Herode anawatuma mamajusi kupeleleza sana habari za mtoto Yesu, na wakimuona wampee taarifa ili naye aende kumsujudia (huu ni mtego). Mamajusi hawakumpa taarifa Herode; Herode hakumpata mtoto Yesu.

Adui hutuma wapelelezi kwenye maisha ya mtu ili aharibu. Adui hushambulia kulingana na taarifa alizopata. Silaha kubwa ni kulinda taarifa. Kuna wakati mtu anashambuliwa na kuharibiwa mambo yake kwa sababu ya kuongea sana / kutoa siri zake hovyo kwa watu wasiofaa. Hata kwenye kutoa ushuhuda mtu anahitaji maarifa, kwa maana ushuhuda hukaribisha vita. Zuia kamdomo; adui anakushambulia kwa sababu ya mdomo wako. Zuia ulimi wako (1 Petro 3:10).

Herode alivyokosa taarifa za mtoto Yesu akapitisha upanga kwa Watoto ili kumuua mtoto Yesu, ila hakufanikiwa (Yeremia 31:15, Mathayo 2:18).

Warumi 13:2

Kisa hiki kinamzungumzia Manoa mwenye mke tasa, asiyezaa. Neno “lakini” lilivyotumika linamaanisha, mbingu zinajua ni tasa, mbingu zinajua ni masikini, mbingu zinajua umelogwa, mbingu zinajua huwezi, lakini inabatilisha yote na kumaanisha, ni tasa lakini atachukua mimba. Lakini ni ya mbinguni. Bila kujali sababu za kibaiolojia alizonazo mke wa Manoa, lakini ya mbinguni kutoka kwa mjumbe wa Bwana inaleta tofauti kwa kufuta sababu zote.

Kisa hiki ndicho kilimleta duniani Samsoni. Kuzaliwa Samsoni kutoka kwa mama tasa ni mpango wa Mungu kuwashinda Wafilisti. Visa vya Samsoni kuwashambulia Wafilisti ilikuwa ni wanawake. Katika kuwapiga Wafilisti chanzo kwa Samsoni ilikuwa kila mwanamke aliyempata (Waamuzi 14, 15, 16).

Badae wakuu wa Wafilisti wakaona Samsoni amewashinda sana hivyo wakatafuta udhaifu wake ili kumkabili kupitia huo. Wafilisti wakataka kujua asili ya nguvu za Samsoni na ili kujua hilo, wakagundua Samsoni ana udhaifu wa wanawake hivyo wanaweza kujua kupitia mwanamke. Wafilisti wakamtuma Delila kumpeleleza Samsoni. Adui hulenga desturi ya mtu kile akipendacho ili akitumie kumfunga. Adui anakupeleleza ili akufunge uwe mtumwa akutese.

Kiasili wanadamu hatuko sawa; watu wote hatuko sawa. Samsoni mwenye vishungi vya nywele na mnadhiri wa Bwana hakuwa sawa na wanadamu wenzake. Tunavaa kama wao, tunakula kama wao ila hatuko kama wao.

Mpelelezi wa maisha yako kuna wakati anahusika moja kwa moja kwenye kifungo chako na mateso yako. Delila alimpeleleza Samsoni ili amfunge ateswe, nyuma ya Delila kuna jeshi la Wafilisti wanaomuotea Samsoni. Usimuone mtu ukamdharau vile anavyoonekana; hujui nyuma yake kuna nini kilichopo dhidi yako. Mfano, nyuma ya Yesu kuna majeshi kumi na mbili ya Malaika ambayo angeweza kutoa amri yawashambulie watesi wake.

Delila alimpeleleza Samsoni, siyo siku moja tu; ilikuwa mara kwa mara, na Samsoni alijitahidi kumficha ukweli. Ukiona mtu anauliza jambo lile lile mara kwa mara na hakati tamaa, kaa mbali naye, na uwe makini na machozi ya anayelia mbele yako.

Samsoni alipelelezwa akapelelezeka, akapofushwa na akawa mtumwa wa Wafilisti. Samsoni akawa mtu wa kawaida. Adui humtesa mtu wa kawaida. Hata hivyo badae nywele zilimuota Samsoni na kuwa siyo mtu wa kawaida tena. Tafsiri ya nywele kuota ni kurudi kwenye njia ya Mungu / kwenye mapenzi ya Mungu.

Nywele zikiota ni wakati wa kulipiza kisasi. Bwana anatutumia sisi kulipa kisasi kwa maana yeye hutenda kazi ndani yetu. Imeandikwa katika Warumi 8:28 kuwa, “…” Kwenye “mambo yote” kisasi kinapatikana, hivyo dhana ya kuwa kisasi ni juu ya Mungu mwenyewe inakosa msingi. Kwenye “mambo yote” utamuona Mungu kwa sura ya mtu. Mungu hufanya kazi na wale wampendao; ukimpenda Mungu anafanya kazi na wewe. Kisasi cha Bwana kipo juu ya wote waletao utumwa kwenye maisha ya watu.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments