UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 23.08.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: MAADUI WA
HATIMA

Hatima ya mtu ndiyo maisha ya mtu. Maadui wa hatima
ndiyo maadui wa maisha ya mtu. Hakuna mtu asiye na adui; maadui ni wengi sana. Silaha
kubwa ya adui ni kufanya uadui wake kwa kutoonekana. Mfano, nchi hununua rada
ili kuwaona maadui wanapowashambulia. Ukifanikiwa kumfahamu adui una uwezekano mkubwa
wa kushinda vita hiyo, kwa maana imeandikwa katika 2 Wakorintho 2:11
kuwa, “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua
fikira zake”. Adui hataki kujulikana.

Maisha ya mtu yanajulikana kabla hujazaliwa, hivyo
adui anaweza akawahi kushambulia hatima ya mtu kupitia maeneo tofauti tofauti.
I.
Kupitia
jina la mtu: Jina la mtu limeungana na hatima ya mtu. Adui akitaka kukuwahi,
anawahi kwenye jina lako. Kwa mtizamo wa Mungu, jina la mtu linabeba hatima ya
mtu, ndiyo maana adui anaweza kukushambulia kwasababu ya jina lako ulilopewa.
Baraka za mtu zinaenda na jina la mtu, na kwa Kadiri watu wanavyoliita jina la
mtu ndivyo wanaita hatima yake “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika
nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi
nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;” Mwanzo 12:1-2.
Mungu alipotaka kumuita mtu
amtumikie, alimbadilisha jina kwanza kwa maana, jina linabeba kusudi la mtu huyo.
Katika kitabu cha Mwanzo 17:1-6, Mungu anafanya agano na Abramu
kuwa baba wa mataifa mengi. Wakati Mungu akifanya agano hilo, Abramu na mkewe
Sarai walikuwa wazee wa umri wa zaidi ya miaka tisini, na hawakuwa na mtoto,
isipokuwa Abramu alikuwa na mtoto aitwaye Ishmaeli.
Mungu akambadilisha jina Abramu
na kumuita Ibrahimu ili aendane na hatima; jina Ibrahimu lina uwezo wa kuwa
baba wa mataifa mengi lakini Abramu halikuwa na uwezo huo. Jina linabadilishwa
ili kubeba hatima ya ki Mungu. Jina likibadilika, hatima ya mtu inabadilika,
afya ya mtu inabadilika na hali ya mtu inabadilika.
Mungu aliposema na Abramu na
kumbadilisha jina kuwa Ibrahimu, akamgeukia mke wa Abramu, Sarai na
kumbadilisha jina kuwa Sara ili awe mke wa Ibrahimu baba wa mataifa mengi, naye
sara awe mama wa mataifa mengi.
Ndoa ya mtu ina uhusiano sana na
hatima yake; mume anaweza akaathiri hatima ya mke, vivyo hivyo mke anaweza
akaathiri hatima ya mume. Mmoja akiwa imara anaweza akafanikisha hatima ya
mwenzake, na mmoja akiwa dhaifu anaweza akaiangusha hatima ya mwenzake.
Mungu akikupa jina, baraka za
jina zinakuja na desturi zake ili ziendane na hatima. Sarai katika umri wa
miaka tisini hakuwa na mtoto na alikoma desturi za mwanamke, lakini Sara
anapewa baraka za kuwa mama wa mataifa mengi naye anapata mtoto (Isaka) ambaye
Mungu anaahidi kuimarisha agano lake kupitia Isaka kuwa la milele.
Baraka za
Mungu kwa Ibrahimu na Sara ni kuwa baba na mama wa mataifa mengi, lakini wao
walipata mtoto mmoja aitwaye Isaka. Mbele za Mungu mtu ni nchi, ni taifa; hata
Rebeka alivyopata mimba ya mapacha ambao walikuwa wakishindana tumboni, Mungu
alimwambia kuwa ni mataifa mawili tumboni mwake yanafarakana “Watoto
wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini?
Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako,
Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa
hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.” Mwanzo 25:22-23.
Katika kutimiza hatima, yapo matumbo huzaa Wafalme mbele za Mungu.
Ibrahimu alipokea baraka zake kwa
umakini sana lakini wakati anaambiwa baraka za mkewe, akacheka. Hili
linatufundisha kuwa, pokea baraka zako wewe mwenyewe na usisubiri kupokelewa na
mwenza wako. Mungu hakuangalia yanayotoka mdomoni mwa Ibrahimu, ila yale
yatokayo moyoni mwake Ibrahimu. Chochote uwazacho na kusema moyoni, kiwe sawa na
vile Bwana anavyosema, na midomo iseme hayo. Alichowaza Ibrahimu na kusema
kilikuwa tofauti na Mawazo ya Mungu (Mwanzo 17:17-19).
Imeandikwa katika Mithali
10:22 kuwa, “Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni
nayo.”. Mungu akisema anatimiza; yeye aliyeishi tasa ataitwa mama wa
watoto na hakuna wasiwasi, nchi ya ukame itazaa matunda, kwa jina la Yesu! Kwa
yote Mungu atakayosema, wewe mwamini tu ili uthibitike, na kwakuwa Mungu
hutenda kazi zake kupitia watu wake, waamini manabii wa Mungu ili ufanikiwe “Wakaamka
asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa
wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa
Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini
manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.” 2 Mambo ya Nyakati 20:20. Mambo
ya Mungu ogopa kuyapima nae limu yakow ala sayansi. Neno la Bwana linakuja kwa
wakati sahihi, na likija linakuja na majibu yote unayoyahitaji; neno likitoka
halirudi bure.
Mungu siyo wa yeyote; hafanyi
kazi na waliopo. Mungu hufanya kazi na aliowachagua kutimiza kusudi lake.
Mfano, nabii Samweli kwenye familia ya Yese hakupaka mafuta Watoto waliokuwepo
tena waliokuwa na sifa kimuonekano kwa sababu aliyechaguliwa na Mungu, Daudi,
hakuwepo lakini alikuwa na neema ya kusubiriwa. Mungu humsubiri aliyemkusudia
hata kama amefichwa mbali asionekane. Neema ya Mungu ya kusubiriwa na iwe kwetu
kwa jina la Yesu, ili kule kwenye hatima zetu tusubiriwe.
Hatima ikiwepo, ipo tu. Daudi
alivyoletwa kutoka nyuma ya jangwa, na nabii Samweli alivyomuona tu,
akammiminia mafuta. Mungu siyo wa mbadala. Ibrahimu alimwambia Mungu kuhusu
uwepo wa Ishmaeli lakini Mungu hakutaka aliyepo (Mwanzo 17:21).
Hii inatufundisha kuwa tuombe kwa ajili ya kusudi la Mungu, vinginevyo tunaomba
vibaya “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu.” Yakobo 4:3.
Mungu aliweka kusudi kwa isaka
ambaye hakuwepo wakati huo. Wakati Mungu anaweka agano na Ibrahimu, ni kama
ilikuwa haiwezekani hivi lakini mwaka uliofuata majira yaleyale Sara na uzee
wake, akamzaa Isaka. Mungu akufanyie muujiza wako ili mwakani majira kama haya
uwe na ushuhuda mbele zake, kwa jina la Yesu!
Kuzaliwa kwa Yesu: Jina la Yesu
lilitangulia kabla ya kuzaliwa kwake (Mathayo 1:18-21). Jina lake
limeambatana na kusudi lake, yaani, mwokozi wa watu wake na dhambi zao.
Alipoanza kuishi hatima yake, wapo waliojaribu kupotosha kusudi lake na kumuita
mwenye pepo. Kwa kusudi lake Yesu, kila neno alilosema lilihusiana na kuokoa
watu na dhambi zao, lakini walimuona mwenye pepo (Yohana 8:45-59).
Yesu hakubadili kusudi lake; alishikilia msimamo wake ambao, maneno yote
aliyosema yalihusu wokovu, yaani, kila amwaminiye hatakufa milele “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16. Kwa
kusudi la Yesu, inawapasa watu wake wamwamini tui li wawe na uzima wa milele (Yohana
17:3).
Kama ambavyo Yesu hakubadili
hatima yake hata baada ya kukataliwa (Yohana 1:11-12), sisi pia
hatubadili hatima; tukibezwa, watu wakiwa kinyume na sisi, hatubadili hatima,
tunang’ang’ania hivyo hivyo kwa maana, “sisi siyo kama wale”. Tukikataliwa
haibadilishi chochote; sisi ni wana wa Mungu tu. Popote tuendapo tunaeneza mila
za mbinguni. Popote tulipo, sisi ni mfano wa Mungu hapa duniani; ukituona
umemuona Mungu duniani, ukitusikia umemsikia Mungu duniani. Imeandikwa katika 1
Yohana 3:1 kuwa, “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa
Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu
haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”.
Jina linabeba hatima. Jina la
Yesu ni jina lililoambatana na ukombozi wa ulimwengu kutoka kwenye dhambi. Hatufi
kwa sababu hamna magonjwa, ila ni kwasababu ya kuamini jina la Yesu. Hatima
iliyobebwa na jina inaonekana katika kitabu cha Mwanzo 32:25-30
ambapo Yakobo anabadilishwa jina na kuitwa Israeli kumaanisha amemshinda Mungu
na watu. Yakobo alishinda kwa sababu ya kanuni ya rohoni; ili roho ifanye kazi
kwa ufanisi, lazima ivae mwili.
Kuzaliwa kwa Yohana: Lilitangulia
jina la Yohana (Luka 1:8-13). Jina huambatana na hatima; hatima
ya Yohana imeelezwa katika kitabu cha Luka 1:15-17. Jina
likichengeshwa hatima inachengeshwa; watu walitaka kuchengesha hatima ya
Yohana, hivyo wakataka kumpa jina tofauti, lakini Zakaria na Elizabethi
walilijua kusudi la Mungu wakamuita mtoto wao Yohana (Luka 1:57-64).
Ukichengesha jina la mtu umeharibu hatima ya mtu; usiwe mwepesi wa kukubali
kupewa majina ambayo yanaweza kupindisha hatima yako.
Wapo watu hutoa majina kulingana
na mazingira ya wakati wa kuzaa; mfano, shida, sikitu, chausiku, butiku,
Mawazo, matatizo, ndivyo maana za majina hufuata maisha yao. Batilisha nguvu
zote za adui nyuma ya jina ulilopewa, kwa jina la Yesu.
II.
Watu
kukusema kinyume na hatima yako: Unapoanza kuishi kusudi lako, jamii inajiinua
kinyume na mwenendo wako ili ukate tamaa. Mfano umeitwa na Mungu kwa ajili ya kuhubiri
neno lake, lakini kwa sababu ya watu kukuzungumzia vibaya kinyume na mwenendo
na jitihada zako, maneno yale yanakudhoofisha na kukufanya uache kile
ulichoitiwa na Mungu kumbe unaenda kinyume na hatima yako.
Kwenye biblia Mungu alimtuma Nehemia
kuujenga ukuta wa Yerusalemu lakini wakaibuka watu wawili waliotaka kukwamisha,
Sanbalati na Tobia (Neemia 4:1-3). Usiogope kughadhibiwa, watu
kuingiwa uchungu, kudhihakiwa na kusemwa kinyume na unachokifanya ili uache
kusudi lako la ki Mungu unalolifanya; piga moyo konde, maneno kama, “eti naye”
yasikurudishe nyuma. Ukisikia hayo wewe amini tu kuwa unayaweza mambo yote
katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13), na kwamba ufalme wa
mbinguni unapatikana kwa nguvu, na ni wenye nguvu pekee wenye uwezo wa kuuteka,
hivyo usisuse (Mathayo 11:12).
Kusemwa, hiyo no roho na ipo
sehemu yoyote kwenye jambo lolote. Kwa kadiri unavyoendelea bila kukata tamaa,
ndivyo unavyomtumikia Bwana; usiionee haya injili (Warumi 1:16).
Usisubiri kupongezwa kwenye yale ufanyayo kwa maana utakumbana na roho ya
Sanbalati na Tobia. Ukiacha kile Mungu anataka ufanye, utawajibika, na
usipokuwa tayari kufanya upaswayo kuyafanya, utapigwa (Luka 12:47-48);
asiwepo wa kumkatisha tamaa mwenzake.
Kokote ulikowekwa kufanya kazi ya
Mungu, Fanya kwa uaminifu sana kwa sababu yeye aonaye sirini anakuona. Hekima ni
kufanya kwa bidii sana bila kujali watu wanakuangaliaje.
III.
Maadui
wa hatima wakishindwa kukukatisha tamaa, watajitokeza waziwazi kushindana na
wewe: Inawezakutokea kwa namna ya kukuletea ushauri, na usipofanya kama
wanavyokushauri watashindana nawe “Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na
Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza
kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa,
basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na
Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.” Nehemia 4:7-8.
Ukibaki katika kusudi la Mungu,
hata wakishindana hawatakushinda. Hatuachi kumtumikia Mungu na Kutenda kusudi
lake jema kwa maana maisha ya wokovu ni maisha ya kupigana vita; TUNAJENGA HUKU
TUNAPIGANA VITA. Sisi ni kanisa la kupigana vita
IV.
Wakijitokeza
ukawashinda, watatuma mashetani: Mara nyingi watu hujiuliza kwanini wanalogwa.
Kulogwa ni hatua ya mwisho kabisa. Wakituma mashetani wanadhamiria wakuongoze
vibaya kwenye maamuzi yako ili uanguke.
Shetani akitumwa anakujia
kukushawishi ufanye vile anavyotaka (1 mambo ya nyakati 21:1). Shetani
anaweza akasimama juu ya familia yako, biashara yako, miradi yako au kusudi
lako lolote akakushawishi ufanye kinyume.
Ni kanuni ya Mungu kuwa siku zote
hutenda kazi kwa utashi wa mtu (Wafilipi 2:13). Shetani huingilia
utashi huo ili mtu asifanye yale yampasayo kufanya. Vile utakavyoamua ndivyo
utakavyomaliza hatima yako; vuzuri au vibaya, itategemea na utakavyoamua.
Ukifanikiwa, utakuwa umeamua sawasawa, na kushindwa, utakuwa umeshawishiwa na
shetani ukashawishika.
Kutumia akili ya shetani ni
chukizo mbele za Mungu. Mawazo ya shetani yanasababisha kubadili tabia ya mtu.
Angalia sana unachowaza kwa maana kile unachowaza, siku moja utakisema; na
unachokisema, siku moja utakifanya. Mungu hakumuadhibu shetani kwa alichotenda
ila kwa alichowaza.
Wakati mwingine mashetani
wanatumwa kwako ili kuharibu tabia; tabia ikiharibika, hatima inaharibika. Unachokifanya
mara kwa mara hugeuka kuwa tabia yako. Pepo humwingia mtu na kuleta tabia
yoyote, mfano, uongo ni pepo (2 Mambo ya Nyakati 18:21), udhaifu
ni pepo (Luka 13:11).
Habari njema ni kwamba, Yesu anao uwezo wa
kuwafungua watu waliofungwa kwa tabia za kipepo kama alivyomfungua mwanamke
aliyepindana kwa miaka kumi; msadiki tu Yesu, naye atakufungua (Isaya
53:1-5).
Unamshinda adui kwa kumkabidhi Yesu maisha yako.
Maisha yetu yamegawanyika katika kambi mbili tofauti; 1) Kambi ya Yesu, 2)
Kambi ya Shetani. Huwezi ukapigana vita ukiwa ndani ya kambi ya shetani, hivyo ni
lazima utoke kwenye kambi ya shetani kwa kumpa Yesu maisha yako halafu
tunaungana kuishambulia kambi ya shetani. Ukimpa Yesu maisha yako unakuwa
umeokoka, na unakuwa na uwezo wa kutandika maadui wanaosimama kinyume na hatima
yako.
Ukiokoka, maadui zako wanakuwa maadui wa Bwana.

0 Comments