UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 16.08.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: MANENO
YALIYOTAMKWA KINYUME NA HATIMA YAKO
![]() |
Mungu katika uumbaji wake aliumba kwa neno, na kila
neno alilotamka lilikuwa vilevile na halisia. Imeandikwa katika Waebrania
11:3 kuwa, “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa
neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.”.
Kila kitu kinachoonekana ni zao la neno alilotamka
Mungu, Nyota, milima vyote ni matokeo ya neno la Mungu. Katika kitabu cha Mwanzo
1:1-3 tunaona Mungu “akasema” ikawa. Mungu kabla hajafanya jambo
lolote, anasema kwanza. Hata kanisani, makuhani wa Mungu hutanguliza kusema
neno kwanza na baada ya hapo maombezi hufuata. Haiwezekani watu waje kanisani
alafu moja kwa moja waanze kuomba bila kusikia neno kwanza, kwa sababu kanuni
ya Mungu ni neno la Mungu kwanza ili watu wafunuliwe kwanza. Neno la Mungu ni
msingi wa kila kitu.
Mambo hutokea sawasawa na neno lililotamkwa. Roho
Mtakatifu huangalia kila neno la Mungu lililosemwa ili alithibitishe. Hitaji la
mtu kwa ajili ya biashara hutanguliwa na neno la Mungu juu ya biashara;
linaanza neno la Mungu badae ufumbuzi wa hitaji la mtu linapatikana. Mungu
akisema, kitu cha ki Mungu kinatokea; wachawi wakitamka neno, matokeo ya
kichawi yanatokea pia. Mwanzo wa kila kitu ni neno, na vyote vinafanyika kwa neno
(Yohana 1:1).
Kanuni ya Mungu iko vilevile hata sasa; pasipo neno
la Mungu hakuna uponyaji; linatangulia neno la kuponya kabla ya uponyaji. Ndani
ya neno kuna uzima tele ambao ni nuru ing’aayo gizani. Giza haliishindi nuru ya
neno la Bwana. Likitokea neno, giza linapotea. Usikimbize giza bali peleka neno
la Bwana nalo Giza litakimbia lenyewe; mfano, giza kwenye ndoa, giza kwenye
biashara, giza kwenye ajira, giza kwenye hatima. Roho Mtakatifu husimamia neno
lililotoka, alitimize.
Baada ya mwanzo kuwako neno, badae neno liligeuka
likawa mtu. Imeandikwa katika Yohana 1:14 kuwa, “Naye Neno
alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa
Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”.
Neno lolote likivaa mwili likawa mtu, watu wanaona
matokeo / matunda. Hakuna neno linalotoka hewani bali kila neno linatoka kwa
mtu. Mfano, ukitamka maneno ya kutishia kuua, hayakamatwi maneno ila anakamatwa
mtu; maneno hayatenganishwi na mtu. Ukisema maneno yanayozuia hatima, maana
yake ni mtu anazuia hatima yake mwenyewe au ya mtu mwingine, ndiyo maana
ukisikia “neno la Bwana likamjia nabii Yeremia, kusema…” maana yake ni Mungu
mwenyewe anashuka kutusaidia kwenye tabu zetu (Yeremia 37:6). Likitamkwa
neno la uponyaji maana yake ni mtu Yesu anakuja kuponya hitaji la mtu.
Kama neno lilimjia Yeremia, Amosi na wengine,
linaweza kutujia hata sisi, na linapotujia, ni Yesu anatutembelea kwenye
biashara zetu, kwenye uponyaji; anatutembelea na kutupa yale tunayoyahitaji.
Neno ni mtu “naye neno akavaa mwili, akakaa kwetu,
na sisi tukauona utukufu wake”. Neno akikaa mahali, utukufu wake unaonekana,
na watu wote wanauona. Kwa jina la Yesu, neno akae kwenye biashara zetu,
kanisani, kwenye maisha yetu, na watu wote wauone utukufu wake maana neno la
Bwana linasema hivyo (Ufunuo 19:13).
Siku zote unaposikia neno maana yake unayemsikia ni mtu.
Ukisoma kwenye kitabu cha Yohana 6:63, imeandikwa
kuwa “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo
niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” Tunapata tafsiri kuwa neno ni roho,
na tunafahamu kuwa mtu ni roho. Kama mtu ni roho, na neno ni roho, hivyo,
tafsiri ya wanamahesabu iko wazi kuwa neno ni mtu; mtu siyo mwili.
Kwakuwa mtu ni roho, imeandikwa katika Ezekieli
2:2 kuwa, “Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha;
nikamsikia yeye aliyesema nami.”. Kila mtu anaposema na wewe kuna roho
inakuingia. Ukitakia kuchagua roho ipi ikuingie, chagua wa kuongea naye; siyo
kila mtu ni wa kumpa sikio lako. Kuna watu ukiongea nao, maneno yao
yanakusimamisha, na kuna watu ukiongea nao, maneno yao yakakufanya uanguke.
Ukitaka kushinda baadhi ya vita, chagua watu wa
kuwasikiliza. Ukichagua wa kumsikiliza, umechagua roho ya kukuingia. Kuna roho
inakuingia na kukutia hofu, kukukatisha tamaa, inazuia hatima, inakurudisha
nyuma na kwa ujumla inakuangusha. Sikiliza watu ambao roho ikikuingia unaiendea
biashara, ndoa, unapata ujasiri na siyo hofu. Chagua wa kukupa ushauri, maana
kuna mtu kwa kadiri anavyokushauri ndivyo anakutia hofu. Usikubali kushauriwa
na mtu aliyeshindwa; kama alishindwa yeye, haimaanishi wewe pia utashindwa.
Kama alishindwa, basi ana roho ya kushindwa; ukimsikiliza, roho ya kushindwa
itakuingia.
Sisi tunaamini kushinda kwenye kila kitu, kwa maana
imeandikwa katika Warumi 8:37 kuwa, “Lakini katika mambo
hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”.
Tunafanya yale ambayo baba yetu amekuwa akitusihi na
kutufundisha ili kufikia hatima zetu. Tatizo watu ni wagumu kuamini katika neno
na kuiendea hatima. Kuna watu labda tutumie kanuni za fizikia (Isack Newton’s
law of motion) kwenye maisha yao kupata nguvu ya kuwasukuma ili waendee hatima
zao. Ukisukumwa, sukumika; kwa jina la Yesu, neno la Bwana likusukume uende
kwenye njia ambayo Bwana ameshakuandalia. Kwa njia ya neno ulizuiwa, basi leo
kwa njia ya neno uachiliwe uende.
Imeandikwa katika Marko 16:17-18 kuwa,
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo;
watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha,
hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Neno la Mungu hutangulia halafu matokeo / matunda
hutokea. Katika kitabu cha Marko, Yesu ametanguliza neno lake. Kila neno
lililosemwa linabeba ishara zinazofuatana nalo; neno la biashara linafuatana na
ishara za biashara, neno la ajira linafuatana na ishara za ajira, neno la
uponyaji linafuatana na ishara za uponyaji.
Kuna roho nyuma ya maneno, kuna mtu nyuma ya maneno
kwa sababu neno ni roho na mtu ni roho. Kuna mtu anaharibikiwa sababu ya maneno
yake mwenyewe. Imeandikwa katika kitabu cha Yakobo 3:2 kuwa, “Maana
twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo
ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”.
Vitu vyote vinavyomsumbua mtu ni sababu ya mdomo wake. Imeandikwa pia katika
kitabu cha 1 Petro 1:10 kuwa, “Katika habari ya wokovu huo
manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za
neema itakayowafikia ninyi.”. Ukitaka kutoboa maisha, siku zako ziwe
njema, ufurahie maisha yako ya ndoa, kazini, zuia ulimi wako usiseme mabaya kinyume
na neno la Bwana; kamdomo katakuponza.
Imeandikwa katika kitabu cha Mithali 18:21
kuwa, “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao
watakula matunda yake”. Ukitaka matunda ya uzima, sema kuhusu uzima;
ukitaka matunda ya ajali, sema kuhusu ajali; ukitaka matunda ya mauti, sema
kuhusu mauti.
Imeandikwa katika kitabu cha Zaburi 118:18
kuwa, “BWANA ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife”. Sababu ya
kutokufa ipo; biashara yangu haitakufa, ndoa yangu haitakufa, hatima yangu
haitakufa … ILI NIYASIMULIE MATENDO YA BWANA, kwa maana Mtetezi wetu yu hai (Ayubu
19:25).
Neno linaweza likageuza maisha ya mtu. Watu wabaya
wakijua unaelekea kupenya kwenye hatima yako, wanatuma neno lakutaka kwenda
kinyume na hatima yako. Mfano; mfalme Dario alitaka kumpa nafasi ya juu katika
ufalme wake mtumishi wa Mungu Danieli, taarifa zikasambaa kwenda kwa watu na
hao watu wakaenda kutoa ushauri kwa mfalme lengo lao kubwa ni kutaka kuzua
kupenya kwa Danieli. Walishawishi mpaka kuweka sheria kali, na wakati wa
kupitisha sheria Danieli hakuwepo.
Neno moja hubadili kabisa moyo wa mtu kumwamini mtu;
mfano, maneno kama “angalia sana mkeo / mumeo” yanaweza kuvuruga ndoa iliyo na
amani. Kuna neno limesababisha mtu aachishwe kazi isivyo sawa.
Neno la laana kwa Reubeni lilibadilisha Reubeni kuwa
mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na nguvu ya neno iliathiri mpaka vinasaba vya
Reubeni kwa Yakobo (1 Mambo ya Nyakati 5:1).
Maneno aliyotamkiwa mtu ni lazima ipatikane nguvu /
mamlaka ya rohoni ya kuyatangua. Maneno na laana kwa Reubeni yalikuja kutanguliwa
na Musa; uzao wa Reubeni ukaonekana tena kwa wana wa Israeli (Kumbukumbu
la Torati 33:1-6, Ufunuo 7:1-5). Kadhalika, neno la laana
juu ya mtu atakayeijenga Yeriko lililotolewa na Yoshua, badae lilitanguliwa na
Elisha.
Kuna uchawi wa kuzuia watu kwa maneno; imeandikwa
katika kitabu cha Ufunuo 2:14 kuwa, “Lakini ninayo maneno
machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye
aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu
vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”.
Maneno, “mafundisho ya Balaamu” ni mafundisho ya
kuzuia watu wasipenye / wasiende kwenye hatima. Ni mafundisho ya kutia ukwazo.
Yapo mafundisho ya kuondoa ukwazo / kuondoa vizuizi. Sisi tumefundishwa na baba
yetu mafundisho haya; jinsi ya kuhubiri, kuwafungua watu na kuondoa vizuizi.
Tunayazuia mafundisho ya Balaamu yasifanye kazi kwenye maisha ya watu. Kama
analaani bila aibu, tunakanusha / tunatangua bila aibu; wanalaani kwa mdomo,
tunatangua kwa mdomo.
BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI


0 Comments