google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MUNGU WA MABADILIKO (THE GOD OF TURNAROUND)

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 20.09.2026
PASTOR DON HEE
SOMO: MUNGU WA MABADILIKO (THE GOD OF TURNAROUND)

Baraka na ulinzi wa kweli wa mwanadamu vimeunganishwa moja kwa moja na kusudi au wito (sehemu) ambayo Mungu amemuitia kuwepo. Kukimbia changamoto na kutafuta faraja ya muda nje ya wito huo huleta maisha ya hofu na kuchelewesha mabadiliko makubwa ya Mungu kwenye maisha ya mwanadamu.

Neno kuu: Mwanzo 26 (safari ya Isaka).

Watu wengi leo wanaondoka kwenye maeneo na wito ambao Mungu amewaweka kwa sababu ya kukimbia shida au changamoto. Isaka alikumbana na njaa kali katika nchi ya ahadi ya Kanaani, ikamlazimu kuhama kwenda Misri kwa maamuzi yake mwenyewe.

Isaka alipofika Gerari akielekea Misri kutoka Kanaani, Mungu hakumwadhibu bali alimwonyesha neema. Mungu akampa Isaka amri tatu azifuate;

1.   Isaka asiende Misri (ishara ya dunia);

2.   Isaka akae Gerari kwa muda;

3.   Isaka aishi katika nchi atakayoambiwa na Mungu (Kanaani).

Mungu anaahidi kuwa kama Isaka atamtii, basi Isaka atapata mambo matano ambayo ni;

1.   Mungu atakuwa naye;

2.   Mungu atambariki;

3.   Mungu atampa ardhi yeye na uzao wake;

4.   Mungu ataongeza uzao wa Isaka kama nyota; na

5.   Mungu atabariki mataifa yote kupitia Isaka.

Kwa shida ya njaa na kutafuta chakula, Isaka akakaa Gerari. Isaka akaishi Gerari kwa hofu na kudanganya kuwa mke wake, Rebeka, ni dada yake (akafanya makosa yale yale ya baba yake, Ibrahimu, aliyedanganya kuwa mkewe, Sara, ni dada yake). Gerari ilikuwa ni katikati ya Kanaani na Misri. Katika maisha yetu, Kanaani inawakilisha mahali pa wito wa Mungu kwa mwanadamu, Misri inawakilisha alama ya anasa za dunia, na Gerari inawakilisha hali ya kutokuwa na msimamo wa kiroho wala kimaadili.

Kama Isaka alivyokwamia Gerari, ni sawa na Wakristo wengi wanaoishi "Gerari" wakiwa na mguu mmoja kanisani na mguu mwingine kwenye tabia za kidunia; haya ni maisha ya kinafiki au uoga wa kushindwa kujitoa kwa asilimia mia moja kwenye utii wa Mungu kwa hofu ya kupoteza marafiki au fursa za kidunia.

Mfalme Abimeleki anagundua uongo wa Isaka aliousema ili akae Gerari, lakini badala ya kumwadhibu Isaka, Mfalme anatoa amri ya kumlinda. Kulindwa kwa Isaka na Mfalme Abimeleki ni kutimiza tu agano ambalo Mungu alikuwa ameliweka kumlinda Isaka, wala haikuwa kwa sababu ya utashi binafsi wa Mfalme; njia ya mtu kujilinda haiwezi kumlinda, isipokuwa, ulinzi wa kweli hutoka kwa Mungu.

Isaka anapata ujasiri, anapanda mbegu na kuvuna mara dufu katika ardhi ile ile ya Gerari, na anakuwa tajiri na mwenye nguvu sana, jambo linalomfanya Mfalme Abimeleki na Wafilisti wamwonee wivu na kumfukuza; ni neema ya Mungu iliyompa nguvu tena. Isaka akaenda bonde la Gerari, na akachimba kisima lakini watu wa Gerari wanagombana naye; mahali hapo akapaita Eseki, yaani Magomvi.

Isaka anahama tena na kuchimba kisima kingine kinachogombaniwa pia, anapaita Sitna, yaani Adui. Hizi zilikuwa fursa ambazo Mungu aliruhusu magumu yatokee ili Isaka asikae hapo bali arudi Kanaani, lakini Isaka hakuelewa. Isaka anahama na kuchimba kisima kingine mahali ambapo hapakuwa na magomvi kabisa, na anapaita Rehobothi, yaani nafasi pana. Isaka anafikiri amepata amani.

Je, ni kweli Rehobothi ni mahali pa amani? "Hapana! Rehobothi bado ni ndani ya Gerari; ni maili 20 tu kutoka mpakani. Rehobothi inawakilisha mafanikio ya kiuchumi au faraja ya kidunia inayomfanya mtu amsahau Mungu au malengo yake makubwa ya maisha; kustarehe Rehobothi kulimchelewesha Isaka kurudi kwenye wito wake halisi.

Hapo awali tumejifunza kuwa moja ya amri tatu za Mungu kwa Isaka ni Isaka akae Gerari kwa muda tu. Tunatakiwa tusifanye 'kwa muda' ikawa muda mrefu; kwa mfano, Naomi na Elimeleki walienda Moabu kukaa "kwa muda" kukwepa njaa, lakini wakakaa miaka 10 na kusababisha Naomi kumpoteza mume na watoto.

Hatimaye Isaka anaondoka Rehobothi na kupanda hadi Beer-sheba (iliyopo ndani ya Kanaani). Mungu anamtokea hapo kwa mara ya pili na kumwambia, "Usiogope, mimi niko pamoja nawe." Adui yake, Mfalme Abimeleki akiwa na mkuu wa majeshi, wanamfuata Isaka kunyenyekea mbele ya Isaka na kuomba wafanye mkataba wa amani kwa sababu wameona Mungu yuko pamoja na Isaka; zamani Isaka alimuogopa Abimeleki, lakini sasa Abimeleki anamwogopa Isaka.

Katika Agano Jipya, msalaba ni Beer-sheba ya Yesu. Pamoja na maumivu makali, Yesu alibaki msalabani hadi mauti, na matokeo yake yakawa ni mabadiliko makubwa ya kufufuka na kumshinda shetani. Mabadiliko makubwa ya maisha ya mtu yanahitaji uvumilivu na uaminifu hadi mwisho wa jambo alilokabidhiwa mtu; hapa ndipo "Mungu wa Mabadiliko" anapopigana vita vyetu na kuwalazimu maadui zetu (umasikini, magonjwa, au wapinzani wetu) wanyenyekee mbele zetu.

Sikia sauti ya Mungu kupitia matatizo: Changamoto au mashambulizi ya shetani unayoyapata ukiwa nje ya wito wako (Gerari) ni fursa au njia ya Mungu kukusukuma urudi kwenye Beer-sheba yako (wito wako halisi). Gerari ni sehemu ya kujitoa nusu nusu; kaa kwenye eneo ambalo unaweza kujitoa kwa asilimia mia moja kwa mapenzi ya Mungu.

Ukimtii Mungu kikamilifu, Mungu atazungumza na wewe moja kwa moja. Kabla Isaka hajamtii Mungu kikamilifu, alibaki Gerari, lakini alipoamua kumtii Mungu kwa ukamilifu, Mungu akamuongoza kuifikia hatima yake na huko akamjengea Mungu mahali pa kumwabudu na kumtukuza.

Unapokuwa kwenye nchi ya ahadi, haimaanishi huwezi ukapata changamoto. Changamoto zitakufuata lakini hazitakushinda kama utamwamini Mungu bila kumuacha. Popote pale Mungu alipokuitia, iwe ni kwenye maombi, kufunga au huduma fulani, baki hapo hapo kwa sababu hapo ndipo Mungu alipoweka neema na baraka zako, hata kama kuna njaa au magumu; amini tu kwa maana imeandikwa katika Zaburi 91:10, “Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.” Baraka ya mtu ina uhusiano na mahali alipoitiwa.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments