google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MATUKIO YA KICHAWI

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 11.10.2026
ARCHBISHOP DR JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: MATUKIO YA KICHAWI

Kuna baadhi ya matukio maishani (magonjwa, balaa, mikosi, au kufeli kibiashara na kimasomo) yanayoonekana kwa macho ya nyama kama ya kawaida au ya kibinadamu, lakini kimsingi ni matukio ya kishetani na yametengenezwa kiroho.

kila ukoo una mchawi wake. Mchawi huyo anakuwa na nguvu zaidi ikiwa humjui; mchawi akijua kuwa amegundulika na anafahamika, anaogopa kuleta madhara. Kwa mfano, ukimjua mchawi na ukampatia mtoto wako akulelee, atamlea bila tatizo lolote na utamkuta mtoto ni mzima; "Mchawi mpe mtoto akulelee."

Matukio yote yametengenezwa. Hakuna tukio la bahati mbaya. kila tukio jema linatoka kwa Mungu na kila tukio baya (kama ajali za barabarani au magonjwa) linapangwa na kuratibiwa na shetani. Tukio baya alilotengenezewa mtu halitaisha mpaka aliyelitengeneza ajulikane na kushughulikiwa na mtu huyo.

Mchawi anashughulikiwa; usipomshughulikia ataendelea kukusumbua siku zote. Mfano; Nzi akitua juu ya jiko la mkaa, tatizo siyo la nzi bali ni kwamba jiko halina moto. Vivyo hivyo, ili majini, wachawi, magonjwa na laana vimtoke mtu, haitakiwi kugombana navyo kimwili, bali ni lazima mtu auwashe moto wa kiroho (maombi) navyo vitakimbia vyenyewe.

Kisa cha Mfalme Ahabu, Mikaya na Mshale wenye Macho (1 Wafalme 22:19-23):

Kila jambo / tukio huanzia rohoni na kudhihirika mwilini. Kwenye ulimwengu wa roho, vikao hukaliwa na matukio huamuriwa kwenye vikao hivyo. Manabii wa uongo walimwambia Mfalme Ahabu kuwa aende vitani atashinda, lakini Mikaya, nabii wa Mungu aliona maono katika ndoto kuwa Mungu aliruhusu pepo wa uongo aingie kwenye vinywa vya manabii wa Mfalme Ahabu ili kumdanganya aende vitani Ramoth-Gileadi akaanguke. Ahabu alijaribu kukwepa unabii wa Mikaya kwa kuvaa nguo za raia wa kawaida na kumwacha Mfalme Yehoshafati avae mavazi ya kifalme vitani; Mfalme Yehoshafati akawa target. Mara nyingi adui anapokupiga vita, au mtu anapokupa ushauri mbaya, hawafanyi hivyo kwa akili zao; wanakuwa wameingiwa na pepo chini ya ushawishi wa kishetani ili kukuangamiza.

Kuna wakati mtu anakutafuta tu kwa kukushambulia ama watoto, ama kazi, au jambo lolote; mkaribishe kwenye uwanja wa vita maana ameshawishika kuja kwenye anguko lake; imepangwa adui aje afie kwenye mlango wako. Anayekushambulia amewekewa kiu na shetani ya kukushambulia, na kikao cha mbinguni kimeridhia adanganyike kuwa atashinda ili aje akushambulie afie mikononi mwako; fahamu ya kuwa adui atashindana nawe lakini hatakushinda kwa maana njia za kutoka mautini zina yeye Bwana (Zaburi 68:20).

Wakati wa vita, askari mmoja wa adui alirusha mshale kwa kubahatisha (kwa nasibu), na mshale ule ulimtafuta Ahabu na kupenya katikati ya maungio ya bampa zake za chuma mwilini, naye akafa mtoni, na mbwa wakalamba damu yake kutimiza unabii wa Eliya.

Mshale wa maombi una macho na utamtafuta mtesi wako popote alipo. Roho Mtakatifu anajua penye maungio. Wote walioungana kufanya vita dhidi yako, mshale wa maombi utawaona; wamekuja kwa njia moja, watatawanyika mbele yako kwa njia saba (Kumbukumbu la Torati 28:7) kwa maana walio upande wako ni wengi kuliko walio upande wa adui (2 Wafalme 6:16).

Ahabu alikuwa na ugomvi na Mungu; yeyote anayemsaidia Ahabu anapigwa sawasawa na anavyopigwa Ahabu. Anapigwa farasi na aliyempanda, gari na aliyechukuliwa ndani yake. Jambo la muhimu vitani, usipigane vita ya wengine. Pigana vita vyako mwenyewe; usiwe Yehoshafati.

Ulimwengu wa roho ndio unaozalisha uhalisia wa ulimwengu wa mwili. Kitabu cha Ayubu 4:14-16 kinaeleza athari za kibaolojia kama vile kusisimka kwa mwili na nywele kusimama, si matokeo ya mabadiliko ya ghafla ya kimazingira tu, bali ni mguso wa dhahiri wa kiroho wakati 'pepo' au roho chafu inapopita mbele ya uso wa mtu.

Katika Luka 13:10-16, ugonjwa wa kupinda mgongo kwa miaka 18 unaonekana kwa nje kama tatizo la kawaida la kimatibabu. Hata hivyo, ugonjwa huo ulikuwa 'tukio la kichawi' lililopangwa na kuratibiwa kikamilifu kupitia kifungo cha roho ya udhaifu; uchovu usio na maelezo au magonjwa yanayogomea tiba ya hospitali mara nyingi ni programu za kishetani zilizorushwa rohoni na kuchukua sura ya kawaida ya kibinadamu mwilini.

Matendo ya Mitume 12:1-11, shetani anamtumia Mfalme Herode kulitesa kanisa; Herode anamuua Yakobo kwa Upanga na kanisa linakaa kimya na kuchukulia tukio lile kwa mazoea na kuliangalia kama changamoto ya kawaida ya kisiasa. Miongoni mwa adui mkubwa wa nguvu za Mungu katika kanisa ni mazoea (familiarization) na kushusha mambo ya Mungu kwenye kiwango cha kawaida cha kibinadamu (equalization). Kama wana Mungu, ni lazima kuwa wapya kila siku. Usiizoee injili wala kuuzoea wokovu.

Kukamatwa kwa Petro kulizua mapinduzi ya kiroho; kanisa liligundua uhusiano uliopo kati ya matukio ya mwilini na mipango ya kichawi, likakataa mtazamo wa kawaida, na kusimama kwa ujasiri kupitia 'maombi ya bidii' (Matendo 12:5). Nguvu hii ya maombi ya pamoja ya kivita ndiyo iliyolazimisha kuingilia kati kwa mamlaka ya mbinguni, ikashusha malaika ndani ya gereza, na kusababisha mageti ya chuma kujifungua yenyewe kwa nguvu ya Mungu na Petro akawa huru.

Maombi ya vita ndiyo suluhu ya kila tukio la kichawi. Bila vita hakuna kumiliki; ni lazima kuamsha moyo wa vita. Mungu alishatoa Baraka zoke, ila kuna watu wametia giza, ndiyo maana Daudi anasema katika Zaburi 35, Bwana atete nao wanaoteta nasi na apigane nao wanaopigana nasi. Ifahamike kuwa ufalme wa Mungu hauna mjadala; ni kwa wenye nguvu tu (Mathayo 11:12).

Kwahiyo, ufunguo wa kumiliki baraka zako ni kuwa na moyo wa vita. Moyo wa vita ni kuomba kwa mamlaka. Ukimpokea Yesu unapewa mamlaka (ruhusa au kibali cha kisheria kiroho). Haihitaji sabuni ya upako, maji, wala vitambaa, bali ni kutumia jina la Yesu kwa ujasiri na sauti ya mamlaka kama ya jeshini. Kwa maombi ya mamlaka, utapita katikati ya kila jaribu huku ukimshukuru Mungu kwa kukupa nafasi ya kujifunza vita vya ngazi husika. Imeandikwa katika Yohana 14:13-14 kuwa, “Nanyi mkiniomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”

Maombi ya vita:

Kuanzia sasa hivi, kila aliyepanga mabaya, kifo, hasara, au laana juu yangu,

nayarudisha kwake; kwa jina la Yesu!

Sitafilisika, sitapata ajali, na nitamaliza maisha yangu nikiwa na viungo vyote na akili timamu; kwa jina la Yesu!

Sitazika mtoto wala mjukuu wangu, bali nitashiba siku; kwa damu ya Yesu!

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments