UFUFUO
NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA
YA JUMAPILI 25.10.2026
BISHOP DR. GERSHOM
MWAKILA
SOMO:
SHAURI LA BWANA NA
KIBALI CHA MTU
![]() |
Hila ni ujanja
ujanja unaokuwa ndani ya mtu, au nia mbaya iliyofichwa. Biblia inasema hila
hizi ni nyingi sana na zinaweza kuwa zinashindana na wewe bila wewe kujua.
Jambo la muhimu sana ni kwamba, hila hazitoki kwa watu walio mbali; iangalie
hila kwa watu walio karibu sana na wewe.
Katika mwanzo wa
dunia, wakati hakuna mganga wa kienyeji, hakuna mchawi, wala hakuna jirani,
dunia ikiwa na watu wanne tu (Adam, Eva, Kaini, na Habili), hila ilionekana
ndani ya familia. Kaini alimwonea hila mdogo wake Habili na kumuua. Kifo kile,
hasara, na mikosi vilikuwa ni chanzo cha hila. Hata hivyo, bila kujalisha wingi
wa hila za wanafamilia, wanaukoo, wanakwaya, au wafanyakazi wenzako, SHAURI LA
BWANA NDILO PEKEE LITAKALOSIMAMA NA KUDUMU VIZAZI NA VIZAZI. Kama Mungu angeruhusu
maisha yako yaongozwe na hila za watu, usingekuwa hapo ulipo leo.
KIBALI:
Kila mtu
aliyezaliwa analo shauri ambalo ni kusudi la Mungu la kuishi kwa mtu huyo hapa
duniani. Ili uweze kulitekeleza kusudi hilo kwa wepesi bila kukwama, Mungu
amelitengenezea kitu kinaitwa Kibali.
Kibali maana
yake ni mvuto, neema, upendeleo, au kukubalika anakokuwa nako mtu wakati wa
kutimiza hatima ambayo ndiyo kusudi la Mungu. Baba yetu amekuwa akisisitiza kwamba ni kanuni ya huduma kuwa “kumtumikia
Mungu ni kuwatumikia watu’, kwa hiyo ni lazima upate kibali kwanza kwa
watu unaowatumikia. Elimu ni ya muhimu, lakini bila kibali humuacha mtu
akihangaika. Wapo watu wana elimu za juu lakini bado maisha yao ni ya
mahangaiko na hayaeleweki kwa sababu hawana kibali. Misaada ya wazazi na ndugu
ipo lakini ina kikomo; kibali hakina kikomo. Kibali kinavuka mipaka yote ya
elimu na misaada ya wazazi, ndugu na jamaa.
Mambo yote
yanaratibiwa na wakati. Unapotimia utimilifu wa wakati, kibali kinahitajika ili
mtu aishi kusudi la Mungu. Imeandikwa katika Warumi 8:28 kuwa, “Nasi
twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”
Neno hili
linatufundisha kwamba, katika MAMBO YOTE yanayohusu maisha yetu, iwe ndoa,
biashara, ajira, au safari, Mungu hufanya kazi na watu. Sasa, ili yale mema
yaliyoshikiliwa na hao watu yakufikie, ni lazima upate KIBALI mbele zao. Kwa
mfano, wakati wa binti wa kuolewa ukifika, haitatosha tu kuwa wakati umefika;
binti huyo atahitaji kibali kiasi kwamba mume akimuona aseme: "Sijawahi
kuona binti wa namna hii tangu nizaliwe", hata kama wengine
wanaona ni binti wa kawaida tu.
KIBALI
KINA NGUVU:
Kibali kina
uwezo wa kumpeleka mtu mahali ambapo mipaka ya mambo yote haiwezi kufika.
Kibali kikipungua, elimu, nguvu, umaarufu na kila uwezo wa binadamu, haviwezi
kusaidia. Unaweza ukawa umefanya maombi na kufunga sana, lakini bado
hujafanikiwa; ni kibali tu umekosa.
MIFANO
KATIKA BIBLIA KUHUSU NGUVU YA KIBALI:
1.
Musa
na Wazee Sabini (70):
Hesabu
11:16-17
Wakati
wana wa Israeli (wanaume zaidi ya laki sita, bila kuhesabu wanawake na watoto)
walipomnung'unikia Musa wakitaka nyama, Musa alichoka na kumlilia Mungu. Mungu
hakwenda kuchagua watu yeye mwenyewe; alimwambia Musa: “Nikusanyie watu sabini, miongoni
mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na
maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe.
Ni
wazi kuwa Musa aliwachagua watu hao kwa viwango vyake mwenyewe. Viwango vya
kiongozi wako ndio viwango vya Mungu wako; ukichaguliwa na kiongozi wako, ndio
umechaguliwa na Mungu. Ili wale wazee wateuliwe na kupokea sehemu ya roho
iliyokuwa juu ya Musa, walihitaji kwanza kupata kibali machoni pa Musa
Eldadi
na Medadi hawakuwepo kwenye kusanyiko lakini kwa sababu walikuwa kwenye orodha
na walikuwa na kibali mbele ya Musa, roho iliwashukia hata wakiwa nje ya hema.
Hata kama haupo ofisini siku ya Jumapili, kibali kitalazimisha jina lako
lizunguke kwenye kichwa cha bosi wako na utatajwa kwenye orodha ya mafanikio
bila wewe kuwepo eneo husika la kazi.
2.
Kornelio
na Petro:
Matendo
10:4-6, 13-20
Malaika
alimwambia Kornelio atume watu kwenda Yafa kumwita Petro. Kornelio alichagua
watumishi watatu kulingana na wale waliokuwa na kibali machoni pake; Kornelio
hakuchagua watu kwa bahati nasibu. Hao watatu walipofika kwa Petro, Mungu
aliingilia kati akasema: "Ondoka ushuke ufuatane nao... kwa
maana ni mimi niliyewatuma." Ukichaguliwa na mamlaka iliyopo (kama
Kornelio), Mungu anaingilia mchakato huo na kuufanya kuwa wake.
Ukikataa
kutumwa na kiongozi au mamlaka iliyopo, unakuwa umekataa kutumwa na Mungu. Kibali
cha Kornelio kiliwageuza watumishi wa kawaida kuwa wajumbe wa Mungu mbele ya
Mtume Petro, na hivyo wakapokelewa kwa heshima kubwa sana.
3.
Gidioni
na Roho ya Wamidiani:
Waamuzi
6:16-19
Wakati
taifa la Israeli lilipokuwa chini ya utumwa wa Midiani, ambapo roho ya Midiani
ilikuwa inawaruhusu walime, wafuge, lakini ikifika wakati wa kuvuna inawaibia
matunda ya kazi zao, Malaika alimtokea Gidioni na kumwambia atawapiga
Wamidiani. Gidioni hakukurupuka, alijua kabisa kuwa nguvu na ahadi pekee
hazitoshi bila kibali; alisema: “Kama nimepata kibali mbele za
macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami.”
Gidioni
alitaka kibali kitakachomtofautisha na wengine. Kibali ndicho kinachofanya watu waache duka au
saluni iliyo karibu na kwenda kwenye duka la mbali lenye bidhaa ile ile, kwa
sababu tu kuna mtu ana kibali cha kukutofautisha.
4.
Esta
na Mfalme Ahasuero:
Esta
2:17
Baada
ya malkia Vashti kupoteza kibali, mabikira wengi walikusanywa ili mfalme
achague mke (malkia). kigezo ilikuwa ni ubikira, lakini mfalme akampenda Esta
kuliko wanawake wote kwa sababu Esta alipata neema na kibali. Kibali
kinakunyanyua juu ya vigezo vilivyowekwa.
NGUVU YA KIBALI
1.
Kibali
kinazidi Elimu, Uzoefu na Kujulikana:
Ikitokea
wakakusanywa watu 200 wenye digrii sawa na GPA sawa na yako, ni kibali pekee ndicho
kinachomshurutisha bosi kukuona wewe unafaa kuliko wengine wote ambao kimsingi
mna sifa zinazofanana; na ukishapewa taji kwa sababu ya kibali, heshima inakuja
yenyewe bila wewe kuiomba.
2.
Kibali
Kinaheshimisha (Hesabu 27:18-20):
kibali humheshimisha mtu aliyedharauliwa.
Mungu alimwambia Musa amwekee Yoshua mikono mbele ya mkutano na kumpa sehemu ya
heshima yake ili wana wa Israeli wamtii. Heshima nayo huhamishika; ukipata
kibali mbele ya mtu mwenye heshima (mamlaka), ana uwezo wa kumega sehemu ya
heshima yake na kuihamishia kwako.
Heshima
haitafutwi kwa kulazimisha watu au kupiga kelele. Ukiona unalazimisha
kuheshimiwa, ujue kibali kimeondoka. Kibali kikirudi, kinarudisha heshima kama
ilivyokuwa kwa Esta aliyekuwa akidharaulika lakini mara alipokuwa malkia watu
wale wale wakaanza kumnyenyekea.
3.
Kibali
Kina Nguvu ya Kukufanya Utafutwe na Watu:
kibali ni kama sumaku; ukiwa nacho, kinavutia vitu
vingine vyote vizuri vije kwako. Kibali kina nguvu ya kuvutia
wateja, fursa, mitaji, na watu wa kukusaidia bila wewe kutumia nguvu nyingi.
Kisa cha
Daudi (1
Samueli 16:7): Daudi alikuwa ameachwa porini na kusahaulika na
baba yake Yese wakati Nabii Samueli alipokuja kuteua mfalme. Samueli alitaka
kuwatazama kaka zake Daudi waliokuwa warefu na wenye muonekano mzuri, lakini
Mungu alimwambia: “…
Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana
haangalii kama binadamu aangaliavyo; ...”
Kibali
kina nguvu ya kusimamisha shughuli zote za mjini au ofisini mpaka utafutwe
kwanza wewe uliyopo kijijini, kama Daudi alivyosubiriwa afike.
DALILI TISA (9) ZINAZOONESHA KUWA
HAUNA KIBALI
1.
Kuishi maisha ya kuhangaika sana. Hauna
ufumbuzi wa matatizo madogo madogo. Kupata kodi, chakula, au hata nauli ya chai
inakuwa ni taabu inayokutoa jasho.
2.
Mwenza wako hakupendi tena. Wakati wa
kuvalishana pete mlikuwa na malingo na manjonjo mengi, lakini ghafla mume au
mke anageuka kuwa mbogo na anakuambia upendo umeisha, kana kwamba upendo ni
maji yanayopungua kwenye chupa.
3.
Kufanya kazi kwa bidii bila kupandishwa
cheo. Wewe ndiye unayeaminika kuwahi ofisini, unapewa burungutu la funguo
kufungua na kufunga ofisi; lakini panapofika promotion au safari za nje,
wanaochelewa ndio wanaopewa, huku wewe ukipewa sifa kuwa wewe ni mchapakazi
unayestahili kuwa ofisini. Funguo hazisaidii kubadilisha cheo chako.
4.
Sio rahisi kwako kupata kazi. Tangu umehitimu
chuo, ni muda mrefu umepita, mfano, mwaka wa tano sasa, unaitwa kwenye usaili
mbalimbali lakini huchaguliwi, mpaka unaanza kuwaza kufungua genge la nyanya.
5.
Kupoteza ushawishi kwa watu. Ukisimama
kuongea au kutoa wazo zuri kwenye kikao, watu hawana hamu ya kukusikiliza. Ndio
kwanza unaona wengine wanaenda chooni, wengine wanajifanya wanaongea na simu,
au wananong'ona. Hausikilizwi.
6.
Haupendwi na yeyote. Hata ukienda dukani
ukiwa na fedha yako mkononi kununua bidhaa, muuzaji anakuletea mbwembwe na
kukuona kama usumbufu.
7.
Wewe mwenyewe haujikubali. Conviction ya
ndani inakuambia kabisa, hili jambo huliwezi, utashindwa, utachekwa, au
utaaibika; inakuondolea kabisa ujasiri wa kutumia fursa.
8.
Biashara yako haifanikiwi. Unabidhaa
bora kuliko wenzako kwenye biashara lakini hupati wateja, kinyume chake,
wenzako wenye bidhaa dhohofu ndio wanapata wateja sana.
9.
Roho ya kukataliwa na mfululizo wa
mikosi. Kila unachofanya kinaleta tukio la kuharibikiwa, kuharibu mambo ya
wengine na hali ya kuchokwa.
NAMNA AMBAVYO SHETANI ANAZUIA AU
KUIBA KIBALI CHA MTU
1.
Kibali
Kimefunikwa:
Ezekieli
28:14 inasema shetani alikuwa kerubi wa kufunika. Ana
uwezo wa kukupiga kifuniko cha magonjwa, vifungo, au tabia mbaya (kama kiburi
na dharau) ili usionekane. Mtu anaweza akawa amepigwa kifuniko cha
kuchanganyikiwa au ugonjwa, kiasi kwamba wanaotaka kumchumbia au kumuajiri wanaona
hawezi. Yesu anaweza kuondoa vifuniko hivyo.
2.
Kibali
Kimeibiwa:
Yohana
10:10 inasema mwizi haji ila aibe, achinje, na kuharibu.
Shetani anaiba vibali na nyota za watu na kuzishikilia kwenye mashimo ya kichawi
au magereza ya kiroho ili mtu asipate kazi wala cheo. Wengine kibali kikiibiwa,
wavulana wanamuona msichana kama mvulana mwenzao na kumuita "kaka"
wakati ni dada, kwa sababu mvuto wa kike umeibiwa. Kristo alikuja kutafuta na
kuokoa kilichopotea.
MAOMBI YA KIBALI
CHA MTU:
Baba Mungu nimeinua
mikono mbele zako ninasalimisha maisha yangu kwako. Ninakuomba Bwana Yesu kibali
kutoka kwako ili niweze kutumikia shauri langu katika maisha yangu; Kibali cha
biashara, kibali cha ndoa, kibali cha safari, kibali cha utawala, kibali cha
masomo, kibali cha ajira, kibali cha kumiliki mali!
Bwana ninaomba leo uso wako na
kibali chako kiwe pamoja nami, na usiponipa leo sitoki mahala hapa!"
Ninataka kibali cha kunitofautisha na wafanyakazi wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na waajiriwa wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na Watanzania wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na wahubiri wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na waimbaji wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na waombaji wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na watoaji wengine! Ninataka kibali cha kunitofautisha na wafanyabiashara wengine! Leo ninataka kibali changu, kwa jina la Yesu Kristo; Amen!"


0 Comments