google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUBOMOA MADHABAHU ZA KISHETANI: MADHABAHU ZA FAMILIA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 01.11.2026
BISHOP DR. GERSHOM MWAKILA
SOMO: KUBOMOA MADHABAHU ZA KISHETANI: MADHABAHU ZA FAMILIA

Madhabahu kimsingi ni daraja; ni eneo maalum ambapo ulimwengu wa mwili (unaoonekana) na ulimwengu wa roho (usioonekana) vinakutana na kuingiliana. Ni kiunganishi kati ya ubinadamu na uungu.

Kuna sheria kali za kiroho zinazozuia viumbe wa rohoni (malaika wa Mungu, na hata upande wa pili kama majini, pepo wachafu, au majoka) kuja kufanya kazi au kuoperate kwenye ulimwengu wa mwili bila kibali. Ili wapate ruhusa na uhalali wa kisheria kuingia duniani, ni lazima ruhusa hiyo itolewe kutokea madhabahuni. Madhabahu ina nguvu ya kuruhusu viumbe hawa kuingia au kuwazuia wasitende kazi.

Mfano wa madhabahu ni kanisani; kila mtu, kuanzia aliye mbele hadi aliye nyuma, ameelekeza kiti chake kuangalia mbele, sio kwa sababu ya kusikiliza maana hata ukiweka kiti chako kuelekea nyuma bado sauti utaisikia. Watu wote wanaangalia mbele kwa sababu mbele ya wote ndipo ilipojengwa madhabahu ya Mungu, na hapo ndipo mahali ambapo uungu na ubinadamu vinakutana.

Neno: Luka 1:10-11

Wakati kuhani alipokuwa akifanya ibada na kufukiza uvumba madhabahuni, malaika wa Bwana alitokea akasimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Hii inathibitisha kuwa madhabahu ndipo mahali pekee ambapo muingiliano wa viumbe wa rohoni na wa mwilini unafanyika.

Vitu Vitano Vinavyopelekea Kuwepo Kwa Madhabahu Yoyote:

Madhabahu yoyote ile, iwe ni ya Mungu wa mbinguni au ya kishetani (kama za kichawi na kishirikina), ili ikamilike na kuitwa madhabahu, ni lazima iwe na vitu vitano vifuatavyo:

1.   Madhabahu Yenyewe: Muundo au mahali panaposimama kama daraja la kiunganishi kati ya roho na mwili.

2.   Kuhani wa Madhabahu: Kila madhabahu ina kuhani wake anayeihudumia juu yake. Hata asipoonekana kwa macho, yupo. Waganga wa kienyeji, wapiga ramli, na wachawi ndio makuhani wa madhabahu za kishetani, wakati watumishi wa Mungu ndio makuhani wa madhabahu takatifu.

3.   Mungu wa Madhabahu: Mamlaka kuu ya kiroho inayotambuliwa na kuabudiwa hapo. Upande wa Mungu ni Yehova, na upande wa giza ni shetani.

4.   Kafara au Sadaka ya Madhabahu: Hii ni dhabihu inayotolewa juu ya madhabahu kwa mamlaka ya rohoni ya madhabahu hiyo. Sadaka ndiyo inayofanya madhabahu izungumze na inatia nguvu maagizo ya kiroho.

5.   Washirika wa Madhabahu: Hawa ni watu walio na mahusiano ya kiagano na madhabahu hiyo, ambapo mambo ya madhabahuni yanawahusu moja kwa moja. Baraka au laana zinazotoka madhabahuni zinashuka kwa washirika hawa.

Sisi tunaomwamini Mungu na kumjengea madhabahu, kwa sasa hatuchomi kuni wala kuleta kafara za wanyama kama mbuzi, ng'ombe, au njiwa kwa sababu Yesu Kristo alichinjwa mara moja tu na Yeye ndiye Kafara ya milele ya madhabahu hii, na damu yake ina nguvu ya kuleta majibu. Vilevile hatuleti moto wa kuni kwa sababu Roho Mtakatifu ndiye Moto wa madhabahu yetu.

Historia Ya Madhabahu Na Tabia Yake Ya Kutokusahau:

Madhabahu ilianza na Mungu wa mbinguni, na shetani hajawahi kuanza chochote isipokuwa kuiga na kupotosha.

1.   Madhabahu ya Nuhu (Mwanzo 8:20-21)

Baada ya kutoka kwenye janga la gharika ambalo liliangamiza wanadamu wote isipokuwa watu wanane, jambo la kwanza kabisa ambalo Nuhu alilifanya halikuwa kupumzika au kujenga nyumba yake, bali alimjengea Bwana madhabahu na kuchukua wanyama safi na kutoa sadaka ya kuteketeza. Biblia inasema Mungu akasikia harufu ya kumridhisha na akasema moyoni mwake: “Sitailaani nchi tena...”

Tunachojifunza hapa: Sadaka Inamfanya Mungu Azungumze. Mungu alikuwa kimya tangu Nuhu akiwa ndani ya safina, lakini harufu ya sadaka ilimfanya aongee na kutoa agano la kutosababisha mauti tena. Ukitoka kwenye shida, ajali, au taabu, jambo la kwanza ni kutengeneza daraja la shukrani na Mungu kupitia sadaka yako ili Mungu anene mema juu ya kesho yako.

2.   Madhabahu Hazisahau Maombi Wala Maagizo

Madhabahu iliyojengwa na Musa (Kutoka 17:15-16): Musa alipopigana na Amaleki alijenga madhabahu akaiita Yehova-Nisi (Bwana ni Bendera yangu). Musa alitoa tamko juu ya ile madhabahu kuwa Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi. Miaka mingi ilipita, Musa akafa, Waamaleki wakasahau kabisa tukio lile.

Hata hivyo, baada ya miaka mingi kupita, katika kipindi cha Mfalme Sauli, Mungu wa ile madhabahu alimwamsha Nabii Samweli na kumwambia, amekumbuka mambo ambayo Amaleki aliwatenda Israeli hivyo Wamaleki wapigwe na kuharibiwa kabisa. Hii inafundisha kuwa madhabahu haisahau. Unaweza ukaomba ukiwa madhabahuni ukiwa kijana kisha ukasahau, lakini madhabahu haisahau, itamkumbusha Mungu na kukuletea majibu hata baada ya miaka 10 au 20.

MADHABAHU ZA FAMILIA NA MATOKEO YAKE:

Kila mwanadamu duniani ametokea kwenye familia, iwe ni nuclear family, extended family, au single parent family. Kanisa, mtaa, wilaya, mkoa, na nchi ni mkusanyiko wa familia mbalimbali, na ndio maana tabia za familia zinaakisi mkoa au nchi husika.

Kuhama kwa Laana na Tabia Ndani ya Ukoo: Kama vile mzee wa kijijini anaweza akawa amejenga madhabahu ya kishirikina na kupanda mti wa Ashera (mti wa kichawi) ambao hataki mtu auguse au kuuchezea mida ya jioni, ile madhabahu inakuwa na nguvu juu ya uzao wake wote. Hata kama mzaliwa katika ukoo huo hajui au hajihusishi na uchawi huo, kwa kuwa ni mshirika wa damu wa familia ile, anajikuta unapatwa na madhara ya ile madhabahu.

Mfano: “Ukienda hospitali unaumwa kisukari au presha, madaktari watakuuliza: 'Je, kwenye ukoo wenu kuna mtu mwenye shida hii?' Utasema ndio, mama alikufa nacho, kaka anacho. Sayansi inaita ugonjwa wa kurithi, lakini kiroho kuna kimadhabahu kilichojengwa kando ya ukoo kuruhusu ugonjwa huo usafiri kwa kila anayezaliwa. Lazima ivunjwe!”

Mifano katika Biblia:

1.   Akani (Yoshua 7:24-25) - Uangamizaji wa Familia: Wakati wa vita vya mji mdogo wa Ai, Israeli walishindwa vibaya. Yoshua alipomlilia Mungu, akajibiwa kuwa kuna kosa limefanyika. Walipopitisha familia kwa familia, Akani alipatikana na hatia ya kuiba dhahabu na joho vilivyowekwa wakfu kule Yeriko. Akani alikuwa ametengeneza madhabahu ya wizi ndani ya hema yake. Adhabu haikumwangukia Akani pekee, bali Yoshua alimtoa yeye, wanawe, binti zake, mifugo yake, na hema yake, wote wakapigwa mawe na kuteketezwa kwa moto. Kosa la mtu mmoja lilileta maafa kwa ukoo mzima.

2.   Rahabu (Yoshua 6:24-25) - Wokovu wa Familia: Kwa upande mwingine, mtu mmoja anaweza akawa chanzo cha wokovu wa ukoo wake mzima. Rahabu alikuwa kahaba wa Yeriko ambaye hakuwa na thamani machoni pa watu. Lakini alipoamua kuwapokea, kuwalinda, na kuwapa siri za nchi wapelelezi wa Israeli, aliingia nao agano. Wakati mji wa Yeriko ulipoangamizwa na kuteketezwa kabisa, Rahabu na watu wote wa nyumba ya baba yake waliokolewa na kuhifadhiwa. Wema wa mtu mmoja uliokoa extended family nzima na kumfanya Rahabu aingie hadi kwenye kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo.

Jinsi Ya Kushughulikia Madhabahu Za Kishetani:

Kama ilivyokuwa kwa Gidioni katika kitabu cha Waamuzi sura ya 6, ambapo aliongozwa na hofu kwa sababu ya madhabahu ya Baali iliyokuwa nyumbani kwa baba yake mzazi (Yoashi), malaika alimwamuru kwenda kuibomoa. Kuna kazi tatu kubwa tunazopaswa kuzifanya kiroho ili kupata ufumbuzi wa asilimia mia moja.

1.   Kuvunja na Kubomoa Madhabahu: Kuharibu miundo yote ya kichawi na malango ya kuzimu yaliyosimama kama daraja kwenye ukoo wenu ili kuifanya iwe vifusi.

2.   Kumkamata na Kumfunga Kuhani wa Madhabahu: Kushughulika na mawakala wa kiroho (pepo wachafu au roho zilizowekwa kusimamia laana hiyo). Ukivunja madhabahu bila kumfunga kuhani, ataenda kujenga madhabahu nyingine mbele yako. Ni lazima afungwe kwa minyororo ya kiroho.

3.   Kuangamiza na Kunyamazisha Kafara za Madhabahu: Kuharibu dhabihu zote (za damu ya wanyama, ndege, au wanadamu) zinazozipa sauti madhabahu hizo, na kuzinyamazisha kwa kutumia Kafara kuu ya Damu ya Yesu Kristo.

Huwezi ukasimama kuvunja madhabahu ya kishetani wakati wewe mwenyewe huna Mungu ndani yako, shetani atakushinda! Hatua ya kwanza ni kumkaribia Mungu na kumpa Yesu maisha yako kuwa Bwana na Mwokozi, ili uwe salama wakati wa vita. OKOKA.

MAOMBI YA VITA:

Baba Mungu wa mbinguni, ninavaa moyo wa vita kuanzia sasa kinyume na madhabahu zote zilizojengwa ndani ya familia yangu na kwenye ukoo wangu kwa jina la Yesu!

Ninajiweka wakfu leo kwa ajili ya vita hii. Imeandikwa, nimejengwa juu ya mwamba, wala malango ya kuzimu hayataweza kunishinda!

Ninasimama kama rungu la Bwana kinyume cha madhabahu ya magonjwa, madhabahu ya umaskini, madhabahu ya mateso, madhabahu ya utasa, mikosi, laana, na talaka ndani ya familia yetu!

Ewe kuhani wa madhabahu za kichawi, nakufunga leo kwa minyororo ya chuma! Ninakufunga kwa damu ya mwanakondoo! Mbingu zimefunga mamlaka yako kuanzia sasa!

Ninachukua nyundo ya kiroho, ninabomoa madhabahu zenu zote na kuzigeuza kuwa vifusi! Ninaangamiza kila kafara iliyotolewa juu ya madhabahu zenu, iwe ni kafara ya wanyama, ndege, au damu yoyote; ninazinyamazisha zote kwa Damu takatifu ya Yesu Kristo! Nanyamazisha kila sauti inayonena matatizo na mkwamo juu ya maisha yangu!


Ninawasha moto wa Roho Mtakatifu juu ya kila kiumbe cha kiroho; majini, mizimu ya ukoo, pepo wachafu, majoka, walioruhusiwa na madhabahu za familia kuja kupindisha maisha yangu, ndoa yangu, au afya yangu!

Teketea kwa jina la Yesu! Ninaondoa nuksi, balaa, na huzuni. Madhabahu ya Bwana inasema: 'Tazama, nafanya mambo yote kuwa MAPYA!' Mambo yangu yanakuwa mapya, biashara mpya, afya mpya, na ustawi mpya kuanzia sasa, kwa Jina la Yesu; Amen!”

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments