google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADHABAHU NA HATIMA YA MTU

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 15.11.2026
BISHOP DR. JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: MADHABAHU NA HATIMA YA MTU 

Neno hatima (destiny) linamaanisha jinsi maisha yako yatakavyomalizika hapa duniani. Siku ya msiba wako wasifu (usia) wako ukisomwa, watu watasema ulizaliwa wapi, ukasoma wapi, na mwisho watamaliziaje? Je, watasema "umauti ulimkuta akiwa kwenye nyumba yake ya ghorofa," au watasema "alifia kwenye nyumba ya kupanga akiwa anabangaiza maisha"? Hilo neno la mwisho ndilo hatima yako. Mungu ana sifa ya kipekee ya kujua mwisho wa mtu kabla ya mwanzo wake.

Mungu anaamua miisho yetu tangu mwanzoni; imeandikwa katika Isaya 46:10, “nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

1.   KWANINI TUNAPITIA VITA?
Tunapitia vita kwa sababu ulimwengu wa giza unao uwezo wa kuona hatima zetu. Shetani, waganga, wachawi, na mapepo wanajua mwisho wa maisha ya mtu. Wanapopambana na wewe, hawashindani na sura yako ya sasa wala hali yako duni; bali wanaiona kesho yako iliyosheheni mambo makubwa. Wanajua ukifikia hatima yako utaharibu "vihenge" na madhabahu zao, ndiyo maana wanataka kukuua au kukukwamisha leo kabla hujafika huko. Hii ndiyo sababu wewe tu ndiye unayefuatwa na magonjwa, chuki kazini, au matatizo ya kifamilia; utakuta mtu anayezongwa na mambo kama hayo mara nyingi huishia kusema "Why me?".
2.   HATIMA KUBWA HUANZIA KWENYE UDHAIFU
3.   KUKATALIWA NA WATU NA KUTOBADILIKA KWA MPANGO WA MUNGU:
4.   MAANA YA MADHABAHU NA JINSI ZINAVYOZUIA HATIMA
5.   MAMLAKA YETU NA VITA VYA KIROHO

Ukisoma Marko 1:34 na Luka 4:41, utaona kwa ushahidi wa wazi kuwa ulimwengu wa giza unatujua; Yesu aliyazuia mapepo yasiongee kwa sababu yalimjua tangu kuzaliwa kwake, kufa kwake, hadi kufufuka kwake, wakati wanadamu walimwona kama mtoto wa Yusufu fundi seremala tu.

Mifano katika Biblia:

a)    Mamajusi wa Mashariki: Walikuwa wanajimu/wachawi walioiona nyota ya Yesu akiwa kichanga cha siku chache na wakajua huyu ni mfalme.

b)   Mchawi Balaamu (Hesabu 24:17): Alikodiwa kwenda kuwalaani Waisraeli milimani. Alipoangalia kundi la mamilioni ya watu, roho yake ya kichawi haikuona umati, bali iliona "nyota moja ikitoka katika Yakobo" (Yesu) itakayowavunjavunja.

c)    Kijakazi wa Wafilipi na Wana wa Skewa (Matendo 16:16-18 & 19:13-16): Pepo ndani ya yule binti lilimtambua Paulo kuwa ni mtumishi wa Mungu aliye juu, na mapepo mengine yaliwaambia wana wa Skewa, "Yesu tunamjua na Paulo tunamjua, ninyi ni akina nani?"

d)   Mfalme Farao: Alinusa kiroho kuwa kuna "jitu" (Musa) linataka kuzaliwa kuwakomboa watumwa, ndipo akatoa amri watoto wote wa kiume wauliwe.

Ni kanuni ya Mungu kuanza na mtu akiwa dhaifu, mnyonge, na asiye na kitu, ili akimwinua dunia ijue ni Mungu amefanya. Imeandikwa katika 2 Wakorintho 12:10, kuwa, “Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” Mungu huwapa nguvu wazimiao na wamngojao watapaa kama tai (Isaya 40:29-31).

Maisha ni kama uumbaji wa dunia ulioanza na jioni kisha asubuhi (Mwanzo 1:5, 8, 13, 19, 23, 31). "Jioni" ni kipindi ambacho huna nyumba, huna mtaji, huna ada ya watoto, kodi imeisha, au umeolewa na mwanaume mkorofi unashindwa hata kuwaambia ndugu zako kwa sababu ulimchagua mwenyewe. Lakini kukiwa na jioni, asubuhi ipo. Ukuu hauanzi kwa bidii ya mtu, bali Mungu hupanda mbegu ya ukuu ndani yako kwanza, na mbegu hiyo ndiyo inayokupa bidii.

Mifano katika Biblia:

a.    Ibrahimu: Alitoka kwao akiwa mnyonge, akitembea kwa mguu bila kujua anakokwenda, hata mkewe Sara na watumishi walipomuuliza hakuwa na jibu ila alifuata maelekezo ya Mungu pekee, lakini akawa baba wa imani.

b.   Musa: Alianza akiwa mtoto mchanga anayeelea kwenye kikapu mto Nile katikati ya mamba, kisha akakimbilia jangwani miaka 40 akiishi ukweni, ndipo akakutana na Mungu mlimani Horebu na kuwa mkombozi pekee aliyeongea na Mungu uso kwa uso.

c.    Daudi na Mzee Yese: Nyumbani kwao kulikuwa na watoto saba, lakini baba yao (Mzee Yese) alimpuuza Daudi na kumtuma kuchunga kondoo porini kwa sababu alimwona kama "kilaza" (gone case), wakati ndugu zake walioonekana wasomi walipangwa mbele ya nabii Samweli. Mungu alimkataa kila mtu hadi Daudi alipoitwa kutoka porini na kupakwa mafuta kuwa mfalme.

d.   Nabii Eliya: Alivaa shuka la ngozi, alikula nzige na asali, na hakuwa na makazi maalum, lakini alikuwa na mamlaka ya kumwambia mfalme kuwa hatatoka kitandani atafia hapo.

Mifano ya Maisha Halisi:

i)             Baba, Askofu Gwajima alikuwa mgonjwa kwa miaka sita (6) akiwa hawezi kutembea na akibebwa, lakini kwa sasa ni kiongozi mkuu wa kanisa la maelfu (Kanisa la Ufufuo na Uzima);

ii)            Kanisa la Ufufuo na Uzima lilifungwa na polisi kwa miezi sita (6) waumini / washirika tukasali barabarani, lakini majaribu hayo yalikuwa yanatunoa tu;

iii)          Nelson Mandela alitoka gerezani akawa Rais wa nchi ya Afrika Kusini;

iv)          Mchungaji Yonggi Cho alianza kanisa kubwa duniani akiwa anakata roho kwa ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Kama watu uliowategemea (ndugu, marafiki, au bosi wako kazini anayekukandia wakati wewe ndiye unayefanya kazi zote) wamekuacha na hawakusaidii, Mungu ndiye aliyewatia nguvu wasikusaidie. Lengo lake ni ili atakapokushika mkono na kukuinua, wasije wakajisifu kuwa "nisingekuwa mimi usingefika hapo."

Yatupasa tutambue kuwa kumtegemea mwanadamu au kumfanya mtu kuwa kinga yako kunakufanya uwe kama mti uliopandwa katika nchi ya chumvi (ukame na kukosa matunda), kinyume chake, unapomtumaini Bwana pekee, unakuwa kama mti uliopandwa kando ya mto unaozaa matunda hata wakati wa ukame, kwa kuwa Mungu mwenyewe ndiye anayekushika mkono na kukuinua.

Kitabu cha Yeremia 17:5-8 kinatufundisha kuwa amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu, na amebarikiwa amtumainiye Bwana. When I am weak, I am strong! Mpango wa Mungu hauhaririwi, na wachawi hawawezi kuunakili na kuubandika, wala hawawezi kuubadilisha. Kupatia au kukosea hakubatilishi yale Mungu amempatia mtu kwenye maisha yake; kwenye milima au mabonde, jifunze. Kuna miaka saba ya shibe na miaka saba ya njaa.

Tofauti na wanadamu wanaochoka au kubadilika, Bwana anayekulinda na kuisimamia hatima yako halali wala hasinzii (Zaburi 121:1-4). Hata ukianguka mara saba, Mungu hahesabu kuanguka kwako, bali anahesabu uwezo wako wa kujipangusa na kuinuka tena kama ilivyoandikwa katika Mithali 24:16 kuwa “Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.”

Wakati wa udhaifu, tulia unolewe. Watu kutokukupenda haibadilishi mpango wa Mungu juu yako; siasa za familia zisikusumbue. Hata kama umezaliwa katika familia maskini na wazazi wako hawakuwa na kitu cha kukurithisha, unapoamua kumcha Bwana katika unyonge wako, Mungu hubadilisha historia. Wale walioonekana matajiri au wanaong'aa kwa njia zisizo za haki wanashuka, na utajiri au baraka zao zinahamishiwa kwako ili hatua kwa hatua upande juu na kuacha urithi kwa vizazi vyako (Mithali 13:22).

Mafanikio yanayotoka kwa waganga, wachawi, au madhabahu za giza yana masharti, laana, na hayadumu. Lakini baraka yoyote (mtoto, ndoa, kazi, au mtaji) unayoipata kutoka kwa Mungu (kama Hana alivyompata Samweli baada ya kuomba hekaluni) ni kamilifu. Kwa kuwa Mungu hana kugeukageuka wala kivuli cha kubadilika, anapokupa kitu au anapokushika mkono, hakuna mchawi wala adui anayeweza kukupokonya (Yakobo 1:17).

Mfano katika Biblia:

I.             Hana na Penina: Mzee Elkana alimwoa Hana, lakini kwa miaka mingi Hana hakuwa na mtoto. Elkana akaoa mke wa pili aliyeitwa Penina ambaye alizaa watoto sita na akawa anamdhihaki Hana (hata kumzuia kuwatuma watoto wake sokoni). Hana hakwenda kwa waganga; alikwenda hekaluni akamimina moyo wake kwa Bwana, na kuhani Eli akamtamkia neno la amani bila kumpa "chumvi wala sabuni ya upako." Hana alimzaa nabii Samweli ambaye alikuja kuwa mtu mkuu aliyebadilisha historia ya Israeli, wakati wale watoto sita wa Penina hawakutajwa hata majina yao kwenye Biblia.

Madhabahu ni daraja (bridge) au muunganiko (connectivity) unaounganisha ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili. Kuna madhabahu za aina mbili tu: za Mungu na za shetani. Ili madhabahu ikamilike lazima iwepo madhabahu yenyewe, kuhani, mungu wa madhabahu hiyo, na kafara.

Wachawi wanapokusanyika usiku kwenye viwanja vyao (chini ya miti, njia panda, mito, makaburini, au kwenye anga) na kutaja jina lako, wanakuwa wameifunga hatima yako chini ya madhabahu zao ili uwe na nuksi, usiolewe, au ufe mapema. Pia kuna madhabahu za ukoo, kabila, na taifa zinazowafanya watu wa kabila au nchi fulani wajione wanyonge.

Mara tu unapogundua kuwa hatima yako imeshikiliwa chini ya madhabahu, hatua ya kwanza ni kutua mzigo. Kupitia nguvu ya upako na maombi ya kubomoa madhabahu (kama Gideoni alivyobomoa madhabahu ya Baali ya baba yake), mzigo wa giza unaondolewa mabegani mwako na nira ya shetani iliyokuwa imekufunga shingoni inaharibiwa (Isaya 10:27).

Ukibomoa madhabahu, weka ulinzi. Kiroho, huwezi kubaki wazi (tupu) baada ya kuvunja madhabahu ya shetani, la sivyo adui atarudi na kuijenga upya. Ndiyo maana kanuni hii inaitwa "tua mzigo, beba mzigo". Mara tu unapotua nira ya shetani na kubomoa madhabahu yake, unapaswa kujenga madhabahu ya Mungu (kama Gideoni alivyojenga madhabahu ya Bwana) na kuvaa nira ya Yesu ambayo ni laini na mzigo wake ni mwepesi (Mathayo 11:29-30).

Mfano katika Biblia:

A.   Gideoni: Gideoni alizaliwa akiwa na hatima ya ushujaa, lakini aliishi maisha ya woga akilima kwa siri na kuficha ngano ili Wamidiani wasiichome moto. Malaika alipomtokea na kumwita "shujaa," Gideoni alikataa kwa sababu alijiona mwoga. Mungu alimwonyesha tatizo: baba yake (Yoashi) alikuwa amejenga madhabahu ya mungu Baali iliyokuwa inashindana na ujasiri wake. Mungu alimwamuru aibomoe usiku na kujenga madhabahu ya Bwana. Alipoibomoa, alishinda jeshi kubwa la Wamidiani kwa kutumia askari 300 tu, kwa sababu ukivunja madhabahu vita haihitaji watu wengi.

Hatupaswi kukaa kimya na kusema "namwachia Mungu" tu, kwa sababu Mungu ameshatupa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge (Luka 10:19). Kumwachia Mungu ni "kujiachia," kwani sisi ni wana wa Mungu tuliopewa uwezo wa kubomoa na kung'oa kazi za giza wenyewe kwa jina la Yesu (Yeremia 1:5, 10).

Hata hivyo, huwezi kumshambulia shetani kama hujaokoka, kwa sababu atakushambulia wewe (Yohana 9:31). Hatua ya kwanza ni kuokoka na kujitakasa kwa damu ya Yesu, kisha kufuta jina lako, familia yako, na biashara zako kwenye madhabahu za wachawi, na kuamuru jina lako litajwe mahali pa heshima (kama wizarani, Umoja wa Mataifa, na kwa wafalme) ili utoke shimoni.

Yesu aliposema "Aliyeniona mimi amemwona Baba," alionesha umoja wake na Mungu. Kwa kuwa sisi tumeokoka na kuwa wana wa Mungu (ndugu zake Yesu), tumepewa uwakilishi huohuo hapa duniani. Unaposimama kuomba na kutamka neno la kubomoa madhabahu kwa jina la Yesu, ni Mungu mwenyewe anayetenda kazi kupitia kinywa chako, na kazi alizofanya Yesu za kufungua waliofungwa nawe unazifanya.

6.   VITA NA KANUNI ZA KUPIGANA VITA

i)             Hakuna Mafanikio ya Bure: Maisha ni vita, na hakuna kitu kinachokuja kwenye sahani ya dhahabu ukiwa umelala. Ili kumiliki hatima yako, lazima upambane katika ulimwengu wa roho ili uyazimishe mashetani na vibwengo vilivyolalia kesho yako viachie (Waefeso 6:12).

ii)            Mungu ni Mtu wa Vita: Mungu anapenda kuona watoto wake wakipigana na kushinda. Ndiyo maana Kutoka 15:3 inamtaja kuwa "Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake". Alipowatoa Waisraeli Misri, hakuwapitisha njia fupi ya Wafilisti kwa sababu walikuwa bado hawajajifunza vita na wangeogopa kurudi Misri; aliwapitisha njia ya jangwani ili kuwanoa na kuwafundisha kupigana.

iii)          Kanuni Nne za Kupigana Vita:

a.    Usichokoze Mtu, Lakini Ukishambuliwa Piga Mpaka Apotee:

Usianze ugomvi na mtu yeyote bila sababu wala kumdhalilisha mtu; ishi maisha ya ki Mungu na usimame kwenye hatima yako pekee. Hata hivyo, ikiwa adui (iwe ni mchawi au nguvu ya giza) atakuchokoza na kuanzisha vita dhidi yako, usimhurumie, mpige kiroho mpaka apotee.

b.   Usipigane Kila Vita: Chagua vita vyako kwa akili. Usipoteze nguvu zako kupigana vita visivyokuhusu au visivyokuwa na uhusiano na hatima yako.

c.    Ukiamua Kupigana, Lazima Ushinde (Hakuna Kurudi Nyuma): Ukishaingia vitani, chaguo ni mawili tu: ama ushinde au ufie uwanja wa mapambano. Hii ni kwa sababu aibu ya kushindwa vita haibebeki, na gharama za kulipa fidia baada ya kushindwa ni kubwa mno.

d.   Jenerali Mzuri Hushinda Vita Bila Kupigana (Kuwahi Uwanja wa Vita): Hata mshindi wa vita vya kawaida hubaki na makovu na hasara (kama Urusi ilivyoshinda Vita vya Pili vya Dunia lakini ikapata hasara kubwa kuliko Ujerumani iliyoshindwa). Ndiyo maana jenerali hodari hufika uwanja wa mapambano kabla adui hajafika. Unapaswa kuwa na macho ya kiroho ya kusoma uwanja wa vita, kuona adui anaelekea wapi, na kumpiga mapema kabla hajakufikia.

7.   MAOMBI:

A.

"Kwa damu ya Yesu, ninatangaza vita katika ulimwengu wa roho. Ninavaa uweza kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kwa neno la Mungu ninabomoa madhabahu zote zilizoshikilia hatima yangu. Ninabomoa madhabahu ya ukoo, madhabahu ya familia, madhabahu ya kabila, na madhabahu ya taifa katika ulimwengu wa roho.

Ninachukua nyundo ya Bwana ivunjayo mawe vipande vipande, ninavunja madhabahu ya miungu migeni, madhabahu ya mizimu ya familia, madhabahu ya udhaifu, magonjwa, laana, kifo, aibu, madeni, shida ya ndoa, na umaskini. Ninashambulia na kusambaratisha kila madhabahu iliyo chini ya maji, chini ya miti, njia panda, makaburini, milimani, jangwani, angani, au iliyowekwa ndani ya mwili wangu. Ninabatilisha kila kafara ya wanyama, ndege, au binadamu iliyotolewa juu ya maisha yangu. Kwa damu ya Yesu, madhabahu hizo zivunjike, zisambaratike, na kuachia hatima yangu sasa!"

B.

"Kwa jina la Yesu Kristo, ninazuia jina langu lisitajwe tena kwenye madhabahu yoyote ya wachawi, waganga, au washirikina. Ninafuta na kuondoa jina langu, jina la mwenzi wangu, majina ya watoto wangu, jina la biashara yangu, kampuni yangu, na huduma yangu kutoka kwenye orodha zote za madhabahu za giza.

Mahali popote watakapokusanyika usiku au mchana kutaja jina langu kwa fitina au ubaya, ninaachia moto wa Roho Mtakatifu na damu ya Mwanakondoo. Watawanyike mbele yangu kwa njia saba na mipango yao yote iteketee. Ninaondoa tumbo langu la uzazi, mikono yangu, afya yangu, na hatima yangu iliyolazwa chini ya madhabahu zao. Kuanzia leo, jina langu limeondolewa kwenye vihenge vya wachawi kwa damu ya Yesu!"

C.

"Kwa jina la Yesu, ninaamuru kuanzia sasa jina langu litajwe mahali pa heshima. Litajwe kwa wafalme, litajwe kwenye makampuni, litajwe wizarani, litajwe kwenye fursa za kimataifa, na mahali popote palipo na funguo za hatima yangu, ili nitoke katika shimo la udhaifu na kwenda kumiliki ndoto yangu.

Maisha yangu yalianza kwenye udhaifu, lakini nitayamaliza nikiwa jabali. Ninakiri kuwa nimepata kutoka kwa Bwana, nimepata afya, nimepata amani, nimepata ndoa njema, nimepata watoto, nimepata kazi, nimepata mtaji, na nimepata ushindi. Ninatembea katika ulimwengu wa roho na kuchukua kila kilichoibiwa kutoka kwangu.

Hatima yangu inatimia mbele ya macho yangu katika jina la Yesu. Amen!"

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI





Post a Comment

0 Comments