google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIKAO VYA UHARIBIFU

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 08.11.2026
BISHOP DR. JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: VIKAO VYA UHARIBIFU 

Ulimwengu wa giza hufanya kazi kupitia maazimio ya kimkakati. Hakuna ajali katika roho; hakuna ugonjwa wa ghafla (kama vile magonjwa ya moyo au presha), laana, talaka, wala umaskini unaotokea hivi hivi tu kwa bahati mbaya duniani. Kila pigo au shida inayomkuta mwanadamu mwilini, huanza kwanza na kikao cha siri kilichokaa usiku na kupitisha agenda au azimio dhidi ya jina la mhusika.

Wachawi huwa hawalogi peke yao bali hufanya kazi kwa vikundi na vikao vya kikanda; mfano, kanda ya Machame, Sengerema, Geita, Mwananyamala, Bagamoyo, n.k. Ili jina la anayelogwa lifike kwenye kikao cha usiku akiwa amelala, lazima kuwe na mchawi wa karibu / wa ndani (ndugu, jirani, rafiki, au mfanyakazi mwenzake) anayepeleka faili kwenye kikao.

Wachawi ni makuhani wa shetani. Wachawi wakaapo kwenye vikao vyao, huona ni nani mwenye kitu; hawapotezi muda kushambulia mtu asiye na kitu au asiye na faida. Kiwango kikubwa cha mashambulizi na vita unavyokumbana navyo ni kiashiria cha ukubwa wa karama, vipaji, na kesho (hatima) yako kubwa. Wachawi wana uwezo wa kuona nyota inayong'aa kwenye ukoo, na ndio maana mara nyingi mtu mwenye matatizo makubwa kuliko wote kwenye familia ndiye mwenye hatima kubwa zaidi kiroho.

Wana wa Mungu pia tuwapo kanisani, tunakuwa tupo kwenye kikao cha kubatilisha yale yaliyoamuriwa na wachawi kwenye vikao vyao. Kwenye vikao vyetu kanisani, Yesu anahudhuria, Makerubi, Maserafi na serikali yote ya Mbinguni inakuwepo; lolote tunalosema kinyume na maadhimio ya wachawi linakuwa vilevile. Yaleyale ambayo wachawi wanajadili kwenye vikao vyao na kutushambulia kwa silaha zao, tunayageuza na kuwarudishia yawapate wao na vizazi vyao, na inakuwa kama tulivyotamka.

Mifano katika Biblia ya Adui Kugeuziwa Kibao:

1.   Danieli katika Tundu la Simba (Danieli 6:3-5, 24):

Huu ni mfano wa njama na fitina za kiofisi au kijamii zilizolenga kumwangamiza Danieli kwa kuliwa na simba wenye njaa. Hata hivyo, ulinzi wa Mungu ulimfungia Danieli vinywa vya simba, akatoka asubuhi akiwa na afya na uzima tele huku msimamo wake wa kumwabudu Yehova ukibaki imara. Kibao kiligeuka pale mfalme alipoamuru wale waliomshtaki watupwe wao wenyewe; simba waliwadaka hewani na kuwatafuna vipande vipande kabla hawajafika chini ya shimo.

Maadui hawakumshambulia Danieli kwa sababu alikuwa mzembe, bali kwa sababu mfalme alitaka kumkweza juu ya ufalme wote. Waliokaa kikao walijua hawataona kosa la kumuangusha isipokuwa kupitia sheria ya Mungu wake. Hili linafanana na vikao vya kichawi vinavyotafuta mbinu za siri (kichawi) ili kukamata hatima ya mtu aliyesimama vizuri mwilini. wale waliokaa kikao cha kumuua Danieli ndio waliotupwa wao wenyewe na familia zao kwenye lile shimo, ikiwa ni vita halisi ya kurudisha mapigo kwa adui.

2.   Hamani na Agenda dhidi ya Modekai (Esta 3:7-13 na Esta 7:10):

Madhabahu na vikao vya giza hupanga agenda za muda mrefu, kuweka tarehe maalum za uharibifu, na kutoa kafara. Hamani alipanga waraka wa kisheria kuangamiza Wayahudi wote tarehe 13 ya mwezi wa 12. Adui alijihakikishia ushindi kwa sababu mfalme alikuwa ameenda kuabudu mizimu kwa miezi mitatu.

Hata hivyo, mfungo wa siku tatu wa Modekai na Esta ulibadili anga la kiroho. Esta (anayeiwakilisha ishara ya Kanisa) aliingia kwa mfalme kinyume cha sheria, agenda ikabatilishwa, na Hamani akanyongwa kwenye msalaba uleule aliotengeneza kwa ajili ya Modekai.

Unapounganisha mifano hii, maombi yanahama kutoka kwenye kulia na kulalamika, na yanakuwa maombi ya kisheria ya kimamlaka. Unamwambia Mungu: "Kama ulivyoamuru simba wawale waliomshtaki Danieli, na kama ulivyoamuru Hamani anyongwe kwenye mti wake, ndivyo ninavyoamuru maazimio yote ya vikao vya kichawi yawajalie wao wenyewe!"

MAOMBI YA VITA

Katika jina la Yesu Kristo na kwa damu ya Mwanakondoo!

Ninageuza mikono yangu kuanzia sasa iwe mikono ya vita na makombora ya kiroho!

Ninatazama na kuvunja kila kikao cha siri kilichokaa usiku au mchana, chini ya maji, njia panda, makaburini, angani, au chini ya mibuyu kikijadili jina langu na hatima yangu!

Ninabatilisha na kuteketeza kila azimio na hukumu iliyopitishwa kichawi dhidi ya ndoa yangu, afya yangu, watoto wangu, na biashara yangu! Agenda zenu zote zimekuwa batili leo, kwa jina la Yesu!

Kama simba walivyowala waliomshtaki Danieli, ninaamuru lile shimo la mauti, umaskini, na mikosi mlilolichimba kwa ajili yangu, mtumbukie ninyi wenyewe na watoto wenu na familia zenu!

Kila mtego wa aibu na talaka mlioniandalia, ninaamuru uwanase ninyi wenyewe! Kifo walichokipanga, kiwarudie wao! Ajali waliyoipanga, iwarudie wao! Aibu waliyoipanga, iwarudie wao wenyewe! Katika Jina la Yesu!

Ninatuma moto wa Roho Mtakatifu kusambaratisha kila mtandao wa wachawi na majini waliotumwa kunifuatilia! Ewe Jini Makata, Jini Mahaba, Jini Maimuna, Jini wa Kimasai, na kila pepo wa bangi na madawa ya kulevya, kwa jina la Yesu Kristo, ninaamuru mporomoke na kuachia maisha yangu kuanzia sasa! Toka! Hama! Hautaniweza tena! Katika Jina la Yesu Kristo, AMEN!

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments