Na Mwandishi wetu.
Sehemu ya Vyombo vya Muziki vitakavyotumika siku ya Uzinduzi |
Kanisa la Glory of Christ
Tanzania maarufu kama Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi
Josephat Gwajima ambaye Mungu amempaka mafuta kufufua wafu na kurudisha
misukule (watu waliokufa katika mazingira tata) linatarajia kufanya uzinduzi wa
Mikutano yake ya Injili kesho Jumapili 3 Agosti 2014 kuanzia saa 3 asubuhi
katika viwanja vya Tanganyika Packers kuelekea nyanda za juu kusini na baadaye magharibi mpaka kaskazini mwa
Tanzania baada ya kufanya mikutano kama hiyo Mashariki mwa Tanzania ikiwa ni
pamoja na Arusha, Moshi, Tanga, Morogoro na Kilombero.
Itakumbukwa kuwa mwezi Septemba
mwaka 2013 Ufufuo na Uzima ilianza rasmi mikutano yake ya injili ambayo kwa
wastani zaidi ya watu milioni moja (1,000,000) walihudhuria mikutano hiyo
iliyofanyika Arusha, Moshi, Tanga, Morogoro na Kilombero mpaka mwezi Disemba
mwaka 2013.
Uzinduzi huo wa Mikutano ya
Injili kuelekea nyanda za Juu kusini inatarajiwa kuanza mkoani Iringa mwishoni
mwa mwezi Agosti, na kuelekea Njombe, Songea, Mbeya, Sumbawanga na Katavi.
Ratiba kamili ya Mikutano hii inatarajiwa kutolewa kesho katika uzinduzi huo.
Uzinduzi huu utapambwa na shamra
shamra za waimbaji maarufu wa nyimbo za Injili hapa nchini akiwemo Rose Mhando,
John Lisu, Bonny Mwaitege, Ambwene Mwasongwe, Jackson Benty, Christina Shusho,
Upendo Nkone na Flora Mbasha. Wengine ni pamoja na Munishi ambaye pia ameambatana
na Malebo, aliyewahi kumtaja katika kibao chake maarufu cha Malebo hataki
kuokoka.
Maelfu ya wakazi wa jiji la Dar
es Salaam wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huu. Watu mashughuli mbalimbali pia
wanatarajiwa kuwepo ikiwa ni pamoja na Mbunge wa jimbo la Kawe Mhe. Halima
Mdee.