Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima.
Kuna swali ambalo kama mtu uliyeokoka unatakiwa ujiulize kila siku, yaani “kama ikitokea leo umekufa una kitu gani cha kumwonyesha Mungu?” ukisoma Danieli 12:3 inaeleza kuwa, Wale Waliowaongoza wengi kutenda mema watang’aa kama nyota siku ya mwisho. Hawa ni watu wanaomtumikia Mungu, kumbe siku ya mwisho tutarudi mbinguni kila mtu atatoa hesabu yake. Lakini kama ulimtumikia Mungu duniani, utang’aa kama nyota.
MAMBO AMBAYO UTAYAPATA KWA KUMTUMIKIA MUNGU:
Pamoja na hayo hapa duniani, kuna
vitu havipatikani kwa kuomba lakini vinapatikana kwa kumtumikia Mungu. Kuna
mambo ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Tuangalie mambo 11
ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Kutoka 23:25
- Atabariki chakula chako:- hapa hata kama utakula chakula chenye sumu, hauwezi kudhurika kwasababu unamtumikia Mungu.
- Atabariki maji yako:- vilevile atabariki maji yako, yaani hayatakudhuru.
- Nitakuondolea magonjwa kati yako:- ukimtumikia Mungu, huwezi kuingia katika magonjwa yaani kama ulikuwa unaumwa Mungu atakuponya kwa vile unamtumikia Mungu.
- Hautakuwa mwenye kuharibu mimba:- Kuharibu mimba maana yake unaanza kitu, lakini kabla hakijafanikiwa kinaharibika. Inaweza ikawa mimba au hata kampuni.
- Kutokuwa tasa:- kama unamtumikia Mungu hata kama una miaka mingi unaweza kuzaa. Alikuwepo Sara ambaye alizaa akiwa na miaka 90 pamoja yakuwa umri ulikuwa umeendelea sana.
- Mungu atatimiza hesabu za siku zako:- unapomtumikia Mungu, atakupa miaka mingi ya kumtumikia Mungu, yaani kwasababu unafanya kazi yake duniani Mungu anakuongezea miaka ili umtumikie vizuri. Maana hata Mfalme Hezekia alipoumwa alimkumbusha Mungu jinsi alivyomtumikia Mungu, na Mungu akamwongezea miaka kumi na tano asingeweza kupata kwa maombi tu bali ni kwa kumtumikia Mungu.
- Mungu atatuma utiisho wake ukutangulie:- yaani huu ni uungu wa Mungu juu ya maisha ya mtu.
- Mungu atawafadhaisha wale watakaokufikiria.
- Mungu atawafanya adui zako wakuonyeshe maungo yao.
- Mungu atatuma mavu mbele ya adui zako wote.
- Mungu atawafukuza aduiazako wote.
Katika biblia watu waliomtumikia
Mungu, Mungu aliwaheshimu. Mwanzo 41:41, Yusufu alipata nafasi ya
kuwa waziri mkuu kwenye nchi ya ugeni. Hii ni kwasababu Yusufu alimtumikia
Mungu, akapewa kuheshimiwa na Mfalme wa Misri. Kila anayemtumikia Mungu, Mungu
humueshimu mtu huyo.
UWEZEKANO WA KUMTUMIKIA MUNGU UKIWA NA KAZI YAKO:
Unaweza ukamtumikia Mungu huku ukiwa na nafasi katika uongozi au unafanya kazi nyingine yoyote. Alianza kuwa kama mbunge ingekuwa siku zetu lakini pamoja na huo uongozi aliweza kumtumikia Mungu. Danieli 2:48; kwa habari ya Danieli tunagundua kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu huku ukiendelea na kazi yake. Kumbe kumtumikia Mungu Danieli 5:25-29; unaweza kumtumikia Mungu katika kiwango cha juu na bado ukafanya kazi zako za kawaida kama Danieli. Danieli 6:48:- hata kipindi cha Mfalme Koreshi, Danieli aliendelea kustawi, kwasababu alimtumikia Mungu.
Danieli 2:49 Hata Shadraka, Meshaki na Abednego pamoja na kuitumikia
nchi, waliendelea kufanya kazi ya BWANA. Unaweza ukajiuliza kuwa ninawezaje
kumtumikia Mungu huku ninabanwa na kazi, lakini kumbe Biblia inatupa ushahidi
kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu. Na ndio maana hata Joshua ingawa
alikuwa anamtumikia Mungu na wakati huohuo akiwa mpelelezi, Hesabu 13:6; Joshua alikuwa mpelelezi
na katika kazi yake ya upelelezi aliifanya vizuri na kuleta ripoti nzuri,
kinyume cha wapelelezi wengine ambao walileta ripoti mbaya Hesabu 14:19.
Kwenye Biblia hata polisi walimtumikia Mungu. Esta 3:1-6 Modekai alikuwa anafanya kazi katika nyumba ya mfalme yaani alikuwa anakaa kwenye lango la mfalme. Kumbe kuna uwezekano wa kuwa polisi na huku unamtumikia Mungu. Uwezekano huo upo.
Pia katika biblia; kulikuwa na
mawakili waliomtumikia BWANA. Luka 8:3
“Yohana mkewe Kuza wakili wa Herode” yaani katika maisha ya leo huyu angeitwa
mwanasheria mkuu, pamoja na kufanya kazi ya sheria na bado ukamtumikia BWANA.
Kuwa mwanasheria hakumzuii mtu kumtumikia BWANA.
Matendo ya Mitume 17:4 “na wanawake wenye vyeo si wachache.” Neno
hili linaonyesha kuwa hawakuwa wachache, kumbe unaweza kumtumikia BWANA na huku
ukiwa na cheo chako kilekile. Yaani, unafanyakazi ya kumtumikia kwa uaminifu na
huku unafanyakazi kwa uaminifu pia.
Matendo ya Mitume 16:14-15 Alikuwepo mwanamke huyu aliyeitwa Lidia
ambaye alikuwa akiuza nguo za zambarau; kumbe unaweza kumtumikia Mungu na huku
ukiwa mfanyabiashara. Siku ukiwa mbinguni huwezi kuonyesha biashara ulizofanya
duniani, bali utamwonyesha kazi uliyofanya katika kumtumikia Mungu. Kuwa mfanya
biashara sio sababu ya kukufanya ushindwe kumtumikia Mungu.
Yeremia 36:32; Baruku alikuwa mwandishi wa habari na huku
alimtumikia Mungu yaani ndiye aliyekuwa anaandika mambo ambayo Yeremia alikuwa
anayanena. Ilifikia kipindi hadi watu wanashangaa jinsi alivyokuwa anaandika. Yeremia 16:17; Yeremia 36:27; Katika
biblia waandishi wa habari walikuwepo pia, Yeremia
36:10, kumbe unaweza kuwa mwandishi wa habari, huku unamtumikia Mungu.
Kutoka 1:38 kwenye biblia
walikuwepo wakunga ; waliokuwa wakimtumikia BWANA; kumbe unaweza kuwa
mzalishaji lakini unamtumika Mungu. Hata kama unafanya kazi za hospitali na
bado ukaweza kumtumikia Mungu, Biblia inasema Mungu aliwatendea mema kwasababu
ya kazi yao ya kuzalisha watoto kwa uaminifu.
Matendo ya Mitume 18:1-4. Paulo pamoja na nyaraka zake zote na
kumtumikia Mungu lakini bado alikuwa anashona mahema kama kazi aliyofanya muda
wa ziada. Kwahiyo kumbe, waweza kufanya kazi yako huku ukimtumikia Mungu kwa
hiyo. Na ndio maana katika Biblia kulikuwa na msomi aliyeitwa Apolo, Matendo ya mitume 18:24-28. Kumbe
pamoja na kusoma kwako waweza kumtumikia Mungu pia. Matendo ya mitume 26:24-25; kumbe hata Paulo alikuwa amesoma sana.
Na ndio maana Paulo ndiye aliyeandika asilimia kubwa ya vitabu vya Biblia
pamoja na roho mtakatifu pia alikuwa amesoma na alikuwa na kazi anayofanya.
FANYA UAMUZI SAHIHI KUMTUMIKIA MUNGU:
Baada ya Kujifunza mambo hayo ni
uamuzi wako kuchagua unataka kumtumikia nani, ukichagua kumtumikia Yesu unakuwa
umechagua hizi Baraka zote 11 za kumtumikia Mungu. Yoshua alisema “chagueni
hivi lleo mtakayemtumikia, lakini mimi na nyumba yangu nitamtumikia Mungu.” amua
kumtumikia Mungu ili uzishiriki baraka zote zilizotajwa.....
Mungu akubariki katika Jina la
Yesu Kristo...
1 Comments
Barikiwa sana mtumishi kwani sisi sote tutadhihirishwa (KUONEKANA WAZI)mbele ya kiti cha hukumu kila mtu apokee ijara (UJIRA AU MALIPO) ya mambo aliyoyatenda kwamba ni mema au mabaya,kwa somo hili nadhani kila mtu ajisike deni la kuwaongoza wengi kutenda mema
ReplyDelete