google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUZIBOMOA MADHABAHU ZA KICHAWI.

 UFUFUO NA UZIMA UBUNGO CATHEDRAL.
IBADA YA JUMAPILI 28th MAY, 2023.
ASKOFU BARAKA THOMAS TEGGGE.
SOMO: KUZIBOMOA MADHABAHU ZA KICHAWI.

“Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake”. Waamuzi 6:25-32

Huyu kijana amezaliwa kwenye madhabahu. Yeye hana madhabahu ila baba yake ana madhabahu, yeye sio mchawi ila baba yake ni mchawi, MUNGU anamtokea anamwambia wewe unaweze kuwapiga Wamidiani, akamwambia nenda na uwezo wako huo ukawaokoe Israeli, hata wewe leo unaweza kuolewa na ukaa kwenye ndoa, unaweza kusoma na ukafaulu ila una madhabahu inakuzuia. Sisi ni watu pekee wenye mamlaka ya kuharibu, kubomoa, kuangamiza madhabahu ya kichawi, ukiona vitu havifanyiki ujue mwenye mamlaka hajafanya kitu. Maandiko yanasema Petro alipokuwa anaomba Roho ikaenda juu ya Kornelio, kanisani hujaja kusali tu au kufanya mambo ya dini ila umekuja mahali ilipo madhababu ya Mungu ili upokee kutoka kwa Bwana, ukiona kanisa hakuna udhihirisho wa Mungu basi fahamu hapo ni kanisa la dini kama yalivyo mengine, kwahiyo ukija kanisani kaa mkao wakupokea kutoka kwa Mungu. Kanisani hatutoi pesa ila tunakupa neno lenye uwezo wa kukufanikisha upate pesa, Paulo alipokuwa anahubiri akamuona mtu mwenye Imani ya kupokea ila anahitaji neno, unaweza kuwa na imani ya kuanza  kusoma, kuanza biashara, ila hujatamkiwa neno, maana imani huja kwa kusikia neno la Mungu.

Hana akaenda kanisa maandiko yanasema akamimina moyo kwa Bwana ila hakupata, mpaka kuhani akasema mama Mungu akupe haja ya moyo wako na mimi nasema Bwana akupe haja ya moyo wako ili watu wajue Mungu alikupatia, unapoenda kanisani usikae kwa hasara kaa mkao wakupokea kutoka kwa Bwana, maana Bwana ana neno la biashara, kazi, masomo ukiamini utapokea kaa kama mtu aliyekuja nyumba mwa Bwana kupokea kutoka madhabahuni. Mungu akijua unamsikiliza basi anaongea na akijua husikii hatasema. Eli alimwambia Samweli akisikia anaitwa aseme nena Bwana mtumishi wako anasikiliza. Ukisikia neno la Mungu litakutoa katika maharibifu yako lakini lazima neno litumwe, lazima pawe na kinywa cha mtu ili neno litumwe. Na leo limekuja kwa kinywa cha Pastor Baraka, amelituma neno lake ili kukuokoa  katika maharibifu, madeni ,shida ya ndoa na leo utatoka.  Kanisani hakuna pesa ila kuna neno.” Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu”. Yohana 1:1-2

Kuna mambo hayawezi kufanyika kwenye ndoa yako, biashara mpaka neno litumwe, asubuhi ya leo Mungu anatuma neno maana kuna mambo anataka yafanyike kwako. Likija neno ndani yake kuna uzima na huo uzima ni nuru hutoa giza. Mwanamke alifiwa na mumeo na akaachwa na madeni na mdeni akaja akamwambia huwezi nilipa ila nitachukua watoto wako, mwanamke akaenda kwa Elisha, akamwambia mkumbuke mtumishi wako alikuwa anafanya kazi kanisani, maana Mungu sio dhalimu, unaweza usiwepo na Mungu akashughulikia mambo yako siku ambayo hautakuwepo hanisani. Ukifanya kazi kwa Bwana mwanao, mkeo na mumeo watakuwa salama. Mungu akijua una muamini atabariki kizazi chako cha kwanza mpaka cha nne. Watu wote walikuwa wana kimbilia Misri kutafuta chakula ila Mungu alimwambia Isaka usiondoke kaa hapa maana nitakubariki maana baba yako alikuwa mtii, Isaka akalima kipimo kimoja akavuna vipimo mia 100. Kwasababu baba yake alikuwa mtii kwa Mungu akambariki Isaka. Naamini wanangu hawatakuwa omba omba , wala kuzaa nje ya ndoa ,naamini kwasababu imendikwa, Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee sijaona mwenye haki wa Bwana akiaachwa hata watoto wake kuwa omba omba.

Ukiwa chini ya baba kuna amani, mimi nina amani maana niko chini ya mbawa za baba. Nawewe tulia kwenye mbawa. Mungu anasema Israel mara ngapi nilitaka niwakusanye nikuweke chini ya mbawa zangu, angalia mmeachwa na nyumba yenu imebaki ukiwa. Mungu anapotaka kukusaidia anatuma watu kwao sisi kwetu ametumwa baba, ana mbawa zakutosha kwa wanae wote, huko nje kuna mbwa, kuna wachawi, kaa chini ya mbawa utakuwa salama, mwanamke anasema baba yangu mtumishi wako hata sisi ni watumishi wa baba yetu na tunafuraha kuwa watumishi wake maana ndio kinga yake hii ndio imefanya hatukuchanjwa kwasababu ya mbawa zake tukawa salama. Usalama wetu nikukaa mahali Mungu amependa tukae ametufunika kwa mbawa zake, chini ya mbawa zake tumepata pa kujificha. Mwizi akija kwako anaanza kumkamata baba kwanza, hata sisi shetani hana shida ya kutupiga sisi, ila baba. Hapa baba ni mchungaji wetu na sisi ni kondoo wake. Mimi ilikuwa nife 22 june 2005 saa tano usiku nilikuwa naumwa ila nikapona kwa maombi ya baba, hata juzi nilikuwa natoka tanga, nilikuwa na pastor Kijana anayependa kuovertake, alivyoovertake alikutana na magari marefu matatu, ila akajitia nguvu, mimi kitu pekee niliongea ni Aaa, ile gari nyingine ilikuja ikapitia kioo cha gari na tairi ya gari, tulipona kwasababu mbawa zake zimetufunika. Kukaa chini ya mbawa ni salama, ni amani kabisa.  Kwanini huyu mwanamke alienda kwa Elisha ni kwasababu anajua alikuwa mtumishi wake, Elisha akamuuliza nyumbani kuna nini akajibu na kumuambia nenda kaazime kwa Jirani chombo, maana ukianza kukumimina mafuta hayatakoma, akamimina vyombo vyakutosha, akarudi kwa Elisha akamwambia neno kauze mafuta uweze kulipa deni.

Watu walipoamka asubuhi kwenda kupata majibu katika madhabahu ya Baali wakakuta tayari imebomolewa, wakaanza kuulizana ni nani aliyetenda haya. Wakaambiwa ni Gideoni mwana wa Yoashi ndio ametenda haya. Wakasema Gidion aje auwawe. Yoashi akasema mtamtea Baali au mtamuacha ajitete mwenyewe maana yeye ni mungu.

Madhabahu ni nini? Ni daraja linalounganisha kutoka ulimwengu wa roho kuja ulimwenguwa mwili au kutoka ulimwengu wa mwili kwenda ulimwengu wa roho. Kuna mambo yanaendelea kwenye ulimwengu wa roho ila hayaathari ulimwengu wa mwili au kuna mambo mengine yanaendelea ulimwengu wa mwili ila hayaathiri na ulimwengu wa roho ni kwa kuwa hapana mahusiano kati ya ulimwengu wa Roho na mwili mpaka liwekwe daraja.

Madhabahu ina mambo makuu matatu. Moja, Mungu wa madhabahu, Pili, kuhani wa mdhabahu. Kuhani  ni mtu aliyepewa ruhusa kufanya kazi kwa niaba ya Mungu, anafanya kazi kuruhusu viumbe wa rohoni kuja kwenye ulimwengu wa mwili na kutenda yale aliyoagizwa. Tatu ni kafara zinazowekwa kwenye madhabau, kuhani anaruhusu viumbe wa rohoni kuja kuchukua kafara na kutenda mambo kwenye ulimwengu wa mwili, Pia kuna watu wa madhababu inayowahusu, kuna watu madhababhu imejengwa kwa ajili yao inaweza kuwa imejengwa kukuzuia usiolewe, usizae au usipate kazi.

Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya”. Mwanzo 8: 20-21.

Nuhu ndiye alikuwa kuhani wa madhababu na yeye akatoa kondoo na kuwachinjwa alipoanza kufanya mambo hayo Mungu akajitokeza na kuzungumza naye, alipojenga madhabahu bado Mungu hakuongea mpaka alipotoka kafara, Mungu akaongea akasema sitailaani nchi tena kwa ajili ya wanadamu. Shetani huwa anakopi vitu, kuna madhabahu inajengwa kwa ajili ya kukulaana au mtu kushindwa. Mungu alisema hata ilaani nchi tena akafanya agano na Nuhu akaweka upinde wa mvua, ukiona upinde wa mvua fahamu ilitakiwa kunywesha mvua ya gharika na asingepona mtu, ukiona hivyo fahamu hiyo sehemu kuna dhambi nyingi sana. Nuhu ajenga Safina akapona gharika na akajenga madhababu katoa sadaka Mungu akaongea baada ya kusikia harufu

Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea. Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana”. Mwanzo 12:7-8

Ibrahmu akajenga madhabahu pale Betheli, miaka mingi ikapita  akazaa mtoto (Isaka) akiwa na miaka 100. Mtoto akafika miaka 60 na kuzaa mtoto wako anaitwa Yakobo, Yakobo alipofikisha miaka 40 siku moja akasafiri na kufika Betheli, akalala sehemu ambayo babu yake alijenga madhabahu, Mungu akamkumbuka. Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua”. Mwanzo 28:10-16

Hata wewe babu yako alijenga madhabahu, ile madhabahu miungu yake ni ya familia mzima, ndio maana Gideon hana madhabahu ila ya babu na baba yake ikawa ina muingilia kwenye ufanisi wake wakazi, ndio maana Mungu akaibomoa, pasingekuwa na haja ya kubomoa hiyo madhabahu kama isingekuwa na athari na Gideoni, ila ilikuwa ina muathiri ufanisi wake wakuwaza alikuwa anajiona mdogo, mdhaifu Mungu akaiboma hiyo madhabahu.

Leo lazima madhabahu za kwenu zibomolewe maana wewe ni shujaa, unakuta mtu anajitenga na wenzake, anaona wanapesa wamesoma ila ni madhabahu za kwao ndio zinamfanya hivyo. Bwana akamwambia Gideon wewe ni shujaa nenda kabomoe madhabahu ya baba yako. Mungu akamwambia Yakobo mimi ni Mungu wa baba yako nitakwenda na wewe. Mtu anajitenga hata wakiitwa wanawake wenzie kanisani haji maana yeye hana gari. Yakobo miaka 21alikaa kwa Laban, akiwa anatoka kwa Laban, Laban akiwa anamuwazia Yakobo kumfanyia jambo, Mungu wa madhabahu ya babu yake Yakobo akaongea na Labani. Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia, akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi. Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi. Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu. Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari “. Mwanzo 31: 22-29

Mungu aliona jambo Laban alipanga kumfanyia Yakobo, akamwonya unakuta mtu anapata wazo lakutaka kukupatia mtaji, au kijana anataka kuchumbia binti ghafla  ile miungu wa babu yako  inamzuia kwakumtoke kwenye ndoto na akaiendelea kung`ang`ania basi atashangaa anakoswa koswa na ajali, mabalaa mengi, kuna madhabahu zimewekwa ili kuzuia mabinti wa familia yake wasiolewe. Kuna mwingine akiwa kanisani ana muomba Mungu awape mume ila akija mwanamme anaanza kumchambua mara anasema huyu mwanaume sura hii hapana, mara mweusi sana ila ukifanikiwa kumuoa utashangaa anasema kumbe uko sawa tu ndio maana leo tutaomba kubomoa madhabahu zao.

Namkumbuka binti mmoja alichumbiwa na kijana mmoja amenyooka, binti akanijia akasema ni kweli kijana ni mcha Mungu ila hatuendani, ni kamuuliza kwanini akasema yaani nampigia simu nusu saa nzima anakuombea yaani huyu kijana yuko kiroho sana, hapana hanifai, asubuhi anakuamsha naandiko ila yeye anataka maneno mazuri yakimahusano, akamkataa kijana. Siku moja binti, alipata mchumba mwingine amepindana hawezi kunyooka kabisa. Madhabahu ina nguvu kuachia viumbe wa rohoni kufanyia kazi mambo yaliyopo kwenye madhabahu. Madhabahu ikijengwa inajengwa ikiwa na dhumuni Fulani, na kafara hufanyikia hapo na Mungu anakuja hapo, kama sio Mungu wa Israeli ni mungu wa dunia hii na kuhani anaongea maneno sawasawa na  kafara iliyotolewa. “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu ikimbieni ibada ya sanamu. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani”1Kor 10:14,18-20

Paulo amewahubiria wameokoka akawaambia ikimbieni miungu, wa Moabu waliwaalika wana waisraeli kwenye ibada zao. Kuna baadhi watu wanafanya sherehe zao na kuchinja wanakuambia wewe una Mungu wako njoo tu ila hiyo ni ibada wanafanya na unajiunganisha na madhabahu yao bila kufahamu. Nguvu ya madhabahu huwafanya watu wengi kuyakataa mambo muhimu kwao wanapokuwa nayo au wanapotakiwa kuwa nayo ila wakiyakosa hujilaumu sana. Nguvu ya rohoni ya madhabahu ndiyo inayo waongoza, mashetani wa madhabahu wanaamua nini kifanyike kwenye familia. Mtu yeyote anayependa mambo ya mila ni hatari sana, mambo ya mila ni mambo ya madhabahu nani hatari sana na kufuata mambo ya mila ni kuungamanishwa na mashetani. Ni lazima ndugu wajue umeokoka na mambo ya mila haya kuhusu na wewe ni mtu wa Mungu na mambo ya mila hufanyagi na hayakuhusu. Wokovu ni swala la rohoni na wewe umechagua upande wa NURU kwa hiyo mambo yoyote yasiyo ya nuruni na kiroho la Kimungu halikuhusu. Madhabahu hujengwa kwa sababu ya jambo Fulani au mtu Fulani. Madhabahu hujengwa na maneno hunenwa kwa ajili ya mtu au jambo Fulani. Hulogwi nje ya madhabahu, kila aliyelogwa ni nguvu na matokeo ya madhabahu za giza. Watu wengi wamefungwa wasiofanikiwe, wasiolewe, wasizae n.k na madhabahu za giza. Mambo yote huanzia na madhabahu na wala si elimu, mtaji wala connection. Watu hawaanzi siasa kwa kuwa ni waongeaji bali huzitegemea madhabahu za giza na hawazitegemei connections, elimu wala fedha zao. Watu wengi hasa wa kiroho waliookoka wanadharau sana mambo ya rohoni na kuambatana na mambo ya mwilini yaani wakifanikiwa tu kidogo wanasahau mambo ya Mungu na kusema wako busy. Madhabahu za giza ni lazima zibomolewe na zisipo shughulikiwa mambo mabaya hutokea. Kumbuka madhabahu zote hujengwa kwa ajili ya kusudi Fulani.

Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki”. Hesabu 22’. 1-7.

Soma Hesabu 23:1-26. Siyo kila anayeita Mungu ana maanisha ni Mungu Yehovah.

Tofauti ya Agano la Kale na Jipya ni kwamba katika Agano la Kale kuna baadhi ya mambo anayafanya kwa sababu walikua hawajapewa mamlaka lakini katika Agano Jipya Mungu haiingilii kati kwa sababu tumepewa mamlaka. Unabii unao uamini ndiyo utakaoupata. Amini neno la Mungu ndilo kila kitu katika maisha. Kila kitu kutoka kwa Mungu huanza kwanza na kuamini ndipo na mengine hufuata. Maneno wanayoyaongea wachawi siyo yakwao bali ni mashetani wana wavuvia ili waseme nayo hutokea kama hayatazuiliwa na mtu wa rohoni. Kila ubaya uliopangwa na shetani kupitia madhabahu, madhabahu hizo zikibomolewa na mtu wa Mungu hubatilisha. Mambo ya rohoni yako hivi anaye yafanya ndiye anashinda, kila upande wa nuru au giza una kanuni zake na taratibu zake. Kumbuka kuolewa ni kuwa mtumwa. Ukilogwa mambo ambayo ni staiki yako unayakataa. Unaoongea kurogwa ukumbuke madhabahu , kurogwa ni maneno yaliyoongewa kwenye madhabahu. Agano Jipya ni wewe unaongea maneno ili malaika wayatendee kazi.” Hata walipokuja matuoni kwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga-piga Wamoabi hata kwao. Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe”. 2 Wafalme 3´.24-27. Mtu aliyelogwa huwa anapambana kupata kitu Fulani anapokaribia kupata huwa anaighairi na kinachosababisha  hayo kutokea ni kafara iliyotolewa. Kwa kuna madhabahu ya mapepo na kwetu kuna madhabahu ya malaika wa Bwana.

Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi. Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika. Na huyo malaika akakitwaa kile chetezo, akakijaza moto wa madhabahu, akautupa juu ya nchi, kukawa radi na sauti na umeme na tetemeko la nchi”. Ufunuo wa Yohana 8:3-5

Sisi tuna nguvu kuliko wachawi maana na kwa neno la ushuhuda tutawashinda, damu tayari tunayo kwahiyo neno linatakiwa, Mkristo anapozungmza anakuwa  anampa malaika kichanganyio cha maombi. Unaweza kuniuliza nitajuaje kuna madhabahu , nakuambia ipo na kuijua angalia maisha unayoishi una miaka 40 bado hujaolewa, uliuza maji ukafilisika kila ukichumbiwa unaachika na unaachwa kwa sababu isiyo ya msingi maandiko yanasema akatoka nabii kule Yuda akasema eeh madhabahu utapasuka madhabahu ili semeshwa ikapasuka neno la Bwana ni kama nyundo ivunjayo vipande vipande, vunja madhabahu zote zilizokushikilia zinazotaka uwe na mfanano na nduugu zako wa kijijini, usisonge mbele zivunje zote madhabahu. Kama babu, baba wote wamezaa nje ya ndoa na wewe umezaa nje ya ndoa hiyo ni madhababhu ivunje. Mkono wa Bwana una nguvu kuna malaika anakusubiria uongee ana chetezo na uvumba anakusubiria uongee maneno, nayeye atende jambo. AMINA.

Post a Comment

0 Comments