UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 21.12.2025
ASKOFU DKT GESHOM
MWAKILA
SOMO: NGUVU YA
MSALABA SEHEMU YA PILI
![]() |
Sehemu
ya kwanza tulijifunza kwamba msalaba ni nguvu ya wokovu na kaburi lililo wazi inamaanisha
kuwa kanisa limeshinda mauti. Nguvu ya msalaba inabeba vitu vifuatavyo: Inabeba
msamaha, Inakupa uhakika kwenye mambo ya maisha yako, Inatupa kukubalika.
Kwa
kila kazi ambayo mtu anafanya, upo mshahara wa kazi hiyo. Ukifanya kazi ya Mungu
sawasawa na alivyokupa, kuna mshahara wake ambao anakupatia. Vivyo hivyo ukifanya kazi ya Mungu kwa uzembe na ukiwa
unajua kuwa hufanyi sawasawa na mapenzi ya Mungu, pia utalipwa mshahara sawa
sawa na kazi yako.
“Tazama, naja upesi, na ujira wangu u
pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” Ufunuo 22:12
Kila
mtu anaefanya kazi kwa mwajiri fulani, basi mwajiri wake ndio mwenye dhamana ya
kumlipa mtu huyo mshahara. Ukifanya kazi ya Shetani atakaye kulipa ni Shetani,
na ukifanya kazi ya Mungu utalipwa na Mungu. Neno la Mungu linaweka wazi kuwa,
msahara wa dhambi ni mauti. Ila kwa kupitia kupigwa kwa Yesu msalabani, alichukua
dhambi ya ulimwengu. Yesu alichukua dhambi zako ili wewe uweze kukubalika kwa
Mungu. Kwa nguvu ya msalaba wa Yesu inakupa kukubalika na kupatana tena na Mungu.
5.MSALABA
WA YESU UNAKUPA UPATANISHO
Kwa
nguvu ya msalaba wa Yesu, inakupa kupatana na Mungu pamoja na watu wengine. Kwa
nguvu ya upatanisho iliyo katika msalaba wa Yesu, inakufanya mpatane tena na
kuwa na umoja na mtu ambaye mlikuwa hampatani. Msalaba wa Yesu ni nguvu ya
upatanisho baina ya watu. Msalaba wa yesu unaleta neema ya upatanisho baina ya
watu.
“Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama
mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi
Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule
mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua
nyumbani kwake.” Yohana 19:25-27
Mungu
ni mmoja na mpatanishi ni mmoja ambaye ni Yesu Kristo. Yeye ambaye ametoa uhai
wake ili kuupatanisha ulimwengu wote na Mungu, na upatanisho wa mtu na mtu. Yesu
ni mpatanishi kati ya mtu na Mungu.
“'Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya
Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;” 1Timotheo 2:5
6.
MSALABA WA YESU UNAKOMESHA MATESO
“Basi
Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa,
akaisalimu roho yake.” Yohana 19:30
Yesu
alidhalilishwa na kuaibika mbele ya watu. Ila hayo aliyaruhusu ili watu walio
mpokea wasiaibishwe tena bali wapte heshima. Yesu ndie mtu ambaye ameaibishwa
kwa asilimia zote, lakini ndiye ambaye Mungu akamwinua juu sana kuliko vitu
vyote. Ila kuinulia kulikuja baada ya kunyenyekea na kustahimili aibu.
“ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU
KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Wafilipi 2:10-11
Unyenyekevu
unaleta kuinuliwa. Unyenyekevu unaleta kibali kwa Mungu, naye Mungu atakuinua
na jina lako litakuzwa. Yesu alikuwa mnyenyekevu wa kufanya mapenzi ya Mungu na
Mungu akampa jina lipitalo majina yote.
“jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika
Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari
za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” Matendo 10:28
Kupitia msalaba wa Yesu Kristo kuna nguvu ya kufufua wafu kutoka kwenye makaburi, na pazia la hekalu likapasuka.
7.MSALABA
WA YESU UNAFUTA HATI ZA MASHITAKA
Kila
mtu alieokoka ni raia wa Mbinguni. Maisha ya kiroho yana mshtaki ambaye ni kiumbe
wa rohoni katika ufalme wa giza. Kazi yake ni kumshtaki raia wa mbinguni pale anapofanya
kosa. Kuna sheria ya mbinguni inayomruhusu mshtakiwa amshitaki raia wa mbinguni
na anapeleka mbele za Bwana.
“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa
yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha
kutusamehe makosa yote;” Wakolosai 2:13
Lakini
kupitia nguvu ya msalaba wa Yesu, mashitaka yote yalifutwa. Kupitia msalaba wa
Yesu, hati ya mashitaka iliondolewa na hukumu nayo ikaondoka. Pasipo mashitaka
hakuna hukumu. Yesu alipokuwa anasulubiwa, alifuta mashitaka ya ulimwengu ili
watu watakao mpokea yeye wasishtakiwe.
Mshtaka
hayo yanaondolewa kwa watu ambao wamemkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha
yao. Mtu anapo mkiri Yesu, anapokea nguvu kutoka kwenye msalaba ambayo inaondoa
hukumu na adhabu ya mashitaka. Pale usipo mwamini Yesu, unakuwa na vazi ambalo
linamaana ya kuhukumiwa. Kuna mambo yanampata mtu na yanamtesa ni kwasababu ya kutomwamini
Yesu, na kutopata ile nguvu ya msalaba yenye kufuta mashitaka.
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa
milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu,
bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi;
asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa
Mungu.”
Yohana 3:16-19


0 Comments