UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 07.12.2025
ASKOFU DKT GESHOM MWAKILA
SOMO:
NGUVU YA MSALABA
![]() |
Zamani mtu alikuwa akifanya makosa fulani, anahukumiwa hukumu ya kifo. Kifo hicho kinaweza kuwa kwa njia tofauti tofauti kama vile kuchomwa kwenye tanuru la moto, kupigwa mawe, ama kwa njia ya kusulubiwa msalabani. Yesu alihukumiwa kifo kwa njia ya msalaba. Kupitia mauti ya Yesu msalabani, na damu yake iliyomwagika imemkomboa mtu kutoka kwenye hukumu ya mauti na laana.
“Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye
kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake
aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti
cha enzi cha Mungu.” Waebrania 12:12
Na
ule uzima wa milele ni huu, kumjua Mungu wa kweli na Yesu Kristo mwanae. Kwa
kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, ndipo damu yake Yesu
iliyomwagika msalabani inakukomboa. Nawe unakombolewa kutoka kwenye mauti na
kuingia katika uzima wa milele.
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa
pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” Yohana 17:3
Kuna
mambo mengine yanampata mtu kwa sababu ya kutokusamehe. Nguvu ya msalaba
inakupatia nguvu ya kusamehe, kama vile Yesu anavyowasamehe watu makosa yao yote.
Ipo nguvu ya msalaba yenye kumfanya mtu kuwa kiumbe kipya, na kila mwana wa
Mungu anayo amri ya kusamehe dhambi hapa duniani.
“Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo
walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande
wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.
Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.” Luka 23:33-34
Kuweza
kupata uhakika wa maisha yako ni kuwa na imani kufuata kile Mungu anakwambia kupitia
neno lake. Kwa kufanya hivyo kwa njia ya msalaba ya Yesu, inakupa uhakika kwa
asilimia mia wa kufanikiwa, kustawi, kuponywa, kumiliki na mambo mengine
yanayohusu maisha yako.
“Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa
maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa
thawabu wale wamtafutao.” Waibrania 11:6
Dhambi
humfanya mtu asiweze kukubalika na Mungu, lakini msalaba wa Yesu unatupa kukubalika
mbele za Mungu. Msalabani Yesu alibeba dhambi za ulimwengu, alifanyika laana ili
wewe ukubalike mbele za Mungu na wanadamu. Kwa njia ya msalaba inamfanya mtu
atoke kwenye kukataliwa hadi kukubalika.
“lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu
wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia” Isaya
59:2
Kuna
nguvu kwenye msalaba wa Yesu inayokata kiu ya mambo mabaya. Mambo hayo mabaya ni
dhambi, kama vile ulevi, uzinzi, chuki, na hofu. Lakini pia kwa msalaba wa
Yesu, ipo nguvu inayoweza kukuwekea kiu na shauku ya kufanya mapenzi ya Mungu
kama vile kuomba, kufunga, kumsifu, kufungua watu, na kuhubiri injili. Kwa kupitia
msalaba wa Yesu, unapata kiu ya kutamfuta Mungu.
“Kwa sababu
neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu
ya Mungu.” 1 wakorintho 1:18


0 Comments