UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI: 05.07.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: AMESIMAMA KUWA KIKWAZO CHA HATIMA YAKO
![]() |
Alichoandikiwa mmoja siyo lazima mwingine aandikiwe hicho hicho. Huwezi kuishi hatima ya mtu mwingine. Yule anayeshambulia cha mwenzake, hawezi kukifanya kuwa chake. Unaanzaje na unamalizaje, kipo kwenye kitabu cha Mungu (Zaburi 139:16). Siku za mtu hazianzi alipozaliwa; tarehe ya kuzaliwa ni kudhihirika katika mwili, ila mtu alishuka ile siku mimba ilipotunga.
Huanza hatima / kusudi halafu anafuata mtu wa kutimiza hilo kusudi, hivyo hatima ya mtu mbele za Mungu ilishaisha kabla mtu hajazaliwa. Kwa mantiki hiyo, vipo vitabu vya Mungu ambavyo vimeandika siku, nyakati na hatima zetu, kwahiyo, tuna kazi kubwa ya kutafuta na kujua ndani ya vitabu vya Mungu kimeandikwa nini kinachohusiana na sisi; kila mmoja ameandikiwa cha kwake. Siyo vizuri watu kugombana kwa sababu ya mafanikio ya mtu kwa sababu kila mtu ana cha kwake binafsi ambacho hata ikitokea ameuliwa, aliyemuua hawezi kuwa yeye (aliyeuliwa). Hivyo basi, haifai kuwa na wivu, kugombana, kulogana kuuana kwa sababu kila mmoja ana kusudi lake.
Kila kitu kipo kwenye kitabu cha Mungu (Isaya 34:16). Mafanikio ya kila mmoja yapo kwenye kitabu cha Bwana. Jukumu la kila mtu ni kutafuta katika kitabu cha Bwana na kusoma ili kujua mambo ya hatima aliyoandikiwa; biblia ni kitabu cha Bwana, hivyo, biashara au ndoa katafute kwenye kitabu cha Bwana. Ukiyatafuta katika kitabu cha Bwana yale uliyoandikiwa, ukayapata na kuyaishi utafanikiwa. Mambo yote yapo kwenye kitabu cha Bwana ila shida kubwa ni watu hawapendi / wavivu wa kusoma.
Neno la Mungu haliwezi kumgusa kila mmoja kwa usawa. Kuna maneno katika biblia ukiyasoma unaona kabisa yanakuhusu wewe; hali hiyo ikikupata, jua kabisa hilo ni la kwako. Mfano ni pale neno linahubiriwa, baadhi ya watu wanainuka na kwenda mbele kutoa sadaka; watu hao hujua kuwa neno hilo ni la kwao kabisa. Kwahiyo ukiona ndani ya moyo wako kunawaka jua hilo ni la kwako, likamate kabisa.
Yesu ni mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi; ni kielelezo cha mambo ambayo Mungu amewaandikia watu. Habari za Yesu zinatakiwa kuongelewa kila mahali. Namna ya kifo chake kilivyokuwa, Yerusalem yote ilikuwa gumzo; habari nyingi zilikuwa kuhusu kifo chake. Biblia inatueleza kuwa miongoni mwa waliokuwa wakijadili habari za kifo cha Yesu ni Kleopa na mwenzake. Watu hao walipokuwa kwenye maongezi yao, Yesu akakutana nao; wakamshangaa kwa kutokuzijua habari zilizotapakaa kila kona kuhusu kifo cha Yesu. Wao wakamuelezea mpaka wakamaliza. Walipomaliza, Yesu akaanza kuwafundisha.
Yesu alichambua mambo mengi kuhusu yeye. Yesu alizoea sana kufanya rejea ya maandiko kuhusu mambo yaliyomuhusu yeye mwenyewe; hakuelezea mambo ya watu wengine. Tafuta mambo yanayokuhusu wewe mwenyewe; kayatafute katika kitabu cha Bwana ili ukisimama kuyazungumza uyazungumze yale yanayokuhusu wewe mwenyewe juu ya kazi yako, biashara yako, ndoa yako, elimu yako, ndoto zako, n.k. Acha kupambana kutafuta mambo ya watu, kwa maana hakuna mtu hapa duniani aliyekuja kufuatilia mambo ya watu au kuwa mtoa maoni (commentator) wa maisha ya watu; umbeya hauleti mafanikio nyumbani mwako (Luka 24:17-27).
Ijue habari yako mwenyewe ili ujue namna ya kuieleza kwa watu wengine. Nyoosha mambo yako uliyoandikiwa, kwa ujasiri. Usione aibu kuieleza habari / mambo uliyoandikiwa; kwa wengine inaweza kuonekana ni ujinga kwa sababu hawakuandikiwa wao, ila kwako ni ya muhimu uliyoitiwa. Usiionee aibu injili kwa maana ni uwezo wa Mungu uletao wokovu (Warumi 1:16).
Sisi Ufufuo na Uzima hatuonei aibu yale ambayo tuliitiwa; wengine watasema ni upumbavu au imani potofu ila ndiyo tunayoyaamini. Tumeitiwa kurudisha wale walionaswa kwenye mashimo au mapangoni waweze kurudi kwenye miili yao, waliowekwa kwenye chupa waweze kurudi kwenye miili yao, biashara iliyopinda inyooke tena, wale ambao hawazai waweze kuzaa, wagonjwa wapone kwa neno la Bwana, na tunao ujasiri wa kusema Yesu anaweza kurudisha yote yaliyoibiwa (Isaya 42:22), Haleluya!
Yashike yote uliyoandikiwa; wale wanaokubeza hawakuandikiwa hayo. Yaseme, yaweke wazi na kuyatangaza yale uliyoandikiwa. Kila mmoja acheze mziki alioandikiwa; wapo walioandikiwa ajira, siasa, utawala, kueneza injili. Biblia ni pana sana; Petro ni mtume aliyeandikiwa mambo ya tohara, na Paulo ni mtume aliyeandikiwa habari za watu wa mataifa, na wote wanamtumikia Mungu. Hatuwezi kufanana.
Huwezi kumtambua mtu zaidi ya anavyojitambua mwenyewe. Usijikatie tamaa kwa sababu kuna watu wanasema mambo fualani kuhusu wewe kuwa huwezi; lazima ujue kuwa watu hawawezi kukuelezea vizuri. Usisikilize watu wanachosema; angalia unachoshawishika wewe mwenyewe, mfano, ladha ya kitu inatokana na ulimi ambao kila mtu anao wa kwake. Tenda uliyoandikiwa, songa mbele kwa hayo; anayekuelezea mambo yako, hayafahamu (Luka 24:25).
Yampasa mtu ayajue mambo aliyoandikiwa. Kasome ujue kusudi lako. Mambo yako / matendo yako yalishatengenezwa tangu mwanzo / awali kabisa (Waefeso 2:10); kabla wewe haupo, yalikuwepo (Yeremia 1:4-5). Kabla ya kuwa tumboni, Mungu alitujua; hii inamaana kuwa, kabla ya kuwa tumboni, kuna mahali tulikuwepo. Kabla ya kuwa tumboni, tulikuwa kwa Mungu (Mhubiri 12:7).
Ganda la nje / nyumba ya udongo iitwayo mwili / mtu wa kwanza, hupajua kwao na mitaa yake; mfano, aliyezaliwa mkoa wa Mbeya, hupajua alipozaliwa na ni mwenyeji ajuaye majirani zake na mitaa ya kwao. Vivyo hivyo kwa yule wa ndani / mtu wa pili ni mwenyeji wa huko kwao mbinguni; anaijua mitaa na majirani zake, wala akirudi kwao hapotei na harudi kama mgeni ila mwenyeji (1 Wakorintho 15:47).
Mungu akituleta duniani hutuweka tuwe namna atakavyo Yeye. Yeremia aliwekwa kuwa nabii wa mataifa. Sisi pia tumewekwa kuwa vile Mungu apendavyo; ama kwenye biashara, ualimu, udaktari n.k. Ukikifanya kile ambacho Mungu amekuweka ukifanye, kifanye kwa uaminifu; usifanye kile ambacho hukuwekwa kukifanya. Ukifanya jambo na huoni mafanikio, rudi kwenye maandiko. Kasome.
Ukimuona Yeremia anafanya unabii, kawekwa; ukimzuia utatokewa na aliyemuweka. Bwana huwatokelezea wale wazuiao waliowekwa wasitende kusudi walilowekwa kulitenda. Yule aliyekuweka anawajibika na ulinzi wako pamoja na mahitaji yako yote ili kufanikisha hilo alilokuweka ulifanye; ikihitajika fedha, Bwana ataleta fedha, akihitajika Roho Mtakatifu, Bwana atamwachilia ashuke.
Kwa jina la Yesu, Bwana naomba uachilie mahitaji kwangu na uwezo wa kufanya sawasawa na lile kusudi ambalo umeweka kwangu, ili nilitimize!
Yeremia aliwekwa kuwa nabii wa mataifa lakini alijiona yeye ni mtoto; Bwana alimwambia asijione mtoto kwa maana ataweka neno kinywani mwake. Bwana akikuweka kwenye nafasi fulani, anaweka na neema / neno lenye kufaa kutumikia nafasi hiyo; uwezo wa Yeremia kungoa, kubomoa, kuharibu na kujenga umewekwa na Bwana mwenyewe. Yeremia akisema tu inakuwa, wala hapambani. Sisi Ufufuo pia tumewekwa na Bwana juu ya nchi na mataifa kwa ajili ya kurudisha wote walionaswa kwenye mashimo na kutekwa kwenye magereza; tukiita njooo, wanarudi. Wengine wakijaribu kuwaita hawarudi; neema ya kuwaita wakaja tumewekewa na Bwana.
Kwa jina la Yesu, kuanzia leo nimewekwa juu ya familia yangu, nimewekwa juu ya mkoa wangu, nimewekwa juu ya ukoo wangu, kwa ajili ya kungoa kila uchawi ndani ya ukoo! Ngokaaa kwa jina la Yesu, kila umasikini ndani ya ukoo, ngokaaa kwa jina la Yesu, kila ugonjwa ndani ya mwili ngokaaa kwa jina la Yesu!
Tumewekwa na Bwana, kila tukingoa vinangoka. Tumewekwa juu ya taifa, mkoa na juu ya kanisa, na hatuondoshwi kizembe kwa maana Mungu aliyetuweka anawajibika na ulinzi wetu; uchawi na magonjwa vikija vitakosa nguvu. Bidii, akili na maarifa ya kutenda jambo tumewekewa; tukilogwa hatulogeki. Yatupasa kutembea kwenye reli tuliyowekewa. Mfano; treni hupita kwenye reli na land cruiser hupita kwenye barabara. Umahiri wa treni ni kwenye reli. Ukifanikiwa kupita kwenye reli uliyojengewa na Mungu hautatoka ila utakuwa mahiri (Kutoka 31:1-6).
Mungu humjaza mtu roho wa Mungu kwenye mambo aliyomweka ayafanye ili ayafanye kwa ufanisi. Hekima ya mtu huwekwa na Mungu. Chochote ambacho hakijawekwa na Mungu, siyo cha Mungu. Anayemshambulia mtu mwenye akili na hekima vilivyowekwa na Bwana hawezi kuchukua nafasi yake na hiyo akili na hekima haviwezi kuja kwake; bora kuvitafuta kwenye maandiko ya Mungu. Uwezo wa kuona fursa nao umewekwa na Mungu; asiyekuwa na uwezo huo, hawezi kuona fursa hizo.
Ukizaliwa unakuja tu / njia ya kuja kufanya kile ulichoandikiwa na Mungu (Yohana 1:6). Wote tumetumwa tokea mbinguni; kupitia miili / maganda, tunashushiwa kwenye koo fulani, familia na kabila fulani; Yesu pia, kwa jinsi ya mwili, alishushiwa kwenye ukoo wa Daudi ila alitoka mbinguni (Warumi 1:3-6). Tuna ajenda kutoka mbinguni ambazo kila mtu ameshushiwa kwenye ukoo wake ili azitimize, lakini sisi sote ni wana wa Mungu kama alivyo Yesu.
Pamoja na kuwa tuna miili, bado katika ulimwengu wa roho tunaonekana. Kwa sababu adui anaona kusudi la mtu, hutengeneza hata sheria ili kuzuia kusudi la mtu alilotumwa kulifanya. Mitume wa Yesu walitumwa ulimwenguni kote kuieneza injili (Marko 16:15). Wakiwa katika kuieneza injili, Masadukayo wakawakamata na kuwaweka kwenye magereza sababu ya wivu. Kwakuwa Mungu huwajibika na ulinzi kwa aliowaweka, akatuma malaika kuwatoa kwenye magereza ili watimize kusudi la kutumwa kwao (Matendo ya Mitume 5:17-42).
Lazima adui atuachie tukalitumikie kusudi la Bwana alilomuitia kila mmoja. Mungu akikufungulia anataka ukamtumikie yeye; hakutoi ukafanye mambo yako mengine. Husianisha maisha yako na kusudi la Bwana kwenye maisha yako. Lazima kila gereza la rohoni liwaachie watu wakafanye yale waliyoletwa na Bwana wayatimize; wachawi waliofunga watu kwenye magereza, mashimo, majangwa, mapori, kwa jina la Yesu lazima waachilie watu. Pingu zao walizofunga miguu ya watu zitabaki vile vile ila waliofungwa hawatakuwa na pingu tena; magereza yao yatabaki vilevile ila waliokuwa wamefungwa hawatakuwemo kwa uwezo wa Mungu, kwa jina la Yesu. Kwa sauti ya Bwana, watu wote waliokwenye vifungo wanakuwa huru; hawakuitiwa kuishia kwenye magereza. Tunavunja kila gereza, tunavunja kila pango na tunawatoa wote waliofichwa na kunaswa humo ili waende wakatumikie kusudi la Bwana, kwa jina la Yesu (Yohana 5:28, Warumi 8:29-30).
Mungu hakumfanya mtu ili aishiye kuwa kichaa. Mungu hakuumba mtu hata mmoja kuwa kichaa. Kila alichokiumba Mungu aliona kuwa ni chema sana (Mwanzo 1:31); watu waliojaa wivu ndiyo humtengenezea mtu ukichaa na mambo mengine mabaya.
Kwa jina la Yesu, kuanzia sasa ninakataa kukaa kwenye gereza kwa maana sikuandikiwa kuwa mgonjwa, sikuandikiwa kuwa tasa, sikuandikiwa kuwa kichaa, sikuandikiwa kupata hasara, sikuandikiwa hayo kwa jina la Yesu!
Kwenye maisha yetu lazima mtu aone kitu kuhusu maisha yake; Mungu huangalia neno lake juu ya maisha ya mtu ili alitimize. Hakuna mahali katika kitabu cha Bwana mtu kaandikiwa kuchanganyikiwa au kupooza akifikia umri fulani, au kupata talaka katika miaka kadhaa ya ndoa, au kuharibu mimba, au kufiwa mtoto, au kulogwa (Yeremia 1:12). Ni ahadi ya Mungu kwetu kuwa hatatutenda kwa mapigo aliyowapiga Wamisri (Kutoka 15:26, Kumbukumbu la Torati 7:15).
Yesu aliandikiwa mambo mengi sana na yalitendeka kama alivyoandikiwa. Mungu akiyaangalia maisha yetu anaona mengi tuliyoandikiwa hatuyaishi. Yesu aliyakataa yale yote ambayo hakuandikiwa. Yesu anatufundisha kuyafanya yale tu tuliyoandikiwa; alipokuwa hekaluni alipewa kitabu asome, ila pamoja na kupewa, Yesu alitafuta pale tu alipoandikiwa akasoma. Hata kunena kwa lugha tumeandikiwa; ujanja ni kujua yale uliyoandikiwa na kuyaishi (Yoeli 2:28).
Ukiyasoma yale uliyoandikiwa ukamaliza, funga kitabu usisome ambayo hukuandikiwa. Ukiona kuna dalili ya kupitia yale ambayo hukuandikiwa, pita katikati yao uende zako. Yesu alipotaka kutupwa kwenye korongo, alijua hiyo haikuwa hatima yake na hakuandikiwa, hivyo alipita katikati yao akaenda zake. Yeu alipotaka kupigwa mawe, wote wakapigwa uzito kwenye mikono wasiweze kumrushia mawe. kwenye korongo, alijua hiyo haikuwa hatima yake na hakuandikiwa, hivyo alipita katikati yao akaenda zake. Yesu alipotaka kupigwa mawe, wote wakapigwa uzito kwenye mikono wasiweze kumrushia mawe.
Yesu alijua safari yake itaishia msalabani ili kuiondoa laana kwa watu wote waliaminio jina lake. Baada ya kuona kila alichoandikiwa amekitimiza na yote yamekwisha, alisema naona kiu (Yohana 19:28). Kimsingi hakuna aliyemuua Yesu; aliutoa uhai wake ili auchukue tena. Baada ya kukamilisha yote, Yesu aliruhusu wamtendee yaliyo ya saa yao.
Hakuna sehemu yoyote kwenye biblia mtu ameandikiwa kukaliwa na wachawi, kulishwa nyama usiku ndotoni (ni kifungo). Yatupasa kuyakataa yote ambayo hatujaandikiwa kwenye kitabu cha Bwana. Ukiamua hivyo ni kuruhusu Mungu apambane na anayezuia kusudi, kwa jina la Yesu. Tunatembea kwenye kusudi la Bwana.
Watu wanaoinuka kuzuia kusudi la Bwana huweka vitu vizuiavyo; inabidi kushindana ili kuwapinga. Tunatoka kwenye magereza yao na tunaliendea kusudi. Mungu akimfungua mtu, analenga mtu huyo amtumikie. Tunaenda kumshinda adui kwa jina la Yesu tulilopewa kulitumia. Unavyohubiri kwa jina la Yesu, ndivyo unaileta damu ya Yesu kwa wote walio kinyume na Yesu (Matendo ya Mitume 5:28). Damu ya Yesu hutusafisha na kutuweka huru ila kwa waovu inawatandika (Ufunuo 12:11). Tunashinda nguvu zote za giza kwa damu ya Yesu yenye nguvu, yenye uweza na mamlaka.
Jina la Yesu huambatana na damu ya Yesu. Yesu alituachia 1) Jina la Yesu, 2) Damu ya Yesu, na 3) Roho wa Bwana. Tunatenda yale Bwana ameyakusudia kwa kutumia jina la Yesu na kuachilia damu ya Yesu ili tuyaishi tuliyoandikiwa, na tuyaone maajabu yaliyo katika sheria ya Bwana, uponyaji wa Bwana, kufunguliwa kwa Bwana na kurudisha; yote haya yameandikwa.


0 Comments