google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUSUDI LA BWANA LITASIMAMA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 18.10.2026
BISHOP DR JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: KUSUDI LA BWANA LITASIMAMA 

Katika safari ya maisha ya mwanadamu hapa duniani, kuna nguvu mbili ambazo mara kwa mara hukabiliana na kuvutana: uwezo wa mwanadamu wa kufikiri na kupanga, na mamlaka kuu ya Mungu ya kukusudia na kutekeleza. Binadamu ameumbwa akiwa na uhuru wa kuwa na mawazo, mikakati, na mipango mingi mioyoni mwake. Hata hivyo, uhuru huo una ukomo pale unapokutana na lile shauri kuu, la milele, na lisilobadilika la Mwenyezi Mungu. Neno la Mungu kupitia Mithali 19:21 linatupa ukweli usiopingika kuwa: "Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama."

Neno 'shauri' linalotumika katika maandiko haya halimaanishi ushauri wa kawaida wa kutoa maoni, bali linamaanisha amri iliyokwisha kupitishwa na Mahakama ya Mbinguni. Unapojifunza ulimwengu wa kiroho, unagundua kuwa binadamu anaishi ndani ya muda (time), lakini Mungu anaishi nje ya muda, yaani kwenye milele (eternity). Hii inaleta utofauti mkubwa sana wa kimtazamo kati ya kile unachokiona sasa na kile ambacho Mungu ameshakikamilisha kwa ajili yako.

Katika Isaya 46:10, Mungu anajitambulisha kuwa Yeye ni Mungu anayetangaza mwisho tangu mwanzo. Mwanadamu anapoandika kitabu au kutengeneza filamu, anaanza sura ya kwanza akielekea mwisho. Mungu hafanyi hivyo. Mungu anaanza kwa kukaa na kuandika Sura ya Mwisho ya maisha yako, Sura ya Ushindi, Sura ya Utajiri, Sura ya Uponyaji. Akishamaliza kuandika sura hiyo ya ushindi, anafunga kitabu, kisha anarudi mwanzo na kukuleta duniani ukiwa mtoto mchanga ili uanze kuishi kuelekea ule mwisho uliokwisha kuandikwa.

Hii ina maana kwamba, unapopita kwenye mateso, unapolia, unapofilisika, hizo ni sura za katikati tu za kitabu chako. Kitabu chako hakiwezi kufungwa au kuishia njiani kwa sababu Sura ya Mwisho ilishatengenezwa na Mungu na inasema: "Ulishinda!" Kila aliye hai, ipo sababu kwanini yupo hai; kusudi lako lazima litimie ndiyo uende mbinguni. Hakuna mtu atakayeondoka duniani mpaka kusudi lake litimie.

Adui (Shetani) hana shida na miili yetu, majina yetu, au elimu yetu ya darasani. Kila unapoona unakumbana na dhoruba kubwa ambazo huzielewi, iwe ni magonjwa yasiyo na vipimo vya hospitali, kukataliwa kazini, au mifarakano isiyo na sababu kwenye ndoa, hiyo ni ishara ya wazi kuwa kuna kitu kikubwa kilicholala ndani yako ambacho kinatishia ufalme wa giza.

Kama ambavyo Farao na Herode walivyoua watoto wachanga wakitafuta kuua kusudi la Mungu ndani ya Musa na Yesu, vivyo hivyo shetani hujaribu kukatisha maisha au matumaini ya watu mapema kabla hawajagundua na kutimiza kile walichoitiwa. Hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya; Shetani hapotezi risasi yake kumpiga mtu asiye na kitu. Akikushambulia, ujue kuna kusudi la Mungu limefichwa ndani yako. Hata hivyo, kwa sababu ni kusudi la Mungu, adui hawezi kushinda.

Kila mtu anayekuja duniani amekuja kwa ajili ya kazi maalum (special mission). Mungu hakuleti duniani ili uishi tu bila malengo; unakuja ukiwa na mkataba ambao unatakiwa uutimize. Mara tu kusudi hilo linapokamilika, hitaji la mtu kubaki duniani linaisha. Maisha ya Mfalme Daudi katika Matendo ya Mitume 13:36 yanathibitisha kuwa, mtu akitimiza kusudi lake, analala; imeandikwa, "Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu." “Katika kizazi chake” inamaanisha ni miaka sabini.

Kama ilivyokuwa kwa Daudi, adui hawezi kukatisha maisha yako ukiwa katikati ya kutimiza kusudi; Mungu atakulinda mbele ya maadui zako wote mpaka ukamilishe ulichoitiwa. Wanaokuchukia hawawezi kuzuia kusudi la Mungu lililo ndani yako. Imeandikwa katika Zaburi 33:11 kuwa, “Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi." Mawazo, hila, na mipango ya kibinadamu au ya kichawi ina ukomo wa muda na inaweza kubadilika au kufutika wakati wowote, lakini shauri la Bwana ni la milele.

Wakati adui au wachawi wanapojaribu kupigana na maisha yako au afya yako, hawapigani tu na wewe kama mtu binafsi; wanajaribu kuzuia "Makusudi ya moyo wa Mungu" yaliyopangwa kupita kwako kwenda kwa vizazi vyako. Kwa sababu Mungu analinda makusudi ya moyo wake mwenyewe, atahakikisha anakulinda na kukuvusha ili mnyororo huo usikatike.

Hakuna kiumbe chochote, kiwe ni wachawi, waganga, roho za ugonjwa, au mifumo ya kibinadamu, kilicho na uwezo wa kuzuia kile Mungu alichokisimamisha; katika kitabu cha Ayubu 42:2 imeandikwa kuwa, "Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika."

Omba kulitumikia na kulikamilisha kusudi la Mungu kwenye kizazi chako kama alivyofanya Daudi kwa maana hakuna awezaye kuzuia, ili siku yako ya kuondoka ikifika uondoke kwa ushindi.

Tunajifunza pia kuwa, hata kama hakuna awezaye kuzuia kusudi la Bwana, bado utajaribiwa ikiwa ni ishara ya kutaka kuzuia kusudi la Bwana.

1.   Unaweza ukashambuliwa kwa maneno ya kukatisha tamaa na kejeli kutoka kwa ndugu au jamaa zako wa karibu: 1 Samweli 17:28 - Eliabu, kaka mkubwa wa Daudi, alimshambulia kwa maneno Daudi alipofika uwanja wa vita, kuwa Daudi ni mwenye kiburi na mbaya wa moyo. Dhihaka hiyo haikubadilisha kile Mungu alichopanga juu ya Daudi. Siku zote, kusudi la Mungu liko palepale.

2.   Unaweza ukataka kuuawa: 1 Samweli 18:10-12 - Sauli (mwenye dola na mamlaka) alijaribu kutumia nguvu na silaha kumuua Daudi. Sauli hakuwa anapambana na sura ya Daudi, bali alikuwa anapambana na kusudi la ufalme lililokuwa ndani ya Daudi. Sauli alijua kichawi (kupitia Samweli aliyetabiri) kuwa ufalme umehamia kwa jirani yake (Daudi).

Maadui wanaoshindana na wewe ofisini, mtaani, au ndani ya familia, wameona hatima yako kichawi; wanarusha "mishale na mikuki" ya magonjwa, umaskini, au fitina ili wakubamize ukutani. Lakini kwa sababu umebeba kusudi, hata wakirusha mkuki mara ya kwanza au ya pili, utakwepa na utatoka salama kwa sababu Bwana yuko pamoja na wewe.

3.   Unaweza ukapandikiziwa hofu ndani ya moyo wako ili ukimbie kusudi: 1 Samweli 27:1 – Daudi aliyemwua Goliati na aliyekuwa na hatima kubwa, kuna wakati uoga ulimjia moyoni mwake akadhani atakufa mikononi mwa Sauli.

Watu waliobeba makusudi makubwa huingiwa na uoga pia. Unaweza ukajiona umekwisha, unaweza ukaona uoga wa maisha, umri, au umaskini unakusonga, lakini hata uoga wako mwenyewe hauna nguvu ya kuzuia kusudi la Mungu kutimia; Mungu atakuvusha tu.

Watu wanaweza kukusema vibaya (kama Eliabu), wanaweza kurusha mikuki ya mateso (kama Sauli), na unaweza kuingiwa na hofu (kama Daudi); lakini kwa sababu neno la Mungu linasema "Shauri la Bwana litasimama," hakuna hata mmoja wao atakayefanikiwa kuzuia hatima yako (kusudi la Bwana). Utaishi na utalitumikia kusudi mpaka liishe. Hakuna serikali, jeshi, dini, uchumi, wala mtu yeyote anayeweza akabadilisha kilichopangwa na Mungu juu ya mtu. Kwa kadili watakavyojipanga kumzuia mtu, ndivyo watakavyomsukuma mtu kulifikia kusudi la Bwana juu ya mtu huyo.

Wachawi wanaona kile kilicho ndani ya mtu:

Unaweza kuwa unatembea mtaani kama binti au kijana wa kawaida kabisa, unajiona huna mbele wala nyuma, na pengine unajidharau, lakini katika ulimwengu wa roho, wachawi wakikuangalia hawakuoni jinsi ulivyo sasa; wanaona kile utakachokuwa kesho.

Wachawi wanaona nyota yako ya biashara, wanaona kuwa utakuwa bilionea, mke wa mheshimiwa, mbunge, rais, au mtu mkubwa wa kuikomboa familia yenu. Wachawi wanajua kesho yako imelala ndani yako kama jitu la mbinguni, na ndiyo maana wanakupiga vita leo ili kuzuia kile walichokiona kisije kikatimia. Ipo mifano;

1.   Mamajusi wa Mashariki:

Imeandikwa katika Mathayo 2:2 kuwa, "Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia."

Mamajusi wa Mashariki walikuwa ni wachawi na wasoma nyota. Waliiona nyota ya ufalme wa Yesu tangu akiwa katoto kachanga kalikolazwa kwenye zizi la ng'ombe; hawakumuona mtoto Yesu kwa umbo lake kama mtu wa kawaida, bali walimuona kama Mfalme wa Wayahudi.

Hii inathibitisha kuwa wachawi wana uwezo wa kuona nyota ya mtu tangu akiwa mdogo au akiwa katika hali ya chini sana. Wachawi wanakupiga vita si kwa sababu una fedha sasa, bali kwa sababu wameona nyota ya ufalme na mafanikio makubwa ndani yako.

2.   Mchawi Balaamu (Yoshua 13:22):

Kumkodisha mchawi ili amlaani mbeba kusudi la Bwana (Hesabu 22:6). Mfalme Balaki alimkodisha mchawi Balaamu aje kuwalaani wana wa Israeli kwa sababu walikuwa na nguvu. Hii ni kama jirani au mtu wa karibu asiye mchawi (mshirikina) lakini anaenda kwa waganga kulipia fedha ili ulaaniwe upindike mdomo, ufilisike, au usizae ili akuchukulie nafasi yako.

Mchawi Balaamu alipopanda juu ya kilima ili alaani, Mungu aligeuza kinywa chake akatamka (Hesabu 24:17), "Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo, Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli ..."

Mchawi Balaamu alikuwa na uwezo wa kuona miaka 1500 ijayo, kwa maana aliona nyota ya Yesu Kristo ikitokea kabila la Yuda wakati ule wana wa Israeli wakiwa bado jangwani hawajafika hata nchi ya ahadi.

  1. Vita dhidi ya wazazi na uzao:

Wakati mwingine wazazi hupita kwenye misukosuko mikubwa, mfano umaskini, na dhoruba nyingi maishani mwao. Vita hivi siyo kwa ajili yao; machawi huona kuwa kuna binti au kaka atazaliwa kupitia wazazi hao ambaye atakuwa hatari kwa ufalme wa giza. Wachawi hujaribu kuwatesa wazazi ili uzao usitokee. Lakini kwa sababu tuko hai leo, kusudi lazima litimie mbele ya macho yao.

Hata kama maadui wamejipanga kichawi kwa njia moja ili binti asiolewe, asizae (kama walivyofanya kwa Hana na Sara kabla hawajazaa majitu ya mbinguni, Samweli na Isaka), watatawanyika kwa njia saba (Kumbukumbu la Torati 28:7).

Huwezi kusimamia kusudi la Mungu ukiwa umekaa kimya na mnyonge. Ni lazima kuvaa silaha zote za Mungu (Waefeso 6:14-17) kwa ajili ya kuwa tayari kuzuia mishale na mikuki ya giza, na kuwashambulia maadui wanaosimama kutaka kuzuia kusudi la Mungu ndani yetu. Tunawashambulia maadui kwa Upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu.

Neno la Mungu si maandishi yaliyokufa; li hai, lina nguvu, lina macho, lina pumzi, lina akili, lina moto, na ni kali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili (Waebrania 4:12); pia ni kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande (Yeremia 23:29).

Tunautumia Upanga wa Roho kufyeka kila adui, katika ulimwengu wa roho. Kufyeka ni kitendo cha kuchomoka na kulitamka andiko la neno la Mungu kwa kinywa na kwa mamlaka kuelekea ulimwengu wa roho.

Unapoomba na kusema: "Imeandikwa, usimwache mwanamke mchawi kuishi" au "Imeandikwa, wakija kwa njia moja watatawanyika kwa njia saba," hapo ndipo unakuwa unachomoa Upanga wa Roho na kuanza kuwafyeka maadui. Ukilitaja andiko, tayari unageuka kuwa vile Neno lisemavyo, mfano rungu (unapondaponda), moto (unachoma) na Upanga (unakata vichwa vya adui / unafyeka).

Kuna muda waliofyekwa wanaonekana bado wapo hai na wana nguvu; usivunjike moyo, hiyo ni sawa na kukata jani la kijani la mti. Jani likatwapo, kwa muda litaendelea kubaki na ukijani wake bila kunyauka; baada ya muda litanyauka na kupoteza rangi na ndiyo mwisho wake.

Unapowafyeka wachawi, magonjwa (kama kansa au corona), au matajiri wa kishirikina wanaotumia nyota za wana familia, wanaweza kuonekana bado wanatamba na kung'aa kwa siku chache. Usiangalie ukijani wao, wameshafyekwa rohoni na ni suala la muda tu itadhihirika mwilini na ndiyo mwisho wao.

MAOMBI YA VITA:

Ee Bwana Mungu wangu, ninasimama kwa mamlaka ya Jina la Yesu Kristo; Ninavunja na kusambaratisha kila ratiba, mipango, na mikakati ya ufalme wa giza iliyopangwa kinyume na maisha yangu, afya yangu, na uchumi wangu wiki hii;

Kila madhabahu ya ukoo inayosema sitavuka, ninaiteketeza kwa moto wa Roho Mtakatifu;

Ninaamuru mipango ya kibinadamu ianguke, lakini Shauri lako Bwana lisimame juu yangu! Kwa Jina la Yesu, Amina!

MAOMBI YA KUINULIWA:

Kwa Jina la Yesu, ninaamsha kila karama na kusudi lililolala ndani yangu;

Mimi ni mbegu ya Mungu; ninakataa kuzikwa na dharau au umaskini; Ninachomoza sasa na kwenda kuwa kichwa na sio mkia;

Ninatamka malango yangu ya baraka yafunguke, na kile Mungu alichokisema nitakuwa, nitakuwa kwa utukufu wa Jina lake! Kwa Jina la Yesu, Amen!

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments