Monday, August 20, 2012

UJUMBE: LAANA YA FAMILIA.

Josephat Gwajima
Mchungaji Kiongozi
Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima:  19.8.2012

Utangulizi:
Biblia inasema Mtu mwema huacha akiba kwa wana wa wanawe, kumbe mtu mwema huwa anaacha urithi kwa wanawe na wana wa wanawe, yaani Baraka za wema wake zinaweza kufikia hadi kwenye kizazi cha wanawe; kimsingi ni ukoo wake. Jambo hili ni bayana; kwahivyo kama laana zaweza kupita hadi kwa wana wa wana, hata laana nazo zinaweza kupita kwa namna hiyo. hiyo kuna familia ukiziona, unaweza kubaini kirahisi kuwa zinatembea ndani ya laana. Kwahiyo leo tutagusa laana ya familia

BARAKA ZAWEZA KUINGIA KATIKA FAMILIA:
Biblia inasema Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;  Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. MITHALI 13:22, hili andiko linaonyesha kuwa Baraka yaweza kusafiri kutoka kwa mtu mwema hadi kwenye ukoo wake.  Hivyo unachotenda leo ni matokeo ya baadaye ya kwenye familia au ukoo wako. jambo hili; pia imeandikwa, Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;1Petro 1:18, wazazi wanaweza kumletea mtu mwenendo usiofaa, hivyo unaweza ukamuona mtu anamwenendo usiofaa kumbe ameurithi amerithi kutoka kwa wazazi/ mfano mama alikuwa kahaba na mototo naye ni kahabba; baba alikuwa maskini na motto naye ni maskini. Hili jambo liko wazi kwenye biblia.

MIFANO YA BARAKA AU LAANA:
Ukiangalia kwenye Biblia; kila jambo baya alilolifanya mtu lazima lilikuja kuleta madhara kwa mwanawe au wana wa wanawe. Mfano; Mfalme Sauli katika ufalme wake alitenda yaliyo maovu mbele za Bwana, hivyo wanawe wakashindwa kurithi ufalme, ingawa alikuwa na wana kama Yonathani ambao wangeweza kurithi lakini kwasababu ya ile laana ya baba yao sauli hawaweza kurithi. Hivyo laana zaweza kupita kutoka kwa babu au baba na kuja  kwenye maisha yako, kama babu au bibi alionea watu miaka hiyo hata kama watoto wake hawajui chochote laana inatembea hadi kwao.

Na ndio maana watumishi wa Mungu wengi unaowaona wanatenda kiurahisi kwenye huduma mara nyingi huwa kuna historia ya babu au baba au mtu kwenye ukoo aliyekuwa mchungaji; Mkimwona mtumishi wa Mungu TD Jakes, na yote yale anayotenda, katika historia yake baba yake alikuwa mchungaji na kanisa alirithi kutoka kwa baba yake hivyo ile Baraka ya uchungaji wa baba yake inapita hadi kwa motto na anafanikiwa kwenye huduma.  Hivyo Baraka pia zaweza kupita kutoka kwa baba na kuingia kwa wanawe au familia.

 Imeandikwa, “nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.  1Timotheo  1:3; kumbe imani yaweza kurithishwa; kuna imani tofauti duniani lakini kumbe nazo zinaweza kurithishwa, yaani mama mcha Mungu anakuwa na watoto wachamungu au mama mchawi anakuwa na watoto wachawi, laana ya uchawi hupita hadi kwa watoto na ndio huo ndio wanaita mkoba. Hivyo kuna Baraka inayotembea ndani ya familia na laana inayotembea ndani ya familia.

MUNGU ALIPOTAKA KUMBARIKI ABRAHAMU, ALIMTENGA KWANZA:
Abrahamu alikuwa anaishi katika huru ya Wakaldayo, na Wakaldayo kwa asili walikuwa hawamwabudu Mungu wa mbinguni wao walikuwa wanaabadu sanamu. Hivyo; Mungu alijua kuwa Abrahamu asingeweza kushiriki baraka kwasababu ukoo wake hauko vizuri na kwa vile Mungu alikusudia kumbariki, ikabidi amwambie Abrahamu undoka ujitenge nao. Imeandikwa, Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;Mwanzo 12:1-2.

Kumbe, Mungu alipotaka kumbariki Abrahimu alimtenga kwanza kutoka kwenye ukoo aliokuwamo, Mungu hakuvunja kanuni yake, maana huwezi pokea Baraka usipotengwa kwanza na ukoo, huku ni kutengwa katika ulimwengu war oho na hakuna haja ya kwenda kuwambia kwamba nawatenga ndugu maana Mungu amekukusudia.hivyo ni muhimu kukataa kujiungamanisha na laana za ukoo au familia. Kwa habari ya Abrahamu tunajifunza kuwa,  mtu yoyote akitaka kupokea Baraka kutoka kwa BWANA ni lazima utengwe na laana za ukoo.

LAANA INAWEZA KUIFUATA FAMILIA:
Kama tulivyoona Baraka zaweza kupita kutoka kwa babu au bibi na kufika kwa wanawe na hata wana wa wanawe,  na ndio maana biblia inasema kwa habari ya sanamu, Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, Kumbukumbu 5:9, Mungu hupitisha laana kwa watu waovu, hili jambo liko wazi kwenye biblia. Wana theologia wakawaida wanahesabu kuwa kizazi kimoja ni miaka 70 hadi 80, lakini kwa kawaida wastani wa maisha inatofautiana nchi hadi nchi, kwa Tanzania ni miaka 45 lakini japani ni watu wanaishi hadi miaka mia na thelathini, hivyo utaona kuwa laana ya Tanzania ni kubwa zaidi.

Na ndio maana biblia inasema utajenga nyumba halafu hutakaa maana yake siku za kuishi zinapungua kiasi cha kushindwa kukaa kwenye nyumba uliyojenga, hiyo ni laana.sasa laana ya kuishi muda mfupi iki[pita kwenye ukoo, Maana yake baba alikufa na miaka michache na motto naye anakufa katika umri mdogo na kadhalika wana wanawe, na wana wa wana wa wanawe. Laana ina tabia ya kutafuna, ikianza inaenda hadi kwenye maisha ya wanaukoo wako.

Tuone mfano wa agano jipya; wakati Yesu alipokuwa anaenda msalabani, wanawake walikuwa wanamlilia Yesu, Yesu akawambia walilieni wana na watoto wenu, kwanini Yesu alisema hivyo; Yesu alijua kuwa laana ya damu ya mtu mwenyehaki ni lazima ipitilize hadi kwa wana wa wanawe, hivyo akawaonya kuwa walilieni watoto wenu kwasababu ndio watako shiriki madhara yah ii laana. Biblia inasema, Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.Luka 23:28

Na ndio maana hata Pilato alipoona Yesu hana hatia, wakati wa kutoa maamuzi alinawa mikono ili kujitoa kwenye laana ya ile damu, Lakini wayahudu wakamwambia tukabidhi tumuue na damu yake iwe mikononi mwetu na kwa wana wa wanetu; wayahudi walijua kuwa laana yaweza kupita kwa wanaukoo. Imeandikwa, “Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.Mathayo 27:25; Kama wangekuwa hawalijui hilo wasingesema maneno yale. Kimsingi maneno yale yalimaanisha kama mtu huyu hana hatia basi laana yake iwe juu yetu na watoto wetu.

KANUNI YA LAANA ZA FAMILIA:
Hii tunaweza kuiona katika Joshua 7:2-26, habari ya wana wa Israeli walienda vitani na kujikuta wamepigwa, lakini Joshua alivyoomba akaambiwa kuna uovu katikati yenu, kumbe mtu mmoja alisababisha laana katika nchi. Akani alisababisha wana wa Israeli kushindwa vita, Tunajifunza kuwa unaweza kuona nchi masikini kumbe kuna mtu mmoja amesababisha (Aliyesababisha umaskini wa Tanzania apigwe kwa jina la Yesu},  ingawa aliyekosea alikuwa Akani akalifanya Taifa la Mungu lote kupata laana; Imeandikwa, mstari wa 24’ Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori ; 26’ naye Bwana akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo 

Hapa tunaona kuwa aliyesababisha laana ile alikuwa mtu mmoja naye ni Akani lakini utajiuliza kwanini waliwachukuwa hadi watoto wake na ng’ombe na vitu vyake? emu pata picha wanawe na mkewe hata vitani hawakwenda na ng’ombe ndio hawahusiki kabisa, utasema Mungu hana huruma? Kimsingi: kanuni ya laana ni kwamba inapiga kuanzia mwenye laana hadi wanawe wote na ukoo na familia nzima. Unavyotenda haki leo unatengeneza maisha mazuri ya wanao, ukoo na hata taifa, biblia inasema, Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu  wote.Mithali 14:34. Kama haki inavyoinua taifa ndivyo laana inavyoangamiza taifa. Kama viongozi wanatumia uchawi basi lazima nchi itaingia kwenye laana na taifa kudidimia.

Kwahiyo; kanuni ya laana ya familia ni kupiga kuanzia babu, baba hadi watoto, na hapo jaribu kuchunguza maisha ya babu au bibi yako yalikuaje; alafu angalia maisha yako. Lazima utakuta uhusiano uhusiano. Kama si kwa babu kwa bibi, mama au baba au baba mkubwa lazima. Kama wazee wako walinuonea mtu na jambo lile likafanyika laana basi lazima ije hadi kwako na kama usi[poivunja itaangamiza maisha yako.

Ukisoma katika kitabu cha 2samweli 3:17-26; Hii ni habari ya Abneri alimkosea mfalme Daudi, lakini baada ya muda Abneri na Mfalme Daudi wakapatana; jambo hili halikumfurahisha Yoabu mkuu wa majeshi wa daudi, akaamua kwenda kwa siri na kumuua Abneri, na Daudi aliposikia hayo; akamtajia Laana Yoabu katika mstari wa 24’ na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula.” Unaona hapo huyu Yoabu ndiye aliyemkosea BWANA lakini laana yote iliwaendea na ndugu na ukoo wake. Hii ndio tafsiri ya ile laana:
·        Ukoma tafsiri yake ni mtu mwenye kupata na kupoteza. Yaani unapata alafu haidumu. Unapata kazi alafu haikai, yaani unapata na kunyanganywa hii ni laana ya familia. Kama upo katika ukoo ulio laaniwa na unatokea kwenye ukoo huo basi lazima uishiriki laana hiyo.
·        Mwenye kutegemea mti; yaani unakuwa na maisha ambayo yanategemea watu wengine, au ndugu yaani unakuwa uwezi kujitegemea ndio maana nchi za Afrika kila kukicha zinategemea msaada kutoka nje hii ni laana, sasa laana hiyo ilipita hadi kwa wanao. (dependency).
·        Anayetembea kwa kuchechemea; mtu huyu awezi kuwa na maendeleo endelevu, akifanikiwa katika jambo halidumu, kila siku anarudi palepale.. hii ni laana ya familia.
·        Mwenye kuhitaji chakula; huyu ni mtu ambaye hawezi kujitosheleza kwa mahitaji yake.  na ndio maana mtu anaweza kuwa mshahara mzuri lakini kila akipata mshahara hela haionekani inakoenda. Hii ni laana na watu wengi wanaishi kwenye laana hii bila ya wao kujua.


MAAGANO YA FAMILIA (FAMILY COVENANT): 
Kama unavyojua historia ya ukristo katika Afrika na hata katika nchi yetu ni fupi sana, yaani ukristo haukuwepo tangu zamani sana kwa hapa Afrika. hivyo kabla ya hapo wazee na mababu walikuwa wanaabudu mizimu, na koo zilikuwa na mazindiko ya ukoo. Wao walikuwa wanaita ulinzi, na ndio maana kuna nyumba ambazo akienda kama ni mchawi ananasa sio kwamba ni ya kiMungu, bali kunashetani kubwa linalo weza kumkamata mchawi asiye na nguvu. Na ndio maana koo nyingi sana ambazo ni ndogo, kubwa na maarufu zimekabidhiwa kwa shetani kwa namna hii.

Maagano haya ndio yanayoleta laana kwenye familia, kwasababu maagano haya hufanya familia kuwa chini ya shetani maana mnakuwa (familia) mmeingia mkataba na shetani. Na hapo mashetani yanakuwa yamekabidhiwa familia, na  ndio mahali shetani anahusika na maisha yako moja kwa moja. Na ukitaka kusaidiwa shetani anakuja juu kwasababu kuna mikataba. Husipoushughulikia huo mkataba huta funguliwa.

Maagano yanaweza kutokana na kupigwa chale; inawezekana ulipozaliwa mama yako alienda kwa mganga, na akapigwa chale ndipo ukapatikana wewe ile damu iliyomwagika ni uhai (Walawi 17:11), hivyo uhai wa familia unakuwa umeuzwa! Ili jambo ni halisi kabisa katika ulimwengu war oho. Unajina unapita kwenye tatizo au ugonjwa kumbe shida ni maagano ya ukoo.

MIKATABA INAYOTOKANA NA MILA:
Mila za kifamilia zaweza pia kutuingiza kwenye mikataba; ukifuatilia historia inashangaza, mfano; kwa wanyamwezi au wasukuma watu wa kanda ya ziwa wanamuita mungu wao mashala, lakini pia kwa waislamu wanatumia jina hilo Mashala yaani mungu wa rehema, wakati hupohuo huyu mungu wa wasukuma sio Mungu Jehova, ni mungu mwingine tu. Kwahiyo mila zaweza kukuweka kwenye laana. Mfano wachawi hutambika kwenye mizimu, hiyo ni mikataba ya kifamilia inayoletwa na mila, na ndio maana utawakuta wanafamilia au wanaukoo wote wanakuwa na matatizo yanayo fanana.

Mikataba hii inafungua milango kwa shetani kushambulia maisha ya watu kwenye familia hiyo. Mfano; mila ya kunyoa nywele wakati wa msiba, ushawahi kijiuliza kwanini? Historia fupi ya kunyoa nywele, hii haibishaniwa kuwa wanadamu walianza kuishi mashariki ya kati na hapo waliaanza kusambaa duniani. Na hata ustaarabu ulianzia hapo, watu wa Mesopotamia (Iraq ya leo) walikuwa wanaamini mtu akifa anaenda katika ulimwengu wa wafu (sheol) na walipokuwa wakinyoa nywele walisema “nitakuja pale pale unapokwenda”  yaani huko alipo. Na hapo walinyoa nywele kama ishara kuwa lazima niende pale ndugu yangu alipokwenda, utajiuliza imeingiaje kwetu?: kupitia ya historia ya kawaida waarabu walianza kusambaa kutoka Iraq na kupitia Misri, Somalia hadi kufika Arusha kwa wamburu na ndio maana asili ya wamburu ni Iraq. Hivyo kutoka hapo wakasambaza mila ya kunyoa nywele mtu akifa; lakini kwa asili hiyo ndio maana yake.

Hivyo kunyoa nywele ni jambo la kimila na maana yake sahihi, ni pale alipokufa, alipoenda, yanayompata marehemu na mimi vilevile, ukili wa maneno haya ndio unadhihirishwa kwa kunyoa nywele; hivyo huo ni mkataba kabisa na unampa nafasi shetani kuingia kwenye ukoo; biblia inasema “wala msimpe ibilisi nafasi” Waefeso 4:27. Kitu kingine ni mila ya kisusio Kumbukumbu 12:23; Matendo 15:20 bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. BIBLIA imekataza kula nyama pamoja na damu yake, na hili limekatazwa katika agano jipya na la kale; kula vitu hivyo vya kimila ni kujiweka kwenye mikataba bila kujua, damu ni uhai kwahiyo unapokula nyama pamoja na uhai wake ni kujiweka katika maagano ya kimila hivyo kuleta laana kwenye ukoo wako.

LAANA YA MTOTO WA DAWA:
Katika biblia tunajifunza pale mtu alipokosa mototo kwa muda mrefu, alikuwa anajikita kuomba hadi Mungu atakapo mpa mtoto, tunaona kwa habari ya Hana muona Hana alikuwa hana mototo akawa anakwenda kuomba shilo, na Mungu akamsikia (1Samweli 1), tatizo au mkataba unakuja pale wazazi wanapoenda kwa mganga wa kienyeji ili ku[pata motto; na inawezekana wewe ulipatikana kwa njia hiyo bila kuju. Kwahiyo kimsingi unakuwa umezaliwa lakini chini ya mikataba ya shetani, kwasababu ndio alisababisha uzaliwe; na watoto wengi wamezaliwa kwa njia hiyo inakuwa ni laana ya familia. Kwahiyo mtu akizaliwa kwa dawa na watoto wake watakuwa chini ya mkataba huo, sasa jiulize unajuaje kama wewe hukuzaliwa kwa dawa; utasema niliambiwa hivyo; haya aliyekuzaa unajuaje kama hakuzaliwa kwa dawa? Hii ni laana inayotafana maisha ya watu.

KUHIFADHI KITOVU CHA MTOTO:
Kuhifadhi kitovu cha mtoto; kuna baadhi ya mama wakipata watoto wao huwa wanahifadhi kitovu mahali, aidha kwa kuelekezwa na mganga au matakwa ya mila. Na maranyingi bibi wa watoto ndio wanao chukua kitovu hiko. Kwahiyo; kama ulifanyiwa hivyo maisha yako yanakuwa yanafatiliwa na shetani, kwasababu anakitovu chako; na watu wengi wanaishi kwenye vifungo bila kujua kwasababu utotoni, walifanyiwa ivyo bila ya wao kujua. Kile kitovu ni ushahidi wako maana kina seli hai zako na genes zako hivyo wanaweza kudhibiti ukuaji wako kwa njia hiyo. Vunja laana za ukoo na familia kwa Jina La Yesu.

WOKOVU KAMILI:
Unapookoka unakuwa umezaliwa na Mungu. Lakini ili upate wokovu kamili unatakiwa ufunguliwe nafsi, mwili na roho; roho yako  iende mbinguni, nafsi ijae  neno na mwili wako uponywe magonjwa, tabu na laana. Kuokoka sio kuwa maskini, na ndio maana Yesu alimwambia Petro maneno haya Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.Mathayo 19:29.

Watu wengine hufikiri kwasababu hawapagawi mapepo basi hawapo kwenye laana. Kuna wakati wengine shetani sio lazima aingie ndani yako ili upagawe pepo. na ndio maana biblia inasema, “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Shetani hakuwa ndani ya Kuhani Joshua; lakini aliweza kushindana naye; hivyo kuna mtu hapagawi mapepo lakini shetani anashindana kutokea nje. Pia ukisoma katika Matendo 13:8; kumbe, shetani aweza kufanya vita na wewe akiwa nje. Inachokifanya; unapokwenda kuomba kazi mahali anamwingia Yule anayetakiwa akupe kazi, au unaomba viza anamwingia yule mtoa viza ili hasikupe viza;  Hapo mtu anakuwa halipuki pepo lakini yupo kwenye kifungo cha laana ya familia

Kumbe ukiokoka unatakiwa utoke kwenye laana za ukoo, utajiri ni haki yetu, uhuru ni haki yetu; lakini Maisha ya watu wengi yameingizwa kwenye mikataba. Usipoivunja mikataba uwezi kupata ushindi kamili kwenye maisha yako; Watu wengi huwaza kuwa unapookoka mikataba inakatika yenyewe automatically, si kweli bali kuokoka ni kupokea mamlaka ya kukuwezesha kuivunja mikataba hiyo; lakini usipoivunja bado inaendelea kuwepo.

Biblia inasema, Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.Luka 10:19 .. unapookoka unapewa mamlaka ya kukanyaga nyoka, kimsingi usipokanyaga hawawezi kutoka kwenye maisha yako, hivyo ili upokee mafanikio unatakiwa usimame kuvunja laana za familia na ukoo. Tumia jina la Yesu kila wakati (Yohana 14:13,14). hatuombi kwa kutumia jina jingine lolote bali tunatumia jina la Yesu.

Watu wengi huwa wanasubiri kuombewa; bila kujua kuwa wana mamlaka ndani yao. Si vibaya kuombewa na biblia inaruhusu lakini pia kuna wakati unapitia hakuna wa kukuombea hivyo inabidi ujue kutumia mamlaka uliyo nayo. Paulo anasema vita amevipiga mwendo amemaliza, kumbe kabla ya kumaliza mwendo kuna kuvipiga vita; Huwezi kumiliki bila kupigana  Waefeso 6:12.  Mungu akubariki sana…. 

{UTAIFAHAMU KWELI NAYO KWELI ITAKUWEKA HURU: YOHANA 8:32}

1 comment: