Monday, September 2, 2013

NI KWELI MUSA AMEKUFA LAKINI TUSIOGOPE

Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.( Yoshua 1:1-2)

Ni huzuni na masikitiko. Hivi ni kweli amefariki? Watu wana majonzi na masikitiko. Rafiki yangu kipenzi aliyehudhuria msiba ananiandikia ujumbe kwa kutumia wasapu. Ananiambia mjukuu wa Musa na mwimbaji wa nyimbo za injili leo hajazimia. Nami namuuliza: “kwani lini alizimia?”. Ananijibu: "Juzi alizimia". Ni kweli kuna huzuni. Watu wanamlilia Musa. Wanakumbuka alivyokuwa shupavu kuongea na Farao ili awape watu wa Mungu ruhusa waende. Wanakumbuka alivyoigawa bahari ya shamu wakavuka. Wanakumbuka alivyowatolea maji kwenye mwamba wakanywa. Ni huzuni na masikitiko kuwa Musa mtenda maajabu amekufa kabla watu hawajarithi nchi waliyoahidiwa. Ni huzuni na masikitiko.

Huenda wanawaza kwa nini Musa aondoke wakati huu. Bado tunamwitaji. Musa kweli amekufa lakini safari ya kwenda Kanaani haijafa. Musa ana upako wa kuwatoa wana Israel utumwani na kuwapitisha jangwani. Anao moyo wa kuwavumilia wanaposhindwa kumwelewa na kuanza kumlaumu. Ni mwepesi kuwalilia watu wenye shingo ngumu ili Mungu awarehemu. Sasa Musa huyu amekufa. Ni kweli amekufa na hakuna alithubutu kumfufua. Amerudi kwao alikotoka. Musa alikuwa shujaa. Shujaa karudi nyumbani kupumzika. Imani ameilinda. Mwendo ameumaliza

Katikati ya Majonzi haya, liko tumaini bado. Kuna mtu anaitwa Yoshua amevaa jezi aingie ulingoni. Asingeweza kuingia uwanjani wakati Musa yupo. Lakini alikuwa akiandaliwa. Mazingira ya mchezo yamebadilika na yanamwitaji mchezaji wa akiba. Alikuwa nje anausoma mchezo wakati Musa yuko ulingoni. Ni kweli bado tuko njiani. Mechi inaendelea. Yoshua kavaa jezi ileile yenye jasho ya Musa. Kocha anajua muda wa kumpumzisha Musa ili Yoshua ainngie. Yoshua yeye ana upako wa kuwavusha watu mto Yordani na kuwaingiza Kanani na kuwamilikisha ahadi yao. Yoshua ni mhubiri kijana. Hasubiri mto ugawanyike kama bahari ya shamu ilivyogawanyika ndo avushe watu. Yeye anawaambia watu wakanyage maji waanze safari mto ukiwa unaendelea na shughuli zake na umefurika mpaka kingo zake. Chini ya uongozi wa Yoshua Mnakanyaga kwanza maji ndo yanasimama. Hayasimami na kuwa chuguu ndo mnavuka. Mnayakanyaga kwanza. Hatari ni kubwa lakini hayo ndo maelekezo ya Yoshua

Yoshua si Musa kama ambavyo Musa si Yoshua. Wote wameitwa lakini wanatumiwa kwa staili tofauti kulingana na namna walivyoitwa. Aliyewaita ni mmoja - Mungu wa mbingu na nchi lakini anawatumia kwa namna ya tofauti. Musa amekufa na ametuacha jangwani - Hatujamiliki ahadi. Mbele tunaiona kanani lakini kuna mto Yordani umefurika. Na hata tukivuka kwa mbali kuna ukuta wa Yeriko. Ni vikwazo vizito na vya kweli kabisa. Tusiogope. Mungu ametuinulia Yoshua wetu atuvushe. Tumtii kama tulivyomtii Musa. Staili yake itakuwa tofauti lakini tumsikilize na kumtii kama tulivyomtii Musa. Ana maelekezo muhimu ya kutuvusha na kutumilikisha. Akisema tuukanyage mto ili tuvuke, tumtii. Tusimuulize mbona Mzee Musa alikuwa anayagawa maji ndo anatuamuru tuvuke? Nimeshawaambia Yoshua sio Musa na tusitegemee kuwa atatumia staili za Musa. Akisema tuzunguke ukuta wa Yeriko mara saba tumsikilize. Tusizunguke mara tano halafu tukasema: "mbona hatuoni nyufa kwenye ukuta. Utaanguka kweli?" Inawezekana tusione dalili za nyufa kwenye ukuta wa Yeriko lakini tukifanya kama alivyosema tukazunguka siku 7 na mara 7 siku ya saba, UKUTA utaanguka maana Mungu amesema kama alivyokuwa na Musa ndivyo atakavyokuwa na Yoshua.

NI KWELI MUSA AMEKUFA LAKINI AMEMWACHA YOSHUA. TUTAMILIKI MALANGO YA ADUI ZETU CHINI YA UONGOZI WA YOSHUA

No comments:

Post a Comment