Monday, October 27, 2014

NGUVU YA IMANI


JUMAPILI YA TAREHE 26_10_2014

MCHUNGAJI JOSEH JONES 
 
 NA MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA
 
SOMO: NGUVU YA IMANI
 

Mchungaji kiongozi Josephati Gwajima akiwa na Mchungaji Joseph Jones

Kama raia wa Tanzania unahitaji upate fedha ya Tanzania ambayo ni shilingi ili uweze kuishi ndani ya nchi hii. Utaihitaji kupanda daladala, kununua chakula  na kugharamia maisha kwa ujumla. Lakini wewe kama mtu aliyeokoka ni zaidi ya raia wa Tanzania, wewe ni raia wa mbinguni. Kama ilivyo kwa nchi ya Tanzania, raia wa mbinguni pia wana fedha ambayo ni imani. Biblia inasema mwenye haki wangu ataishi kwa imani. Hatuwezi kumpendeza Mungu wala kuingia katika ufalme wa Mungu bila imani.

“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;”  Waefeso 2:8

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waebrania11:1

Kama unataka kumpendeza Mungu lazima uishi kwa imani; ndani ya maisha ya imani kuna uponyaji, wokovu, amani, nguvu. Pasipo imani huwezi kamwe kupokea baraka hizi. Lakini imani huendana na uvumilivu.

“Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.” Warumi1:17

Imani inakuja kwa kusikia neno la Mungu, hiyo ndiyo njia pekee unayoweza kupokea imani. Unahitaji kusoma neno la Mungu, kulitafakari na zaidi kulitenda ndipo upokee imani. Kama ambavyo leo ungeenda kwenye ATM ya  benki mojawapo ya Tanzania kuchukua fedha; nenda kwenye ATM ya Mungu ambayo ni biblia ukachukue imani. Neno la Mungu ni mbegu; Yesu alitoa mfano huu wa mpanzi:

 Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?  Mpanzi huyo hulipanda neno.  Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao.  Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha;  ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa.  Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno,  na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.  Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.  Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi.  Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.” Marko4: 13  

Neno la Mungu ni mbegu ambayo siku zote hutenda kazi. Tunalipanda neno la Bwana ndani ya mioyo yetu. Baada ya muda mbegu hii hukua ndani ya mioyo yetu na kuzaa matunda. Je, ni nani aliyepanda viazi akavuna mahindi? Hayupo. Vivyo hivyo basi mtu akitaka kuishi maishi ya imani lazima apande mbegu ya imani ambayo ni neno la Mungu.

Tunaposoma neno la Mungu au kusikiliza mahubiri hiyo ni mbegu inakuwa inapandwa. Baada ya kusikia mara kwa mara kwa muda fulani mti wa imani huanza kukua. Ili kuyaona matunda ya mti wa imani inatupasa kuwa wavumilivu.

“Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.  Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.  Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” Yakobo1:21

Kukombolewa kwetu kunatokana na lile neno tunalolipokea. Kazi yetu sisi ni kulisikia neno, kulitafakari na kulitenda. Kazi ya Mungu ambaye ndiye mpanzi ni kulikuza hilo neno ili lizae matunda..

“Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Warumi10: 8

Imani ni kuamini kwa mioyo yetu na kukiri kwa midomo yetu. Unapookoka watakuwepo watu watakaokueleza habari mbalimbali za wokovu wakati kanisa nalo linajitahidi kukufundisha habari za wokovu. Wote hawa wanajaribu kupanda mbegu ndani yako. Utakachokiamini ndani ya moyo wako na kukiri kwa midomo yako hicho kitakuwa.

Imani yaweza kuelezewa kwa mfano wa ujauzito. Ili mama awe mjamzito ni lazima iwepo mbegu ambayo inapandwa ndani ya tumbo lake. Hawezi kuamka tu siku moja akajikuta ana tumbo kubwa. Wakati wa ujauzito zipo adha mbalimbali ambazo mama huyu atazipitia. Hata muda wa kujifungua unapowadia mama huyu hujua kuwa muda wake umefika bila hata kuambiwa. Zile dakika chache kabla ya kujifungua kwake huwa ni za mateso na maumivu makali sana lakini hufuatiwa na furaha isiyoelezeka baada ya mama huyu kumuona mwanaye kwa mara ya kwanza. Ndivyo ilivyo imani; lazima neno lipandwe, na hakika zitakuwepo adha nyingi utakazopitia wakati wa ujauzito wako wa imani. Na kabla tu imani yako haijazaa matunda kutakuwa uchungu ambao hufuatiwa na ule muujiza ambao ndilo tunda la imani yako. Beba ujauzito wa imani leo kwa jina la Yesu.

Mtu anaweza kuwa anajidanganya kuwa ana imani kwa kukiri maneno ya ukombozi. Lakini kama unatamka maneno hewa bila kuwa na neno ulilopanda ndani ya moyo wao huwezi kuwa na imani wala huwezi kuzaa matunda ya imani. Biblia inaiita imani ya namna hii imani iliyokufa. Kama wewe ni mgonjwa na unang’ang’ana  kusema nimepona, nimepona bila kuwa na neno la kusimamia hakika imani yako imekufa.  Unatakiwa kusema , “Imeandikwa kwa kupigwa kwale mimi nimepona, nimepona kansa kwa jina la Yesu.” Kama unataka ulinzi unasema, “Mabaya hayatanipata mimi wala tauni haitakaribia hemani mwangu, hakuna uchawi juu ya Yakobo wala uganga juu ya Israeli.” Imani ya namna hii hakika itazaa kwa wakati wake. Biblia inasema ukiwa na imani ndani yako chochote utakachokisema utakipata  sawa sawa na imani yako kama usemavyo.

Inawezekana unasema mimi ninaamini lakini siwezi kukisema ninachokiamini kwa sababu kama kisipotokea nitachekwa. Watu wengi huwa na mtazamo huu. Lakini kama huu ni muamala basi bila kutamka kile ulichopanda ndani ya moyo wako muamala huu haujakamilika. Ni lazima usikie neno ili lipandwe ndani yako halafu ukiri  kile unachokiamini.

Baada ya kupanda mbegu ya imani upo muda wa kusubiri ili mbegu hii iweze kumea, kukua na kisha kuzaa matunda. Hakuna mkulima apandaye mahindi leo na kutegemea kuvuna kesho; wala hakuna mama atungaye mimba leo akitegemea mtoto kesho. Ipo miezi tisa ya kusubiri mimba kugeuka mtoto. Watu wengi hukata tamaa wanapokosa kuona matunda ya imani yao mapema. Ili uweze kuzaa unahitaji kuwa mvumilivu kusubiri imani yako izae.

No comments:

Post a Comment