Monday, December 31, 2012

NITAPITA KATIKATI YAO 2013

Na Mwandishi wetu.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Rev.Josephat Gwajima ameutangaza mwaka 2013 kuwa mwaka wa kupita katikati ya adui zetu. Akitangaza hayo katika Mkesha wa Mwaka mpya kanisani hapo Mchungaji alisema kuwa "Mwaka huu ni mwaka wa Kupita Katikati Yao" 

Ufunuo huu wa kupita katikati yao unatoka katika kitabu cha Luka 4:30 imeandikwa "Lakini Yeye (Yesu) alipita katikati yao, akaenda zake."  Yesu alipita katikati ya adui zake nao hawakuweza kumdhuru. Mchungaji alisisitiza kuwa kwa kawaida ukilikwepa jaribu utalikuta mbele, unatakiwa kupita katikati yake. Majaribu yapo namna hiyo. Pita katikati, neema imeachiliwa tayari. 

Mishumaa ikiwashwa kwa  moto kutokea madhabahuni
Mchungaji Kiongozi aliyasema hayo katika ibada ya Mkesha ambapo maelfu ya watu walikuwapo kanisani hapo wakimshukuru Mungu kwa neema ya kuingia mwaka 2013 salama. Katika ibada hiyo, ilipotimia saa 6 kamili usiku, taa zote zilizimwa na mishumaa mingi  iliyonyanyuliwa juu na kila mtu aliyekuwepo ibadani hapo iliwashwa kwa moto wa mshumaa ulioanzia madhabahuni ikiwa ni ishara kuwa moto wa madhabahuni utawaka mwaka wote 2013 kwa kila mmoja na hautazimika. 

Wachungaji wakazi (Resident Pastors) wakiomba kwa ajili ya maombi 10 ambayo kila mshirika aliandika ya kwake ili Mungu amtendee kwa mwaka 2013


Sunday, December 30, 2012

UBATIZO WA KIBIBLIA KUFANYIKA TAREHE 1 JANUARI 2013


Na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima

Kila mtu aliyeokoka ni askari wa jeshi la Yesu, hivyo kama askari wa Yesu tunatakiwa kufuata kile ambacho Mungu anatuagiza, 1Timotheo 2:4; sisi ni wanajeshi wa jeshi la BWANA, Filemoni 1:2; Hivyo mkristo mwenzako aliyeokoka ni askari mwenzako.  Ndio maana katika biblia kila mahali Mungu alipojitambulisha alitumia jina la BWANA wa Majeshi. 1Samwel 15:2; 2Samweli 7:8. Utajiuliza majeshi haya ni yapi; haya ni majeshi ya Yesu ambayo ndio sisi tuliookoka. Mambo ya Nyakati17:7; Isaya 1:24;3:15; 10:24; 14:13;

Mara tu unapookolewa Yesu ambaye ni Bwana wa majeshi anatuagiza kutii amri yake.  Malaki 3:17; 4:3;  Mathayo 28:18-19, hapa BWANA wa majeshi anatoa Amri ya kuifuata. Kumbe kuwabatiza watu ni amri ya BWANA wa majeshi, hivyo tuna jukumu la kutii amri ya Yesu Kristo. Na unapookolewa Mungu anakutarajia utii amri ya mkuu wa majeshi Yesu Kristo.

MAANA YA NENO UBATIZO
Neno “ubatizo” linatokana na neno la kigiriki linaitwa “babto” au zamisha; hili neno Babto limetumika mara nyingi sana katika biblia Yohana 13:26.  Yesu alisema ambaye nitachovya naye tonge ndiye atakaye nisaliti” kumbe kuzamisha tonge katika mboga ndio mana rahisi ya kubatiza yaani chovya au kuzamisha. Kwahiyo kutokana na maana ya neno ubatizo tunaweza kujua kuwa ili mtu abatizwe anatakiwa awe kwenye maji tele.

UBATIZO WA KIBIBLIA
Yohana 3:23; kwa maana hiyo ya ubatizo ndio maana tunaona Yohana alibatiza mahali penye maji tele. Huwezi kuzamisha mtu ndani ya bakuli au birika, ni lazima maji yawe tele ili mtu aweze kuzama. Hivyo ubatizo wa kibiblia ni wa kumzamisha mtu ndani ya maji.  Na ndio maana katika kitabu cha Matendo ya mitume 8:26; hivyo ubatizo wa Kibiblia wote wawili hutelemka majini, hapo unaweza ukajiuliza je ulipobatizwa wote wawili mlitelemka majini? Kama sivyo basi ujue haukuwa ubatizo wa Kibiblia.
Na jambo lingine la kuangalia huyu towashi alihubiriwa, akaamini na kubatizwa. Unaweza ukalinganisha kama ulipobatizwa uliamini kwanza na je wote mliingia majini, na ndio maana mstari wa 29” unasema “kisha walipopanda kutoka majini” kumbe ubatizo wa kibiblia hutelemka majini na kupanda kutoka majini.

KWANINI WATU WANABATIZA NDANI YA BAKULI AU BIRIKA
Watu wengi wanayapindisha maandiko, lakini biblia inatuagiza kutumia neno la Mungu kwa halali, 2Timotheo 2:15. Na ndio maana utaona watu leo wanatumia maandiko vibaya kuwabatiza watu katika bakuli, bila kutelemka majini. Haya ndio maandiko ambayo watu huyatumia kupindisha ukweli, Hesabu 8:5-7; Mungu alimwambia Musa anyunyize maji ya utakaso, lakini huu si ubatizo bali ni utakaso. Na watu wengi waliokuwa wamefanyiwa hivi ni wale waliokuwa wameshika maiti, ilikuwa mtu ashikapo maiti anakuwa najisi mpaka amwagiwe maji ya farakano. Kimsingi huu haukuwa ubatizo wa kibiblia, bali ulikuwa utakaso tu na si ubatizo wa kibiblia.

MTU YUPI ANAYETAKIWA KUBATIZWA
Huyu ni mtu aliyetubu dhambi, kama hujatubu dhambi ubatizo wako si wa kibiblia. Matendo ya Mitume 2:37, hivyo kanuni ya Mungu ni kwamba mtu anatubu kwanza ndipo anabatizwa, lakini maeneo mengi watu hubatizwa wakiwa watoto wachanga ambao hawawezi kutubu. Hivyo kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo sio ubatizo wa kibiblia. Marko 16:15-16, Na ndio maana Yesu aliagiza kwa kusema aaminiye na kubatizwa, kumbe kinachoanza ni kuamini alafu unabatizwa.

Tumeona mambo kadhaa yanayoendana na ubatizo wa kibiblia, yaani unatubu kwanza, ndipo unabatizwa. Matendo ya Mitume 8:12, Biblia inaendelea kusema kuwa wakaamini wakabatizwa, huwezi kusema umebatizwa kama hujaamini bado. Matendo ya Mitume 8:35-38, katika biblia hakuna aliyebatizwa bila kuamini kwanza, na ndio maana Filipo alimwambia Yule towashi kwa habari ya ubatizo “ukiamini inawezekana” kumbe ubatizo wa kibiblia unaamini kwanza ndipo inawezekana kubatizwa. Ni swali la kujiuliza kuwa ulipobatizwa uliamini kwanza.  Matendo ya mitume 19:1-…

UBATIZO UNAWEZWA KUFANYWA KWA MTOTO MCHANGA
Mtoto mdogo hawezi kuamini, na kwa maana hiyo hawezi hata kutubu dhambi zake. Mama au baba wa ubatizo hawezi kutubu kwa niaba ya mtoto, huu ni usanii na si ukweli kabisa. Mtu anatakiwa asikie mwenyewe na atubu mwenyewe pasipo kujibiwa na mtu. Kwahiyo jibu la swali hili kuhusu ubatizo kwa watoto wadogo ni kwamba hakuna ubatizo kwa watoto wadogo, kwasababu hawezi kuamini, na pia ukimzamisha mtoto katika maji unaweza ukamuua.

Kwa maana hiyo; kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo haukuwa ubatizo. Na hata ukiamua kubatizwa ubatizo wa KIBIBLIA sio kwamba unabatizwa kwa mara ya pili bali ni mara ya kwanza, ule wa kwanza haukuwa ubatizo. Katika biblia mama au baba awezi kumuaminia mwanaye imeandikwa,Ezekieli 18:20. Kuwa baba hawezi kuchukua uovu wa mwanaye. Hata hivyo dhambi ya mtoto haihesabiwi kwasababu akili yake haijaweza kuitambua sheria bado, hivyo dhambi inaweza kuwepo lakini haijaanza kuhesabiwa kwasababu hawaijui sheria bado.

Kwa asili, mtoto anakuwa amezaliwa na asili ya dhambi, lakini haihesabiwi, Warumi 5:12-13 kumbe dhambi haisebawi kwa mtoto kwasababu haijui sheria na wala haijawa wazi kwake. Warumi 4:15. Matendo 2:38; Biblia inasema kwa siku moja walibatizwa wakiwa na umri tofauti tofauti.  Hivyo sio lazima kubatizwa ukiwa na umri kama wa Yesu bali awe mtu mwenye uwezo wa kuijua sheria.

NANI AKUBATIZE
Katika biblia waliobatizawalikuwa ni wanafunzi wa Yesu, na si wa musa mfano: Wasabato ni wanafunzi wa Musa na si wa Yesu. Kama ulibatizwa katika kanisa ambalo si la watu waliookoka maana yake ulibatizwa na mtu ambaye sio mwanafunzi wa Yesu. Hivyo huo haukuwa ubatizo wa kibiblia. Ubatizo wa kibiblia hufanywa na mwanafunzi wa Yesu na si  vinginevyo.

UWEZEKANO WA KUBATIZWA MARA MBILI AU ZAIDI
Ubatizo wa kibiblia unafanya mara moja tu, hivyo kama ulishawahi kubatizwa ubatizo wa kibiblia unafanyika mara moja tu. Lakini kuna mtu alibatizwa kabla ya kuamini, kibiblia hujawahi kubatizwa na ukibatizwa unakuwa ni mara ya kwanza. Mfano ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga au ulibatizwa na mtu ambaye si mwanafunzi wa Yesu ule haukuwa ubatizo, lakini ukibatizwa sasa unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza.

Unapoamiua kubatizwa leo unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza kwasababu hakuna ubatizo kwa mtu ambaye alikuwa hajaokoka bado, hajaamini au alikuwa bado mtoto.

MAANA YA KIROHO YA UBATIZO
Ø  Ni kufa, kuzikwa na kufufuka pamoja na Bwana Yesu Wakolosai 2:12; hivyo katika ubatizo tunazikwa na kufufuliwa pamoja na Yesu Kristo.
Ø  Ni kutimiza haki yote; Na ndio maana Yesu alikuwa Mungu lakini alipokuja duniani alikwenda kubatizwa, hakustahiri kubatizwa lakini alibatizwa ili awe kielelezo kwetu. Ili sisi tumfuate yeye, unapokuwa umebatizwa unakuwa umetimiza haki yote ila kama hujabatizwa utakuwa hujatimiza haki yote
Ø  Ni ishara ya kumkiri Yesu hadharani. Kuna tofauti kati ya kumwamini na kumkiri Yesu Yohana 12:41-42. Lakini unapobatizwa ni kumkiri Yesu kuwa BWANA na mwokozi.

Maswali
Utajiuliza mbona yule mwizi msalabani alimwamini Yesu akaenda mbinguni bila kubatizwa?. Jambo la kujiuliza hapa je wewe upo msalabani, na haujapata nafasi ya kubatizwa?, Yule mwizi hakupata nafasi ya kubatizwa ndio maana alienda mbinguni lakini kwasasa una nafasi ya kubatizwa unatakiwa ubatizwe kibiblia.

Ukibatizwa lazima ubadilishe jina?
Kimsingi kuna majina ambayo ni lazima  ubadili mfano, tabu, makoye, sikuzani n.k lakini kama jina lako lina maana nzuri hakuna haja ya kubali jina. Na ndio maana katika biblia watu wa Mungu wengi walibadilishiwa majina yao.

Saturday, December 29, 2012

UFUFUO NA UZIMA KUITEKA DAR ES SALAAM KWA MOTO WA MUNGU MWAKA 2013


Na mwandisi wetu.

Sehemu ya Maelfu wa Washirika wa Ufufuo na Uzima
wakiwa Tanganyika Packers ibadani
(Majeshi ya BWANA)
Mwaka mpya wa 2013 Dar es Salaam itatekwa na moto wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida ambapo maelfu na maelfu ya roho za watu zitavunwa kumwelekea Mungu kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya moto wa Mungu hapa jijini.

Akitoa sehemu ya salamu za mwaka mpya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mch. Josephat Gwajima alisema hayo leo tarehe 29 Disemba 2012 alipokuwa akifundisha kundi kubwa la viongozi wa  wapatao elfu 10,000 wa kanisa hilo lenye washirika zaidi ya 70,000.

Mchungaji kiongozi alisema kuwa ameamua kusitisha mikutano yote ya Injili ya nje ya nchi kwa mwaka 2013 isipokuwa mikutano miwili itakayofanyika China na Marekani. Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam litaanza rasmi mikutano ya injili itakayofanyika nchi nzima kwa mwaka 2013 ambapo maefu ya watu wanatarajiwa kuokoka, kuipa dunia kisogo, kuacha dhambi na kuwa watoto wa Mungu.

Mkutano wa kwanza wa Ufufuo na Uzima unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Biafra kwa muda wa juma moja mpaka majuma matatu mwaka 2013. Mikutano itakayofuata itafanyika katika wilaya zote za Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga (Temeke), Biafra (Kinondoni) na Kidongo chekundu (Ilala).

Sunday, December 23, 2012

KUMTUMIKIA BWANA 23.12.2012
Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima.

Kuna swali ambalo kama mtu uliyeokoka unatakiwa ujiulize kila siku, yaani “kama ikitokea leo umekufa una kitu gani cha kumwonyesha Mungu?” ukisoma Danieli 12:3 inaeleza kuwa, Wale Waliowaongoza wengi kutenda mema watang’aa kama nyota siku ya mwisho.  Hawa ni watu wanaomtumikia Mungu, kumbe siku ya mwisho tutarudi mbinguni kila mtu atatoa hesabu yake. Lakini kama ulimtumikia Mungu duniani, utang’aa kama nyota. 


MAMBO AMBAYO UTAYAPATA KWA KUMTUMIKIA MUNGU:

Pamoja na hayo hapa duniani, kuna vitu havipatikani kwa kuomba lakini vinapatikana kwa kumtumikia Mungu. Kuna mambo ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Tuangalie mambo 11 ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Kutoka 23:25


 1. Atabariki chakula chako:- hapa hata kama utakula chakula chenye sumu, hauwezi kudhurika kwasababu unamtumikia Mungu.
 2. Atabariki maji yako:- vilevile atabariki maji yako, yaani hayatakudhuru.
 3. Nitakuondolea magonjwa kati yako:- ukimtumikia Mungu, huwezi kuingia katika magonjwa yaani kama ulikuwa unaumwa Mungu atakuponya kwa vile unamtumikia Mungu.
 4. Hautakuwa mwenye kuharibu mimba:- Kuharibu mimba maana yake unaanza kitu, lakini kabla hakijafanikiwa kinaharibika. Inaweza ikawa mimba au hata kampuni.
 5. Kutokuwa tasa:- kama unamtumikia Mungu hata kama una miaka mingi unaweza kuzaa. Alikuwepo Sara ambaye alizaa akiwa na miaka 90 pamoja yakuwa umri ulikuwa umeendelea sana.
 6. Mungu atatimiza hesabu za siku zako:- unapomtumikia Mungu, atakupa miaka mingi ya kumtumikia Mungu, yaani kwasababu unafanya kazi yake duniani Mungu anakuongezea miaka ili umtumikie vizuri. Maana hata Mfalme Hezekia alipoumwa alimkumbusha Mungu jinsi alivyomtumikia Mungu, na Mungu akamwongezea miaka kumi na tano asingeweza kupata kwa maombi tu bali ni kwa kumtumikia Mungu.
 7. Mungu atatuma utiisho wake ukutangulie:- yaani huu ni uungu wa Mungu juu ya maisha ya mtu.
 8. Mungu atawafadhaisha wale watakaokufikiria.
 9. Mungu atawafanya adui zako wakuonyeshe maungo yao.
 10. Mungu atatuma mavu mbele ya adui zako wote.
 11. Mungu atawafukuza aduiazako wote.


Katika biblia watu waliomtumikia Mungu, Mungu aliwaheshimu.  Mwanzo 41:41, Yusufu alipata nafasi ya kuwa waziri mkuu kwenye nchi ya ugeni. Hii ni kwasababu Yusufu alimtumikia Mungu, akapewa kuheshimiwa na Mfalme wa Misri. Kila anayemtumikia Mungu, Mungu humueshimu mtu huyo.


UWEZEKANO WA KUMTUMIKIA MUNGU UKIWA NA KAZI YAKO:
Unaweza ukamtumikia Mungu huku ukiwa na nafasi katika uongozi au unafanya kazi nyingine yoyote. Alianza kuwa kama mbunge ingekuwa siku zetu lakini pamoja na huo uongozi aliweza kumtumikia Mungu.  Danieli 2:48; kwa habari ya Danieli tunagundua kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu huku ukiendelea na kazi yake. Kumbe kumtumikia Mungu Danieli 5:25-29; unaweza kumtumikia Mungu katika kiwango cha juu na bado ukafanya kazi zako za kawaida kama Danieli. Danieli 6:48:- hata kipindi cha Mfalme Koreshi, Danieli aliendelea kustawi, kwasababu alimtumikia Mungu.


Danieli 2:49 Hata Shadraka, Meshaki na Abednego pamoja na kuitumikia nchi, waliendelea kufanya kazi ya BWANA. Unaweza ukajiuliza kuwa ninawezaje kumtumikia Mungu huku ninabanwa na kazi, lakini kumbe Biblia inatupa ushahidi kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu. Na ndio maana hata Joshua ingawa alikuwa anamtumikia Mungu na wakati huohuo akiwa mpelelezi, Hesabu 13:6; Joshua alikuwa mpelelezi na katika kazi yake ya upelelezi aliifanya vizuri na kuleta ripoti nzuri, kinyume cha wapelelezi wengine ambao walileta ripoti mbaya Hesabu 14:19.

Kwenye Biblia hata polisi walimtumikia Mungu. Esta 3:1-6 Modekai alikuwa anafanya kazi katika nyumba ya mfalme yaani alikuwa anakaa kwenye lango la mfalme. Kumbe kuna uwezekano wa kuwa polisi na huku unamtumikia Mungu. Uwezekano huo upo.


Pia katika biblia; kulikuwa na mawakili waliomtumikia BWANA. Luka 8:3 “Yohana mkewe Kuza wakili wa Herode” yaani katika maisha ya leo huyu angeitwa mwanasheria mkuu, pamoja na kufanya kazi ya sheria na bado ukamtumikia BWANA. Kuwa mwanasheria hakumzuii mtu kumtumikia BWANA.


Matendo ya Mitume 17:4 “na wanawake wenye vyeo si wachache.” Neno hili linaonyesha kuwa hawakuwa wachache, kumbe unaweza kumtumikia BWANA na huku ukiwa na cheo chako kilekile. Yaani, unafanyakazi ya kumtumikia kwa uaminifu na huku unafanyakazi kwa uaminifu pia.


Matendo ya Mitume 16:14-15 Alikuwepo mwanamke huyu aliyeitwa Lidia ambaye alikuwa akiuza nguo za zambarau; kumbe unaweza kumtumikia Mungu na huku ukiwa mfanyabiashara. Siku ukiwa mbinguni huwezi kuonyesha biashara ulizofanya duniani, bali utamwonyesha kazi uliyofanya katika kumtumikia Mungu. Kuwa mfanya biashara sio sababu ya kukufanya ushindwe kumtumikia Mungu.


Yeremia 36:32; Baruku alikuwa mwandishi wa habari na huku alimtumikia Mungu yaani ndiye aliyekuwa anaandika mambo ambayo Yeremia alikuwa anayanena. Ilifikia kipindi hadi watu wanashangaa jinsi alivyokuwa anaandika. Yeremia 16:17; Yeremia 36:27; Katika biblia waandishi wa habari walikuwepo pia, Yeremia 36:10, kumbe unaweza kuwa mwandishi wa habari, huku unamtumikia Mungu.


Kutoka 1:38 kwenye biblia walikuwepo wakunga ; waliokuwa wakimtumikia BWANA; kumbe unaweza kuwa mzalishaji lakini unamtumika Mungu. Hata kama unafanya kazi za hospitali na bado ukaweza kumtumikia Mungu, Biblia inasema Mungu aliwatendea mema kwasababu ya kazi yao ya kuzalisha watoto kwa uaminifu.


Matendo ya Mitume 18:1-4. Paulo pamoja na nyaraka zake zote na kumtumikia Mungu lakini bado alikuwa anashona mahema kama kazi aliyofanya muda wa ziada. Kwahiyo kumbe, waweza kufanya kazi yako huku ukimtumikia Mungu kwa hiyo. Na ndio maana katika Biblia kulikuwa na msomi aliyeitwa Apolo, Matendo ya mitume 18:24-28. Kumbe pamoja na kusoma kwako waweza kumtumikia Mungu pia. Matendo ya mitume 26:24-25; kumbe hata Paulo alikuwa amesoma sana. Na ndio maana Paulo ndiye aliyeandika asilimia kubwa ya vitabu vya Biblia pamoja na roho mtakatifu pia alikuwa amesoma na alikuwa na kazi anayofanya.
FANYA UAMUZI SAHIHI KUMTUMIKIA MUNGU:

Baada ya Kujifunza mambo hayo ni uamuzi wako kuchagua unataka kumtumikia nani, ukichagua kumtumikia Yesu unakuwa umechagua hizi Baraka zote 11 za kumtumikia Mungu. Yoshua alisema “chagueni hivi lleo mtakayemtumikia, lakini mimi na nyumba yangu nitamtumikia Mungu.” amua kumtumikia Mungu ili uzishiriki baraka zote zilizotajwa.....


Mungu akubariki katika Jina la Yesu Kristo...

Sunday, December 16, 2012

Ujumbe: Vita Vya Wakati Wa Mwisho 16.12.2012

Ibada ya Jumapili: Matukio katika Picha, Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church (Ufufuo na Uzima), Josephat Gwajima akifundisha kuhusu Vita ya Wakati wa Mwisho. 
Sunday, December 9, 2012

MTU WA IMANI 9.12.2012

Na Mch. MWANGASA (Resident Pastor)


Warumi 4:13; Ibrahimu ALiitwa na Mungu kutoka nchi aliyokuwepo (Uru ya wakaldayo), Mungu akamuahidi kuwa atakuwa baba wa mataifa (uzao wake kama mchanga wa bahari). Lakini ikapita miaka bila Ibarahimu kupata mtoto, na kwa hali ya kawaida angeweza kukata tamaa. Kupitia habari hii, tunajifunza mambo matatu:-
1    
 •      Ibrahimu hakuangalia udhaifu wa kutokuzaa bali aliangalia Ahadi ya Mungu.
Kuna wakati wa kuangalia jambo ambalo Mungu amekuahidia. Neno la Mungu ni ahadi za Mungu kwetu. Na ndio maana alipoona uzee na hata tumbo la Sara mkewe. 19-20’ “Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;” 

 •          Pamoja na jambo hilo, Ibrahimu pia aliangalia uweza wa Mungu.

Kuna wakati mwingine majina ya vitu yanaweza kukutisha, aidha kwa kuangalia       desturi au asili. Kama Ibrahimu angeangalia desturi asingetarajia kupata mtoto katika wakati ule. Katika Mstari 21’  huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.Ibrahimu aliangalia uweza wa Mungu anayemwamini. 


Mtu wa Imani huwa anaangalia anapokwenda, na sio anapotoka. Warumi 4:17 “(kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.”  Mungu anayataja mambo ambayo hayapo, yaani yajayo kama yapo nah ii ndio tafsiri ya Imani. Na ndio maana; ingawa Mungu haonekani kwa macho lakini hilo halimfanyi asiwepo. Mtu mwenye Imani aangalii yanayoonekana bali yasiyoonekana. Mtu mwenye Imani hata kama ameambiwa kuwa ni tasa yeye anakwenda kununua kitanda cha mtoto. Hama kutoka katika kuangalia yaliyopo bali angalia kwa kufuata imani.

 •    Ibarahimu aliamini kwa kutarajia, lisiloweza kutarajiwa.
Warumi 4:18 “Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”  Usiogope kutarajia makubwa, Mungu anaweza kutenda yaliyo makuu mno. Kuna hazina zipo gizani ambazo imani pekee ndio inaaweza kuzichukua. Ibrahamu kilichomfanaya atarajie yaliyo makubwa Ni kwasababu aliiangalia ahadi ya BWANA. Hata sisi hatujaletwa duniani kwa hasara. Mungu anakusudi la sisi kuwepo hapa duniani.

Yawezekana unapita katika wakati mgumu, lakini unachotakiwa ujue ni kwamba, Mungu anaweza kutenda kwako ambayo watu wengi hawayatarajii. Swali la kujiuliza.. “Unatarajia jambo gani?”  Tafakari na uchague kuwa mtu wa Imani: ili uweze kuwa mtu wa imani jifunze kuangalia kwanza uweza wa Mungu kabla ya uweza wako mwenyewe.

Miliki Milango yote ya Baraka maana sisi ni wa Uzao wa Ibrahimu: Mwanzo 13:14 “Bwana akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.”  Miliki ahadi ya Mungu kwetu…Pamoja na Ibada nzuri; kulikuwa na Uzinduzi wa Album mpya ya Mwimbaji Peter (Mp)