Monday, December 31, 2012

NITAPITA KATIKATI YAO 2013

Na Mwandishi wetu.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Rev.Josephat Gwajima ameutangaza mwaka 2013 kuwa mwaka wa kupita katikati ya adui zetu. Akitangaza hayo katika Mkesha wa Mwaka mpya kanisani hapo Mchungaji alisema kuwa "Mwaka huu ni mwaka wa Kupita Katikati Yao" 

Ufunuo huu wa kupita katikati yao unatoka katika kitabu cha Luka 4:30 imeandikwa "Lakini Yeye (Yesu) alipita katikati yao, akaenda zake."  Yesu alipita katikati ya adui zake nao hawakuweza kumdhuru. Mchungaji alisisitiza kuwa kwa kawaida ukilikwepa jaribu utalikuta mbele, unatakiwa kupita katikati yake. Majaribu yapo namna hiyo. Pita katikati, neema imeachiliwa tayari. 

Mishumaa ikiwashwa kwa  moto kutokea madhabahuni
Mchungaji Kiongozi aliyasema hayo katika ibada ya Mkesha ambapo maelfu ya watu walikuwapo kanisani hapo wakimshukuru Mungu kwa neema ya kuingia mwaka 2013 salama. Katika ibada hiyo, ilipotimia saa 6 kamili usiku, taa zote zilizimwa na mishumaa mingi  iliyonyanyuliwa juu na kila mtu aliyekuwepo ibadani hapo iliwashwa kwa moto wa mshumaa ulioanzia madhabahuni ikiwa ni ishara kuwa moto wa madhabahuni utawaka mwaka wote 2013 kwa kila mmoja na hautazimika. 

Wachungaji wakazi (Resident Pastors) wakiomba kwa ajili ya maombi 10 ambayo kila mshirika aliandika ya kwake ili Mungu amtendee kwa mwaka 2013


Sunday, December 30, 2012

UBATIZO WA KIBIBLIA KUFANYIKA TAREHE 1 JANUARI 2013


Na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima

Kila mtu aliyeokoka ni askari wa jeshi la Yesu, hivyo kama askari wa Yesu tunatakiwa kufuata kile ambacho Mungu anatuagiza, 1Timotheo 2:4; sisi ni wanajeshi wa jeshi la BWANA, Filemoni 1:2; Hivyo mkristo mwenzako aliyeokoka ni askari mwenzako.  Ndio maana katika biblia kila mahali Mungu alipojitambulisha alitumia jina la BWANA wa Majeshi. 1Samwel 15:2; 2Samweli 7:8. Utajiuliza majeshi haya ni yapi; haya ni majeshi ya Yesu ambayo ndio sisi tuliookoka. Mambo ya Nyakati17:7; Isaya 1:24;3:15; 10:24; 14:13;

Mara tu unapookolewa Yesu ambaye ni Bwana wa majeshi anatuagiza kutii amri yake.  Malaki 3:17; 4:3;  Mathayo 28:18-19, hapa BWANA wa majeshi anatoa Amri ya kuifuata. Kumbe kuwabatiza watu ni amri ya BWANA wa majeshi, hivyo tuna jukumu la kutii amri ya Yesu Kristo. Na unapookolewa Mungu anakutarajia utii amri ya mkuu wa majeshi Yesu Kristo.

MAANA YA NENO UBATIZO
Neno “ubatizo” linatokana na neno la kigiriki linaitwa “babto” au zamisha; hili neno Babto limetumika mara nyingi sana katika biblia Yohana 13:26.  Yesu alisema ambaye nitachovya naye tonge ndiye atakaye nisaliti” kumbe kuzamisha tonge katika mboga ndio mana rahisi ya kubatiza yaani chovya au kuzamisha. Kwahiyo kutokana na maana ya neno ubatizo tunaweza kujua kuwa ili mtu abatizwe anatakiwa awe kwenye maji tele.

UBATIZO WA KIBIBLIA
Yohana 3:23; kwa maana hiyo ya ubatizo ndio maana tunaona Yohana alibatiza mahali penye maji tele. Huwezi kuzamisha mtu ndani ya bakuli au birika, ni lazima maji yawe tele ili mtu aweze kuzama. Hivyo ubatizo wa kibiblia ni wa kumzamisha mtu ndani ya maji.  Na ndio maana katika kitabu cha Matendo ya mitume 8:26; hivyo ubatizo wa Kibiblia wote wawili hutelemka majini, hapo unaweza ukajiuliza je ulipobatizwa wote wawili mlitelemka majini? Kama sivyo basi ujue haukuwa ubatizo wa Kibiblia.
Na jambo lingine la kuangalia huyu towashi alihubiriwa, akaamini na kubatizwa. Unaweza ukalinganisha kama ulipobatizwa uliamini kwanza na je wote mliingia majini, na ndio maana mstari wa 29” unasema “kisha walipopanda kutoka majini” kumbe ubatizo wa kibiblia hutelemka majini na kupanda kutoka majini.

KWANINI WATU WANABATIZA NDANI YA BAKULI AU BIRIKA
Watu wengi wanayapindisha maandiko, lakini biblia inatuagiza kutumia neno la Mungu kwa halali, 2Timotheo 2:15. Na ndio maana utaona watu leo wanatumia maandiko vibaya kuwabatiza watu katika bakuli, bila kutelemka majini. Haya ndio maandiko ambayo watu huyatumia kupindisha ukweli, Hesabu 8:5-7; Mungu alimwambia Musa anyunyize maji ya utakaso, lakini huu si ubatizo bali ni utakaso. Na watu wengi waliokuwa wamefanyiwa hivi ni wale waliokuwa wameshika maiti, ilikuwa mtu ashikapo maiti anakuwa najisi mpaka amwagiwe maji ya farakano. Kimsingi huu haukuwa ubatizo wa kibiblia, bali ulikuwa utakaso tu na si ubatizo wa kibiblia.

MTU YUPI ANAYETAKIWA KUBATIZWA
Huyu ni mtu aliyetubu dhambi, kama hujatubu dhambi ubatizo wako si wa kibiblia. Matendo ya Mitume 2:37, hivyo kanuni ya Mungu ni kwamba mtu anatubu kwanza ndipo anabatizwa, lakini maeneo mengi watu hubatizwa wakiwa watoto wachanga ambao hawawezi kutubu. Hivyo kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo sio ubatizo wa kibiblia. Marko 16:15-16, Na ndio maana Yesu aliagiza kwa kusema aaminiye na kubatizwa, kumbe kinachoanza ni kuamini alafu unabatizwa.

Tumeona mambo kadhaa yanayoendana na ubatizo wa kibiblia, yaani unatubu kwanza, ndipo unabatizwa. Matendo ya Mitume 8:12, Biblia inaendelea kusema kuwa wakaamini wakabatizwa, huwezi kusema umebatizwa kama hujaamini bado. Matendo ya Mitume 8:35-38, katika biblia hakuna aliyebatizwa bila kuamini kwanza, na ndio maana Filipo alimwambia Yule towashi kwa habari ya ubatizo “ukiamini inawezekana” kumbe ubatizo wa kibiblia unaamini kwanza ndipo inawezekana kubatizwa. Ni swali la kujiuliza kuwa ulipobatizwa uliamini kwanza.  Matendo ya mitume 19:1-…

UBATIZO UNAWEZWA KUFANYWA KWA MTOTO MCHANGA
Mtoto mdogo hawezi kuamini, na kwa maana hiyo hawezi hata kutubu dhambi zake. Mama au baba wa ubatizo hawezi kutubu kwa niaba ya mtoto, huu ni usanii na si ukweli kabisa. Mtu anatakiwa asikie mwenyewe na atubu mwenyewe pasipo kujibiwa na mtu. Kwahiyo jibu la swali hili kuhusu ubatizo kwa watoto wadogo ni kwamba hakuna ubatizo kwa watoto wadogo, kwasababu hawezi kuamini, na pia ukimzamisha mtoto katika maji unaweza ukamuua.

Kwa maana hiyo; kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo haukuwa ubatizo. Na hata ukiamua kubatizwa ubatizo wa KIBIBLIA sio kwamba unabatizwa kwa mara ya pili bali ni mara ya kwanza, ule wa kwanza haukuwa ubatizo. Katika biblia mama au baba awezi kumuaminia mwanaye imeandikwa,Ezekieli 18:20. Kuwa baba hawezi kuchukua uovu wa mwanaye. Hata hivyo dhambi ya mtoto haihesabiwi kwasababu akili yake haijaweza kuitambua sheria bado, hivyo dhambi inaweza kuwepo lakini haijaanza kuhesabiwa kwasababu hawaijui sheria bado.

Kwa asili, mtoto anakuwa amezaliwa na asili ya dhambi, lakini haihesabiwi, Warumi 5:12-13 kumbe dhambi haisebawi kwa mtoto kwasababu haijui sheria na wala haijawa wazi kwake. Warumi 4:15. Matendo 2:38; Biblia inasema kwa siku moja walibatizwa wakiwa na umri tofauti tofauti.  Hivyo sio lazima kubatizwa ukiwa na umri kama wa Yesu bali awe mtu mwenye uwezo wa kuijua sheria.

NANI AKUBATIZE
Katika biblia waliobatizawalikuwa ni wanafunzi wa Yesu, na si wa musa mfano: Wasabato ni wanafunzi wa Musa na si wa Yesu. Kama ulibatizwa katika kanisa ambalo si la watu waliookoka maana yake ulibatizwa na mtu ambaye sio mwanafunzi wa Yesu. Hivyo huo haukuwa ubatizo wa kibiblia. Ubatizo wa kibiblia hufanywa na mwanafunzi wa Yesu na si  vinginevyo.

UWEZEKANO WA KUBATIZWA MARA MBILI AU ZAIDI
Ubatizo wa kibiblia unafanya mara moja tu, hivyo kama ulishawahi kubatizwa ubatizo wa kibiblia unafanyika mara moja tu. Lakini kuna mtu alibatizwa kabla ya kuamini, kibiblia hujawahi kubatizwa na ukibatizwa unakuwa ni mara ya kwanza. Mfano ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga au ulibatizwa na mtu ambaye si mwanafunzi wa Yesu ule haukuwa ubatizo, lakini ukibatizwa sasa unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza.

Unapoamiua kubatizwa leo unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza kwasababu hakuna ubatizo kwa mtu ambaye alikuwa hajaokoka bado, hajaamini au alikuwa bado mtoto.

MAANA YA KIROHO YA UBATIZO
Ø  Ni kufa, kuzikwa na kufufuka pamoja na Bwana Yesu Wakolosai 2:12; hivyo katika ubatizo tunazikwa na kufufuliwa pamoja na Yesu Kristo.
Ø  Ni kutimiza haki yote; Na ndio maana Yesu alikuwa Mungu lakini alipokuja duniani alikwenda kubatizwa, hakustahiri kubatizwa lakini alibatizwa ili awe kielelezo kwetu. Ili sisi tumfuate yeye, unapokuwa umebatizwa unakuwa umetimiza haki yote ila kama hujabatizwa utakuwa hujatimiza haki yote
Ø  Ni ishara ya kumkiri Yesu hadharani. Kuna tofauti kati ya kumwamini na kumkiri Yesu Yohana 12:41-42. Lakini unapobatizwa ni kumkiri Yesu kuwa BWANA na mwokozi.

Maswali
Utajiuliza mbona yule mwizi msalabani alimwamini Yesu akaenda mbinguni bila kubatizwa?. Jambo la kujiuliza hapa je wewe upo msalabani, na haujapata nafasi ya kubatizwa?, Yule mwizi hakupata nafasi ya kubatizwa ndio maana alienda mbinguni lakini kwasasa una nafasi ya kubatizwa unatakiwa ubatizwe kibiblia.

Ukibatizwa lazima ubadilishe jina?
Kimsingi kuna majina ambayo ni lazima  ubadili mfano, tabu, makoye, sikuzani n.k lakini kama jina lako lina maana nzuri hakuna haja ya kubali jina. Na ndio maana katika biblia watu wa Mungu wengi walibadilishiwa majina yao.

Saturday, December 29, 2012

UFUFUO NA UZIMA KUITEKA DAR ES SALAAM KWA MOTO WA MUNGU MWAKA 2013


Na mwandisi wetu.

Sehemu ya Maelfu wa Washirika wa Ufufuo na Uzima
wakiwa Tanganyika Packers ibadani
(Majeshi ya BWANA)
Mwaka mpya wa 2013 Dar es Salaam itatekwa na moto wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida ambapo maelfu na maelfu ya roho za watu zitavunwa kumwelekea Mungu kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya moto wa Mungu hapa jijini.

Akitoa sehemu ya salamu za mwaka mpya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mch. Josephat Gwajima alisema hayo leo tarehe 29 Disemba 2012 alipokuwa akifundisha kundi kubwa la viongozi wa  wapatao elfu 10,000 wa kanisa hilo lenye washirika zaidi ya 70,000.

Mchungaji kiongozi alisema kuwa ameamua kusitisha mikutano yote ya Injili ya nje ya nchi kwa mwaka 2013 isipokuwa mikutano miwili itakayofanyika China na Marekani. Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam litaanza rasmi mikutano ya injili itakayofanyika nchi nzima kwa mwaka 2013 ambapo maefu ya watu wanatarajiwa kuokoka, kuipa dunia kisogo, kuacha dhambi na kuwa watoto wa Mungu.

Mkutano wa kwanza wa Ufufuo na Uzima unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Biafra kwa muda wa juma moja mpaka majuma matatu mwaka 2013. Mikutano itakayofuata itafanyika katika wilaya zote za Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga (Temeke), Biafra (Kinondoni) na Kidongo chekundu (Ilala).

Sunday, December 23, 2012

KUMTUMIKIA BWANA 23.12.2012
Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima.

Kuna swali ambalo kama mtu uliyeokoka unatakiwa ujiulize kila siku, yaani “kama ikitokea leo umekufa una kitu gani cha kumwonyesha Mungu?” ukisoma Danieli 12:3 inaeleza kuwa, Wale Waliowaongoza wengi kutenda mema watang’aa kama nyota siku ya mwisho.  Hawa ni watu wanaomtumikia Mungu, kumbe siku ya mwisho tutarudi mbinguni kila mtu atatoa hesabu yake. Lakini kama ulimtumikia Mungu duniani, utang’aa kama nyota. 


MAMBO AMBAYO UTAYAPATA KWA KUMTUMIKIA MUNGU:

Pamoja na hayo hapa duniani, kuna vitu havipatikani kwa kuomba lakini vinapatikana kwa kumtumikia Mungu. Kuna mambo ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Tuangalie mambo 11 ambayo huwezi kuyapata popote mpaka umemtumikia Mungu. Kutoka 23:25


 1. Atabariki chakula chako:- hapa hata kama utakula chakula chenye sumu, hauwezi kudhurika kwasababu unamtumikia Mungu.
 2. Atabariki maji yako:- vilevile atabariki maji yako, yaani hayatakudhuru.
 3. Nitakuondolea magonjwa kati yako:- ukimtumikia Mungu, huwezi kuingia katika magonjwa yaani kama ulikuwa unaumwa Mungu atakuponya kwa vile unamtumikia Mungu.
 4. Hautakuwa mwenye kuharibu mimba:- Kuharibu mimba maana yake unaanza kitu, lakini kabla hakijafanikiwa kinaharibika. Inaweza ikawa mimba au hata kampuni.
 5. Kutokuwa tasa:- kama unamtumikia Mungu hata kama una miaka mingi unaweza kuzaa. Alikuwepo Sara ambaye alizaa akiwa na miaka 90 pamoja yakuwa umri ulikuwa umeendelea sana.
 6. Mungu atatimiza hesabu za siku zako:- unapomtumikia Mungu, atakupa miaka mingi ya kumtumikia Mungu, yaani kwasababu unafanya kazi yake duniani Mungu anakuongezea miaka ili umtumikie vizuri. Maana hata Mfalme Hezekia alipoumwa alimkumbusha Mungu jinsi alivyomtumikia Mungu, na Mungu akamwongezea miaka kumi na tano asingeweza kupata kwa maombi tu bali ni kwa kumtumikia Mungu.
 7. Mungu atatuma utiisho wake ukutangulie:- yaani huu ni uungu wa Mungu juu ya maisha ya mtu.
 8. Mungu atawafadhaisha wale watakaokufikiria.
 9. Mungu atawafanya adui zako wakuonyeshe maungo yao.
 10. Mungu atatuma mavu mbele ya adui zako wote.
 11. Mungu atawafukuza aduiazako wote.


Katika biblia watu waliomtumikia Mungu, Mungu aliwaheshimu.  Mwanzo 41:41, Yusufu alipata nafasi ya kuwa waziri mkuu kwenye nchi ya ugeni. Hii ni kwasababu Yusufu alimtumikia Mungu, akapewa kuheshimiwa na Mfalme wa Misri. Kila anayemtumikia Mungu, Mungu humueshimu mtu huyo.


UWEZEKANO WA KUMTUMIKIA MUNGU UKIWA NA KAZI YAKO:
Unaweza ukamtumikia Mungu huku ukiwa na nafasi katika uongozi au unafanya kazi nyingine yoyote. Alianza kuwa kama mbunge ingekuwa siku zetu lakini pamoja na huo uongozi aliweza kumtumikia Mungu.  Danieli 2:48; kwa habari ya Danieli tunagundua kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu huku ukiendelea na kazi yake. Kumbe kumtumikia Mungu Danieli 5:25-29; unaweza kumtumikia Mungu katika kiwango cha juu na bado ukafanya kazi zako za kawaida kama Danieli. Danieli 6:48:- hata kipindi cha Mfalme Koreshi, Danieli aliendelea kustawi, kwasababu alimtumikia Mungu.


Danieli 2:49 Hata Shadraka, Meshaki na Abednego pamoja na kuitumikia nchi, waliendelea kufanya kazi ya BWANA. Unaweza ukajiuliza kuwa ninawezaje kumtumikia Mungu huku ninabanwa na kazi, lakini kumbe Biblia inatupa ushahidi kuwa kuna uwezekano wa kumtumikia Mungu. Na ndio maana hata Joshua ingawa alikuwa anamtumikia Mungu na wakati huohuo akiwa mpelelezi, Hesabu 13:6; Joshua alikuwa mpelelezi na katika kazi yake ya upelelezi aliifanya vizuri na kuleta ripoti nzuri, kinyume cha wapelelezi wengine ambao walileta ripoti mbaya Hesabu 14:19.

Kwenye Biblia hata polisi walimtumikia Mungu. Esta 3:1-6 Modekai alikuwa anafanya kazi katika nyumba ya mfalme yaani alikuwa anakaa kwenye lango la mfalme. Kumbe kuna uwezekano wa kuwa polisi na huku unamtumikia Mungu. Uwezekano huo upo.


Pia katika biblia; kulikuwa na mawakili waliomtumikia BWANA. Luka 8:3 “Yohana mkewe Kuza wakili wa Herode” yaani katika maisha ya leo huyu angeitwa mwanasheria mkuu, pamoja na kufanya kazi ya sheria na bado ukamtumikia BWANA. Kuwa mwanasheria hakumzuii mtu kumtumikia BWANA.


Matendo ya Mitume 17:4 “na wanawake wenye vyeo si wachache.” Neno hili linaonyesha kuwa hawakuwa wachache, kumbe unaweza kumtumikia BWANA na huku ukiwa na cheo chako kilekile. Yaani, unafanyakazi ya kumtumikia kwa uaminifu na huku unafanyakazi kwa uaminifu pia.


Matendo ya Mitume 16:14-15 Alikuwepo mwanamke huyu aliyeitwa Lidia ambaye alikuwa akiuza nguo za zambarau; kumbe unaweza kumtumikia Mungu na huku ukiwa mfanyabiashara. Siku ukiwa mbinguni huwezi kuonyesha biashara ulizofanya duniani, bali utamwonyesha kazi uliyofanya katika kumtumikia Mungu. Kuwa mfanya biashara sio sababu ya kukufanya ushindwe kumtumikia Mungu.


Yeremia 36:32; Baruku alikuwa mwandishi wa habari na huku alimtumikia Mungu yaani ndiye aliyekuwa anaandika mambo ambayo Yeremia alikuwa anayanena. Ilifikia kipindi hadi watu wanashangaa jinsi alivyokuwa anaandika. Yeremia 16:17; Yeremia 36:27; Katika biblia waandishi wa habari walikuwepo pia, Yeremia 36:10, kumbe unaweza kuwa mwandishi wa habari, huku unamtumikia Mungu.


Kutoka 1:38 kwenye biblia walikuwepo wakunga ; waliokuwa wakimtumikia BWANA; kumbe unaweza kuwa mzalishaji lakini unamtumika Mungu. Hata kama unafanya kazi za hospitali na bado ukaweza kumtumikia Mungu, Biblia inasema Mungu aliwatendea mema kwasababu ya kazi yao ya kuzalisha watoto kwa uaminifu.


Matendo ya Mitume 18:1-4. Paulo pamoja na nyaraka zake zote na kumtumikia Mungu lakini bado alikuwa anashona mahema kama kazi aliyofanya muda wa ziada. Kwahiyo kumbe, waweza kufanya kazi yako huku ukimtumikia Mungu kwa hiyo. Na ndio maana katika Biblia kulikuwa na msomi aliyeitwa Apolo, Matendo ya mitume 18:24-28. Kumbe pamoja na kusoma kwako waweza kumtumikia Mungu pia. Matendo ya mitume 26:24-25; kumbe hata Paulo alikuwa amesoma sana. Na ndio maana Paulo ndiye aliyeandika asilimia kubwa ya vitabu vya Biblia pamoja na roho mtakatifu pia alikuwa amesoma na alikuwa na kazi anayofanya.
FANYA UAMUZI SAHIHI KUMTUMIKIA MUNGU:

Baada ya Kujifunza mambo hayo ni uamuzi wako kuchagua unataka kumtumikia nani, ukichagua kumtumikia Yesu unakuwa umechagua hizi Baraka zote 11 za kumtumikia Mungu. Yoshua alisema “chagueni hivi lleo mtakayemtumikia, lakini mimi na nyumba yangu nitamtumikia Mungu.” amua kumtumikia Mungu ili uzishiriki baraka zote zilizotajwa.....


Mungu akubariki katika Jina la Yesu Kristo...

Sunday, December 16, 2012

Ujumbe: Vita Vya Wakati Wa Mwisho 16.12.2012

Ibada ya Jumapili: Matukio katika Picha, Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church (Ufufuo na Uzima), Josephat Gwajima akifundisha kuhusu Vita ya Wakati wa Mwisho. 
Sunday, December 9, 2012

MTU WA IMANI 9.12.2012

Na Mch. MWANGASA (Resident Pastor)


Warumi 4:13; Ibrahimu ALiitwa na Mungu kutoka nchi aliyokuwepo (Uru ya wakaldayo), Mungu akamuahidi kuwa atakuwa baba wa mataifa (uzao wake kama mchanga wa bahari). Lakini ikapita miaka bila Ibarahimu kupata mtoto, na kwa hali ya kawaida angeweza kukata tamaa. Kupitia habari hii, tunajifunza mambo matatu:-
1    
 •      Ibrahimu hakuangalia udhaifu wa kutokuzaa bali aliangalia Ahadi ya Mungu.
Kuna wakati wa kuangalia jambo ambalo Mungu amekuahidia. Neno la Mungu ni ahadi za Mungu kwetu. Na ndio maana alipoona uzee na hata tumbo la Sara mkewe. 19-20’ “Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;” 

 •          Pamoja na jambo hilo, Ibrahimu pia aliangalia uweza wa Mungu.

Kuna wakati mwingine majina ya vitu yanaweza kukutisha, aidha kwa kuangalia       desturi au asili. Kama Ibrahimu angeangalia desturi asingetarajia kupata mtoto katika wakati ule. Katika Mstari 21’  huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.Ibrahimu aliangalia uweza wa Mungu anayemwamini. 


Mtu wa Imani huwa anaangalia anapokwenda, na sio anapotoka. Warumi 4:17 “(kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.”  Mungu anayataja mambo ambayo hayapo, yaani yajayo kama yapo nah ii ndio tafsiri ya Imani. Na ndio maana; ingawa Mungu haonekani kwa macho lakini hilo halimfanyi asiwepo. Mtu mwenye Imani aangalii yanayoonekana bali yasiyoonekana. Mtu mwenye Imani hata kama ameambiwa kuwa ni tasa yeye anakwenda kununua kitanda cha mtoto. Hama kutoka katika kuangalia yaliyopo bali angalia kwa kufuata imani.

 •    Ibarahimu aliamini kwa kutarajia, lisiloweza kutarajiwa.
Warumi 4:18 “Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”  Usiogope kutarajia makubwa, Mungu anaweza kutenda yaliyo makuu mno. Kuna hazina zipo gizani ambazo imani pekee ndio inaaweza kuzichukua. Ibrahamu kilichomfanaya atarajie yaliyo makubwa Ni kwasababu aliiangalia ahadi ya BWANA. Hata sisi hatujaletwa duniani kwa hasara. Mungu anakusudi la sisi kuwepo hapa duniani.

Yawezekana unapita katika wakati mgumu, lakini unachotakiwa ujue ni kwamba, Mungu anaweza kutenda kwako ambayo watu wengi hawayatarajii. Swali la kujiuliza.. “Unatarajia jambo gani?”  Tafakari na uchague kuwa mtu wa Imani: ili uweze kuwa mtu wa imani jifunze kuangalia kwanza uweza wa Mungu kabla ya uweza wako mwenyewe.

Miliki Milango yote ya Baraka maana sisi ni wa Uzao wa Ibrahimu: Mwanzo 13:14 “Bwana akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.”  Miliki ahadi ya Mungu kwetu…Pamoja na Ibada nzuri; kulikuwa na Uzinduzi wa Album mpya ya Mwimbaji Peter (Mp)Sunday, November 25, 2012

UWEZA WA MUNGU WETU


Na Mch. MWANGASA   25.11.2012
Mchungaji Mwangasa (Resident Pastor)

Danieli 3:1-30; 6:10-38;  tumesoma habari mbili ambazo zinawahusu kwa ukaribu watu wane yaani, Danieli, Meshaki, Shedraka na Abednego.  Kipindi kile Babeli walivamia Yerusalemu na kuwachukua waisraeli utumwani, na kati yao wakachukuliwa watu kadhaa kwenda kufanya kazi za mfalme, baadhi ya waliokuwepo ni hawa wane. Kupitia hao tunapata kujifunza:-


Habari ya Kwanza kuhusu Sanamu iliyowekwa na Mfalme Nebkadneza: (Danieli 3:1-30):

Mfalme Nebkadneza baada ya kuvamia wayaudi na kuwachukua utumwani, akatenga siku na kuwalazimisha watu wote waiabudu sanamu aliyoitengeneza. Mfalme akaandaa tanuru la moto ili yeyote atakae kiuka amri ya mfalme atupwe humo. Lakini Shedraka, Mashaki na Abednego hawakukubali kuinama kuiabudu sanamu.  Ndipo baadhi ya Wakaldayo wakapeleka mashtaka, tunaona hili katika mstari wa 8* “Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.” Hawa ndio waliopeleka mashtaka kwa Mfalme. Mfalme akakasirika akasema, moto na uongezwe mara saba. Kibiblia mara saba ni namba ya ukamilifu wa Mungu, ukianzia kwa habari ya ukuta wa Yeriko ulianguka siku ya saba hivyo, hawa wakina shedraki hawakushtuka kwasababu walijua ukamilifu wa utukufu wa Mungu umekaribia.

Jambo la ajabu likatokea pale mfalme alipowatupa kwenye moto, maana moto uliwalamba na kuwateketeza wale waliokwenda kuwatupa. Lakini wao (Shedraka, Meshaki na Abednego) hawakuungua, moto haukuwaweza kabisa. Jambo la muhimu kujifunza kupitia habari hii. Pata picha ya hali iliyokuwepo kwa hawa watu watatu, maana lilikuwa ni jambo gumu kwao. Wangetarajia Mungu awaokoe mapema yaani Mungu asingeruhusu watupwe kwenye moto, lakini kinyume na matarajio yao, Mungu akawaokoa dakika ya mwisho. Hapa tuna mambo kadhaa ya kujifunza :- 

Kwanza; Mungu alitaka atimize neno lake alilonena kupitia nabii Isaya, KWAMBA, “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.” Isaya 43:2, Mungu wetu ni moto ulao, na kwakulithibitisha hilo akaruhusu hadi wafikie dakika ya mwisho, ili ajichukulie utukufu wake.

Pili; Mungu huwa anaokoa dakika ya mwisho, pale unapohisi kuwa huna msaada mwingine ndipo Mungu anajichukulia utukufu; watu wengi wanakata tama mapema bila kujua kuwa Mungu huokoa katika saa ambayo hukuitarajia, Wakina Shedraka wangetarajia Mungu awaokoe katika hatua ya kwanza, lakini Mungu alikuja kwao dakika ya mwisho.

Tatu; tunaona watu walioenda kuwashtaki kwa Mfalme; hapa tunajifunza kuwa unapoishi kuna watu watasema, kuna watu watakupinga, kuna watu watakushtaki kwa waganga wa kienyeji wakitaka kukuangamiza. Lakini ni muhimu kujua kuwa Mungu wetu ni Mungu wa kuokoa. Unapookoka Mungu anakuwa pamoja na wewe.

Nne; ndani ya moto kulikuwa na mtu wane; Yesu Kristo yupo pamoja nasi, imeandikwa, “wa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu;” 1 Yohana 5:4, hakuna moto ambao umeanzishwa na wanadamu, utakaoweza kukushinda. Sisi tumezaliwa na Mungu, na lazima tuushinde ulimwengu. Ni kweli unaweza kuwa unapitia kunye tatizo ambalo limekuwa moto kwenye maisha yako, lakini jambo la muhimu kujua kwamba, Hakuna moto uliofanywa na wanadamu utakaoweza kukushinda, kwasababu maana baada ya kuokoka unakuwa umezaliwa na Mungu.


Habari ya pili kuhusu, Danieli na Mfalme Dario: (Danieli 6:10-28):

Katika kipindi cha Mfalme Dario, watu kadhaa wakaamua kwa hila kumuangamiza Danieli, na hawakuona jambo lolote la kumuangamiza isipokuwa kwa habari ya Mungu wake. Imeandikwa, “Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.” Hivyo, Mfalme akaweka muhuri kwenye sharia, lakini Danieli bila kujua ile sharia yeye akaendelea na Ibada kama kawaida; wakati huohuo, liliandaliwa ntanuru la samba ambao nao hawakupewa chakula kwa muda wa siku saba. Lakini cha ajabu kuwa walipomtupa ndani ya shimo wale samba hawakuweza kumdhuru. Ndipo mfalme akaamuru wale waliopangia hila watupwe wao. Ambapo samba waliwadaka hewani kabla ya kufika chini. Katika habari hii kuna mambop kadhaa ya kujifunza:-

Kwanza; Simba wakagoma kumla Danieli; biblia inasema, “Na kwa habari za malaika asema, Afanyaye malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto.” Waebrania 1:7.  Mungu anasema hutufanya sisi watumishi wake kuwa miale ya moto, n wale samba walimuona danieli kama mwali wa moto hivyo hawakuweza kumrarua. Unapookoka unakuwa mwali wa moto katika ulimwengu wa roho na hakuna silaha inayoweza kukudhuru.

Pili; Danieli alikuwa mtu wa kabila la Yuda na kwaabari ya Yuda kuna Simba wa kabila la Yuda, samba wasingeweza kumdhuru, kwa kuwa Danieli alikuwa pamoja na Mungu aliye simba wa kabila la Yuda. Hakuna haja ya kuogopa yale magumu unayopitia,. Kwa kuwa ndani yako kuna simba wa kabila la Yuda yaani Yesu Kristo. Pamoja na kukosa chakula kwa muda wa siku saba, hawakuweza kumla Danieli mtu wa Mungu.

Tatu; baada ya Mfalme kugundua kuwa samba wameshindwa kumuua Danieli, ndipo akaamuru wale waliotaka kumuua Danieli kwa hila waingize wao shimoni. Likatimia andiko kuwa, “Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake;  Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.” Mhubiri 10:8, wale waliokuandalia kifo au aibu kwa hila, itamrudia mwenyewe. Mungu huwaondoa wenye haki kwenye ajali na kuwaweka waovu badala yake.  Wanakupiga vita kwa hila usiangaike we mwangalie Mungu, yeye atakupigania.

Unapokuwa unaomba, inabidi ujue kuwa upo na Mungu awezaye kutenda kwa namna ya ajabu sana; Yoshua 10:9 “Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Bethhoroni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Bethhoroni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.” Mungu aliwahi kuwaangushia mawe, maadui wa Israeli, Unatakiwa ujue BWANA amewatia adui zako mikononi mwako uwatende unavyotaka. Unatakiwa ujue hauko peke yako Mungu yupo kwaajili yako, kukuokoa. Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa na njia za kutoka mautini zina yeye!!!

Glory Of Christ (T) Church
Ufufuo na Uzima
Dar es Salaam, Tanzania.

Sunday, November 18, 2012

UJUMBE: MIAKA YA MAISHA YETU


Na. Mch. Mwangasa (Resident Pastor)
Mchungaji Mwangasa (Resident Pastor) akihubiri kanisani
Ufufuo na Uzima, Dar es Salaam

Mwanzo 47:7-12
9* “Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.” Haya yalikuwa ni mazungumzo baina ya Yakobo na Farao baada ya Yusufu kwenda kumtambulisha babaye kwa Farao. Lakini kitu cha kushangaza Farao akamuuliza Yakobo, siku za maisha yako ni ngapi? Na hilo ndilo lilikuw jibu ya Yakobo kwa Farao.Jibu la Yakobo linatupa jambo muhimu la kujifunza, ukifuatilia maisha ya Yakobo utagundua kuwa ni kweli yalikuwa ya kusafiri sana, ukianzia tangu alipozaliwa, baadaye alimkimbia Essau na kwenda kwa Labani, haikutosha akarudi kupatana na Essau, bado taarifa za mauaji ya Yusufu nayo yalichangia kufanya maisha yake yawe ya tabu. Na ndio maana alipoulizwa na Yusufu siku za maisha yake ni ngapi, ikabidi atenge muda aliosafiri yeye na maisha yaliokuwa wameishi wazee wake yaani (Ibrahimu na Isaka).

Mch. Bihagaze akimkaribisha Mch. Mwangasa
madhabahuni
Tukitaka kufuatilia maisha ya Yakobo alipokuwa kwa Labani, tunaweza kufahamu kupitia andiko hili Mwanzo  31:38-41, haya ni maelezo ya Yakobo kwa Labani, baada ya Labani kumpekuwa kutokana na upotevu wa miungu yake. Ndio maana hapo Yakobo anasema alikuwa anafanya kazi mchana na usiku, alibadilishiwa mishahara mara kumi kwasababu kila hasara ililopatikana ilirudishwa kwa Yukobo. (Mwanzo 30:25-44) pamoja na yote hayo, bado Labani alimdhulumu Yakobo, hivyo maisha ya Yakobo yalikuwa yamejaa tabu na dhulumiwa.

Wakati Labani akiwa amevuruga makubaliano yale, Yakobo akamtazama Mungu, na hapa ndipo tunaona jambo la ajabu pale Yakobo alipoweka fito kwenye maji, na wale wanyama walipokunywa wakapata mimba. Hapa tunajifunza jambo kuwa hata kama wanadamu wamekudhulumu, Mungu anaweza kukusaidia nawe utaneemeka kuliko waliokudhulumu. Hili jambo lilitokea wakati Labani ametorosha madume yote ili Yakobo asipate uzao kwa wanyama wale. Ukiokoka unakuwa na Mungu, hakuna haja ya kusikitika kuwa umebaki peke yako, kuna Mungu ambaye hawezi kukuacha.

Maelfu ya Watu wakimwabudu Mungu Jumapili hii
Ufufuo na Uzima
Imeandikwa Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” Yohana 5:4. Ukiokoka Mungu anakuwa pamoja na wewe, yaani umezaliwa na Mungu, na kila kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Na hapa kwa Habari ya Yakobo, Mungu alikuwa anataka ile ahadi aliyomuahidi Ibrahimu itimie kwa Yakobo.

Inawezekana kwenye maisha yako, unaishi kama Yakobo, maisha yaliyojaa kusafiri ena huku ukipapasa papasa bila kujua unakoelekea. Inabidi ujue jambo hili kuwa ukimpata Mungu unakuwa umepata jibu la maisha yako. Imeandikwa, Utajiri na heshima ziko kwangu,  Naam, utajiri udumuo, na haki pia.” Mithali 8:18. Mtafute Mungu ndipo utakutana na Utajiri na Heshima. Wewe ndio unajua siku za miaka yako ni mingapi, unajua mambo gani magumu unayopitia, lakini Mungu anakuuliza siku za maisha yako ni ngapi.

Hata katika habari ya mwana mpotevu, aliposemezana na baba yake kuhusu maisha aliyopitia, alirudishiwa yote (Luka 15:17-23). Leo mwambie Mungu miaka ya maisha yako. Mungu anasema “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” Isaya 43:26. Kuna haja ya kuhojiana na Mungu, usiwambie watu mwambie Mungu. Yesu akamwambia Yule mwanamke kwenye kisima, kuwa yeye ndio maji yaliyo hai, kama unakiu ya jambo lolote mwambie Yesu Kristo (Yohana 4:14). Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa na njia za kutoka mautini zina yeye!!!!!

The Glory Of Christ Tanzania Church
Ufufuo na Uzima
Dar es Salaam
Tanzania

Sunday, October 28, 2012

SOMO: MKARIBISHE YESU KWENYE CHOMBO CHAKO 28 Oct. 2012

Na Mch.: Mwangasa (RP-Resident Pastor)

Mathayo 14:22-33, Yesu alikuwa akiendelea kutenda kazi alizokuja kuzifanya duniani na ukisoma kuanzia Mathayo 14:1-… Utaona aliwalisha watu elfu tano (waume). Na wakati watu wakitaamaki akawalazimisha wanafunzi wake kupanda chomboni ili wavuke bahari. Wanafunzi wake walipokuwa katikati ya bahari ndipo ilipotokea upepo mkali na kuanza kusukasuka chombo. Tuna mmbo mengi ya kujifunza kupitia maandiko haya:-

HALI YA WANAFUNZI KATIKA CHOMBO:
Ukitafakari kwa makini utaweza kuona hali ya wanafunzi chomboni; inawezekana walishaanza kumlaumu Yesu, au kumlaumu kwa kuwalazimisha kupanda chomboni na yeye asiwemo.

Pia, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamekata tama, kwasababu tukio hili lilipotokea mwanzo walikuwa na Yesu chomboni akaukemea upepo lakini mara hii Yesu hakuwepo chomboni. kwa maana hiyo wanafunzi walikuwa katika hofu kuu.

Biblia inasema hata wanafunzi walipomuona Yesu akitembea juu ya maji, wakahisi ni kivuli chake. hapa tunajifunza kuwa kuna wakati kwenye maisha unaweza kuwa unapita kwenye hatua ngumu kimaisha, na kwasababu ya hofu ukajikuta unaiogopa njia ambayo ndio ufumbuzi wa tatizo lako. 

KWANINI YESU ALITEMBEA JUU YA MAJI:
Yawezekana umejiuliza kwanini Yesu alikuja huku akiwa juu ya maji; Kimsingi bahari ndio ambayo ilikuwa tatizo kwa wanafunzi wake, kwahivyo Yesu alikanyaga bahari kuonyesha kuwa lile tatizo lilikuwa chini ya miguu ya Yesu. Kumbe Yesu yupo juu ya tatizo linalokuzunguka maana lipo chini ya miguu yake.

Na ndio maana Petro naye alijaribu kupita juu ya tatizo yaani bahari lakini alipoiangalia bahari alipata hofu. HAPA tunajifunza jambo kwamba hatakiwi kuliangalia tatizo bali mwangalie Yesu ambaye yupo juu ya tatizo.

Ukimwamini Yesu unavuka kutoka mautini unaingia uzimani, na Yesu ana mamlaka na funguo za mauti na kuzimu. Hivyo ukiwa kwenye tatizo, usiangalie tatizo bali mwangalie Yesu. unapoelekea kwa Yesu usipepese macho, mtazame Yesu aliyekufa msalabani kwaajili yako. 

JAMBO LA KUFANYA UKIWA NDANI YA TATIZO:
Katikati ya bahari wanafunzi wakamuona Yesu kama tumaini lao, na ndipo Petro alipoamua kumfuata. kimsingi uamuzi wa Petro kumfuata Yesu kwa kutembea juu ya maji ni sahihi kabisa, ila tatizo ni kwamba petro alitumia uzoefu wake wa bahari ambao ukamfanya asiwaze sauti ya Yesu aliyemuita. watu wengi wameshindwa kutoka ndani ya tatizo kwasababu ya taarifa walizozisikia kutoka kwa watu. 

Mfano; Mtu ana tatizo la ndoa na ndio limeanza, lakini baada ya kuongea na mtu mwengine mwenye tatizo kama hilo, anamwambia kuwa amedumu kwenye tatizo hilo kwa miaka mingi. Taarifa hiyo moja tu inamfanya huyu ambaye tatizo la ndoa ndio limeanza, akate tamaa na kuingiwa na hofu kabisa kwa kuhisi naye atadumu kwa miaka hiyo yote.

Ni muhimu kujua hakuna haja ya kuangalia tatizo wala watu wengine waliopo kwenye tatizo. tunatakiwa tumuangalie Yesu Kristo ambaye aweza kukutoa kwenye tatizo ulilonalo. unapomwita Yesu kwenye mwili wako uliojaa magonjwa atakapofika yeye yote yatakoma, ukimwita Yesu kwenye ndoa yako yenye matatizo atakapofika tatizo litakama.

Isaya 41:9-10 “wewe niikushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwamaana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” Kama ukijua jambo ambalo Mungu anataka utend kwenye tatizo utalibadili tatizo hilo na kuwa daraja la kukuvusha na kukupeleka kwenye hatma njema ya maisha yako.

Maombi:
Baba Mungu katika Jina la Yesu Kristo leo nimetambua kuwa ninatakiwa nitakiwa nikutazame wewe ninapokuwa kwenye tatizo. ninaomba msamaha kwasababu ya kutazama mambo mengine badala kukutazama wewe Mungu, Mungu naomba unisamehe katika Jina la Yesu. 

Katika Jina la Yesu nimeamua kukuita wewe leo, imeandikwa katika Yeremia 3:33 “niite, nami nitakuitikia, name nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Leo ninakuita katika Jina la Yesu. Mungu kutoka katika kiti chako cha enzi ninakuita katika Jina la Yesu. Ninakutumaini wewe Mungu katika Jina la Yesu. Natakanivuke na wewe Mungu hadi ng’ambo ya maisha yangu katika Jina la Yesu.

MWITE YESU KWENYE TATIZO ULILONALO!!!

Monday, October 8, 2012

UJUMBE: NGUVU YA MSAMAHA

Na Mchungaji Yekonia Bihagaze (RP)     Jumatatu 8.10.2012
 
UTANGULIZI:
Mwisho wa somo ili utagundua nguvu iliyopo nyuma ya kusamehe. Kuna watu wanapitia kwenye matatizo na magonjwa kwasababu ya kutokusamehe.
Mathayo 6:9-12  “basi ninyi salini hivi…12 msipowasamehe wengine makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”  Zaburi 103:3 Hapa tunaona kuwa kanuni ya Mungu ni kusamehe kwanza kabla ya kuponya. Na ndio maana waweza kumwona mtu anasema ameokoka lakini bado yupo kwenye ugonjwa kwasababu ya kutokusamehe.
 
KWANINI UMSAMEHE ALIYEKUKOSEA:
Kumsamehe mtu aliyekuumiza sio jambo la mzaha, na ndio maana kuna watu wanasema kuwa wamesamehe lakini ndani ya mioyo yao bado hajasamehe.  Tunatakiwa kusamehe kwasababu kuna nguvu iliyopo nyuma ya mtu aliyekukwaza au kukuumiza.
Watu wengi wanashindwa kusamehe kwasababu hawajui nguvu  iliyopo nyuma ya yule mtu aliyewakwaza. Emu tuangalie mfano wa gari; Gari linapomgonga mtu serikali haishtaki gari bali anayeshtakiwa ni dereva. Vivyohivyo ukiumizwa unatakiwa uangalie ile nguvu iliyopo nyuma ya aliyekuumiza. Kimsingi kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya aliyekuumiza na usipoijua hiyo nguvu utajikuta unashindwa kusamehe.
 
VITU VITATU AMBAVYO NI VIPIMO KAMA UMESAMEHE AU BADO HUJASAMEHE:
1.       Ukimsamehe mtu utamwongelea vizuri:
Kama kweli umemsamehe mtu utamwongelea vizuri mbele za watu, kama unasema umemsamehe mtu alafu bado unamwongelea vibaya ujue bado hujasamehe kutoka moyoni mwako. Ukimkuta mtu anaongea mabaya kuhusu mtu aliyemkwaza basi ujue ndani ya moyo wake kuna madabahu ya makwazo na machungu. Na kwasababu hiyo kuna watu wamefukuzwa kazi, wamepigwa kwasababu ya kushindwa kuwanenea watu mazuri.
 
2.       Ukimsamehe mtu utamwombea:
Ishara nyingine kuwa ya kuonyesha kuwa umesamehe ni kumwombea mwingine mazuri; na ndio maana Eliya alipotaka kujenga madhabahu ya  Mungu alibomoa kwanza madhabahu ya baali, hata leo huwezi kujenga madhabahu ya Mungu ya amani kama bado moyoni unamadhabahu ya kutokusamehe. Watu wengi wamejikuta wakiomba mabaya kwa watu waliowakosea na kwa namna hiyo wanashindwa kupokea majibu ya matatizo yao.
 
3.       Ukimsamehe mtu utawasiliana kwa uzuri:
Ukimsamehe mtu utawasiliana naye kwa uzuri, nah ii ni kwenye madhabahu ya moyo wako. Hata kama amekujibu vibaya wewe mjibu kwa uzuri. Ni kweli kuwa ukisamehe Yule mtu atakudharau lakini ni muhimu kujua kuwa tunasamehe si kwa ajili ya waliotukosea bali kwa ajili yetu.
 
Watu wengi wanashindwa kusamehe kwasababu ya kukosa nguvu ya uwezesho ya kuweza kusamehe. Kila mtu aliyeokoka anayo nguvu ya uwezesho ya kusamehe, nayo ni Roho Mtakatifu. Kila mtu aliyeokoka ana Roho Mtakatifu naye hutuwezesha kusamehe, kuokoka kunakupa nguvu ya uwezesho kusamehe. Bila kusamehe huwezi kupokea kutoka kwa BWANA.
MAOMBI YA KUSAMEHE:
Baba katika Jina la Yesu Kristo ninaomba nguvu ya msamaha wako; leo nimetambua kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya mtu aliyenikwanza, leo ninawasamehe wote walionikwaza katika Jina la Yesu. Ninatangaza msamaha, ninavunja madhabahu ya makwazo na kutokusamahe ndani yangu katika jina la Yesu Kristo.
Baba ninaomba uniponye na matatizo yaliyoingia ndani yangu kwasababu ya kutokusamehe katika Jina la Yesu. Leo ninabadilika katika Jina la Yesu. Mimi ni mzima na nimeponywa katika Jina la Yesu.
UFUFUO NA UZIMA (THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH)
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.